Ushirikiano na mivutano kati ya China na Marekani

    • Author, Laura Bicker
    • Nafasi, BBC

Marekani na China zimeongeza mazungumzo yao ya mara kwa mara ili kuepusha mizozo katika Bahari ya China Kusini, licha ya uhusiano wao wenye ushindani.

Balozi wa Marekani nchini China alitoa tangazo hili katika mahojiano na BBC.

Mapema wiki hii, mwandishi wa BBC China Laura Vicker alimhoji Balozi Robert Nicholas Burns kuhusu uhusiano wa Marekani na China.

"Wanajeshi wa Marekani na China wanafanya kazi kwa ukaribu katika Bahari ya Kusini ya China na Mlango wa Bahari wa Taiwan," anasema Burns.

Bahari ya China Kusini imekuwa kitovu cha mvutano, huku madai ya China yakizidisha mvutano kati ya Taiwan, Ufilipino na hata Marekani, taifa rafiki ambalo linaunga mkono nchi zote mbili.

Meli kutoka China na Ufilipino zimekuwa zikifanya safari ya hatari katika maji yanayogombaniwa katika miezi ya hivi karibuni.

Katika mvutano wa wiki hii, walinzi wa pwani ya China waliripotiwa kupanda meli ya Ufilipino na kuwashambulia wanajeshi kwa mapanga na visu.

Pia unaweza kusoma

Kunyoosheana vidole

Marekani, kwa upande mwingine, imeanzisha mashirikiano mengi ya kijeshi na nchi kama vile Ufilipino na Japan, na imeahidi kulinda haki za washirika wake katika Bahari ya Kusini ya China.

Na hii inasababisha kuzorota zaidi kwa uhusiano kati ya Marekani na China. Uhusiano wa Marekani na China tayari umetikiswa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mvutano kati ya China na Taiwan, na vita vya kibiashara.

Balozi Burns alikiri kwamba masuala haya yanasalia kuwa chanzo cha "mgawanyiko" kati ya nchi hizo mbili. Kwa upande mwingine, anasema ni muhimu kufanya jitihada za "kuwaleta watu pamoja" katika maeneo ambayo inawezekana.

"China imekubali kuongeza mawasiliano ya kijeshi na Marekani. Hili ni muhimu sana kwetu. Mawasiliano ni muhimu, ni jambo lisiloepukika kabisa kwani ajali na kutoelewana kutasababisha migogoro.”

Ingawa hali ya wasiwasi imepungua, uchaguzi ujao wa rais wa Marekani mwezi Novemba unaweza kwa mara nyingine kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

"Tumeionya China kutoingilia uchaguzi wetu kwa njia yoyote ile," Burns anasema, akiongeza kuwa "ana wasiwasi sana juu ya uwezekano huo.’’

Shirika la Upelelezi (FBI), lilionya kwamba China itaendelea kutafuta kuigawanya Marekani na kushiriki kueneza habari za uongo mtandaoni.

Balozi Burns anasema FBI pia ina ushahidi wa "mashambulizi ya mtandao kutoka serikali ya China dhidi ya Marekani.”

Serikali ya China siku zote imekuwa ikikanusha madai ya vita vya mtandaoni vinavyofadhiliwa na serikali na kusema China pia ni mwathirika wa uhalifu huo.

Rais Joe Biden na Rais wa zamani Donald Trump wanashindana katika misimamo yao mikali kuhusu China, wakiamini kufanya hivyo kutawapa kura.

Mwezi Mei, Rais Biden alitangaza ushuru mpya kwa magari ya umeme yaliyotengenezwa na China (EVs) na paneli za umeme wa jua.

Ingawa kuna magari machache sana yanayoingizwa nchini Marekani kutokea China. Lakini Balozi Burns anasema, “siasa za ndani hazikuhusika kwenye kutoa uamuzi huu.”

Balozi alielezea ushuru huo ni "hatua ya kiuchumi" ya kulinda kazi za wa-Marekani. Nayo, China imeonya inaweza kuweka ushuru wa kulipiza kisasi.

Ushirikiano wa panda shuka

Kabla ya mahojiano ya BBC, Balozi Burns alihudhuria mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa ulioandaliwa na China.

Marekani na China, nchi zinazoongoza kwa uchafuzi wa mazingira duniani, zinajaribu kutafuta njia za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.

"Mazungumzo mengine ya ngazi ya juu kati ya serikali hizo mbili yanafanyika ili kuzuia dawa ya kulevya ya opiate fentanyl kuingia Marekani, Burns alielezea mazungumzo hayo ni muhimu sana.

Nchi hizo mbili pia ziliahidi kukuza mabadilishano ya wanafunzi. Haya yanajiri baada ya idadi ya wanafunzi wa Marekani wanaosoma nchini China kupungua kutoka 15,000 mwaka 2011 hadi 800.

