Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
China ni sehemu ya uchaguzi wa Marekani - lakini ni mgombea mmoja pekee anayeizungumzia nchi hiyo
Marekani na China ni nchi zilizo na uchumi mkubwa zaidi duniani. Wana majeshi yenye nguvu zaidi duniani. Ushindani kati ya Marekani na China, kulingana na baadhi ya wachambuzi wa kimataifa, utakuwa mada kuu ya Karne ya 21.
Lakini kwa sasa, ni mmoja tu wa wagombea urais wa vyama viwili vikuu ambaye anazungumza mara kwa mara kuhusu sera ya Marekani na China - kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara kwa miakakadhaa.
Kulingana na uhakiki wa BBC Verify, mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump ameitaja China mara 40 katika mikutano yake mitano tangu mjadala wa urais mapema mwezi huu. Katika muda wa saa moja tu katika kongamano la ukumbi wa jiji wiki iliyopita huko Michigan, aliitaja nchi hiyo mara 27.
Na anapozungumzia China, Trump anaangazia masuala ya mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani, akiashiria nchi hiyo na taifa hilo la pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, kama aina fulani ya wahujumu uchumi.
Amezungumzia kuhusu ushuru mpya anaopanga kuweka dhdi ya uagizaji kutoka kwa makampuni ya China - na kutoka kwa mataifa mengine - ikiwa atarejea Ikulu.
Amesema anataka kuzuia magari yaliyotengenezwa na China yasiuzwe kwa sababu anaamini yataathiri sekta ya magari ya Marekani. Ameionya China kutojaribu kubadilisha dola ya Marekani kama sarafu ya akiba ya dunia. Na kuilaumu serikali ya China kwa janga la Covid.
Baadhi ya wanauchumi wanatilia shaka ufanisi wa mipango ya ushuru ya Trump na kuonya kwamba hatimaye itakuwa na madhara kwa Wamarekani. Lakini ujumbe wa Trump unaelekezwa kwa wapiga kura wa sekta ya viwanda, ujenzi na usafiri katika majimbo muhimu ya Midwest ambao wameathiriwa moja kwa moja na ushindani kutoka kwa wazalishaji wa China.
Huku hayo yakijiri BBC Verify imebaini kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris hakutaja China hata kidogo katika mikutano yake sita tangu mjadala wa Septemba 10. Ingawa, katika hotuba yake ya Jumatano alasiri huko Pittsburgh, Pennsylvania,aliangazia masuala ya uchumi akitaja nchi hiyo machache.
"Sitasita kuchukua hatua za haraka wakati China itahujumu sheria za barabara kwa gharama ya wafanyikazi wetu, jamii, na kampuni," alisema katika hafla hiyo.
Alipoombwa kutoa maoni yake, msaidizi wa makamu wa rais aliambia BBC kwamba hata kama Harris hatazungumza kuhusu China mara kwa mara, ana rekodi ya kufanya kazi kukabiliana na kile walichokitaja kuwa ni juhudi za China kudhoofisha utulivu na ustawi wa dunia.
Lakini linapokuja suala la kujadili China, tofauti kati ya mtazamo wa Trump na Harris ni dhahiri.
Siku ya Jumatatu alasiri, kwenye hafla huko Smithton, mji mdogo wa vijijini magharibi mwa Pennsylvania, Trump alifanya majadiliano na kundi la wakulima wa ndani na wafugaji hususan kuhusu China.
Mji huo ambao huenda uko umbali wa saa moja nje ya Pittsburgh, ngome ya mijini ya Chama cha Democratic, lakini pia unasadikiwa kuwa na wafuasi wa Republican.
Mada ya tukio hilo, iliyoandaliwa na Protecting America Initiative, taasisi ya kihafidhina ilichanganua suala la iwapo "tishio la Chama cha Kikomunisti cha China kwa usambazaji wa chakula wa Marekani linaloongezeka".
Mjadala huo uliishia kuwa mazungumzo ya wazi zaidi kuhusu tishio la China kumiliki mashamba ya Marekani. Wakulima, wafugaji na wasimamizi wa biashara kwenye jopo hilo walilalamikia ushindani kutoka waagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka China na ubora wa bidhaa hizo..
Ingawa rais huyo wa zamani hakutumia muda mwingi kujadili hatari inayoonekana ya umiliki wa Wachina wa mashamba ya Marekani - aliahidi kwamba atamshawishi Rais wa China Xi Jinping kununua bidhaa zaidi za kilimo za Marekani - alisisitiza tena kwamba atatumia ushuru kukinga Uchumi wa Marekani dhidi ya China.
Wakati mmoja, alizungumzia haja ya kulinda sekta ya chuma ya Marekani - ili kujiandaa kwa kukabiliana na hatua yoyote itakayochukuliwa na China.