Rais Xi anataka kukaribisha wanafunzi 50,000 wa Marekani kusoma China katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakati wa ziara yake huko San Francisco Novemba mwaka jana, Xi alisema hilo ndilo "tumaini la mwisho la ushirikiano kati ya watu wetu."

Lakini Burns anaituhumu serikali ya China kwa kutochukua maneno hayo kwa uzito. "Tangu mkutano wa kilele wa San Francisco, vikosi vya usalama na wizara za serikali, zimezuia raia wa China kushiriki katika programu za umma za kidiplomasia kupitia balozi.

Na wamezuia raia wa China kusafiri kwenda Marekani kushiriki safari za pamoja. Imekuwa kazi nguvu kuwaleta watu wa nchi hizi mbili pamoja.

Wakati huo huo, wanafunzi na wasomi wa China pia wameripoti kutendewa vibaya na maafisa wa mipaka wa Marekani.

Ubalozi wa China mjini Washington umedai, serikali ya Marekani imewahoji na kuwanyanyasa wanafunzi kadhaa wa China bila sababu za msingi, licha ya kuwa na vibali halali vya kusafiri.

Vilevile, China inaishutumu Marekani kwa kubatilisha viza na hata kuwarudisha nyumbani wanafunzi kadhaa kutoka China.

Marekani kwa upande wake imetoa onyo kwa wanaotaka kusafiri kwenda China, watafakari upya safari zao.

Balozi Burns alitetea onyo hilo kama hatua ya tahadhari na haina dhamira ya kukinzana na sera ya Marekani ya "kuwaleta watu pamoja."

"Kuna Wamarekani waliofungwa nchini China ambao naamini waliwekwa kizuizini isivyo haki na kufunguliwa mashitaka isivyo haki. Ninawatembelea waliozuiliwa na kutoa wito waachiliwe huru."

Balozi huyo anasema Wamarekani kadhaa wamepigwa "marufuku kutoondoka" China, huku pasi zao za kusafiria zikichukuliwa katika viwanja vya ndege na kushindwa kuondoka nchini.

China kwa upande mwingine, imeiondoa Marekani kwenye orodha yake ya nchi ambazo hazina haja ya viza kwa safiri ya hadi siku 15. Lakini Australia imewekwa kwenye orodha hii kwa sababu ya kurejeshwa uhusiano wa nchi hizo.

Mpango wa mabadilishano ya watu ni rahisi katika utekelezaji, lakini kwa nchi hizi mbili umekuwa mgumu, na ni ushahidi wa ukosefu wa kuaminiana kwa pande zote mbili.

Vita nchini Ukraine

Mgawanyiko mkubwa kati ya Marekani na China ni vita vya Ukraine. Marekani inaonekana kuamini kuwa China inashikilia ufunguo wa kuizuia Urusi kusonga mbele.

Balozi Burns alirudia msimamo wa Marekani kwamba haikubaliki kwa China kuunga mkono vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

"China inaonyesha rangi yake halisi, inamuunga mkono Rais Putin na Urusi katika kuendesha vita hivi vya kinyama dhidi ya raia wa Ukraine.”

Balozi huyo pia alidokeza, kuna maelfu ya makampuni ya Kichina yanayounga mkono Urusi.

"Marekani tayari imeweka vikwazo kwa makampuni mengi ya China na iko tayari kuchukua hatua za ziada ikiwa Beijing haitarudi nyuma."

Matamshi hayo yanalingana na kauli zilizotolewa katika mkutano wa kilele wa nchi tajiri, G7 nchini Italia wiki iliyopita.

G7 inasema uungaji mkono wa China kwa Urusi unafanya vita nchini Ukraine viendelee. Pia ilitishia kuweka vikwazo vya ziada kwa makampuni ya China yanayoaminika kuisaidia Urusi kukwepa vikwazo vya biashara vya Magharibi.

China imepuuzilia mbali maonyo hayo na kusema, "yamejaa kiburi, chuki na uongo."

Licha ya hayo yote, uhusiano wa Marekani na China umeboreka ikilinganishwa na 2022. Baada ya Spika wa zamani wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi kutembelea Taiwan.

China ilikasirika na kukata mawasiliano yote na Baraza la Mawaziri la Marekani. Mapema mwaka wa 2023, uhusiano ulidorora tena, wakati wa maandalizi ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken nchini China.

Blinken alighairisha ziara yake baada ya Marekani kudungua puto la China lililokuwa likiruka juu ya anga ya Amerika-Kaskazini.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili hatimaye ulitulia baada ya Biden na Xi kukutana San Francisco Novemba mwaka jana.

Balozi Burns anakiri miaka yake miwili ya kwanza nchini China, ilikuwa migumu, akisema kulikuwa na mawasiliano machache na serikali ya China.

Na anasema, “ushindani huu mgumu, utaendelea kwa muda, na anaona mambo yatakuwa magumu mbeleni.”

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla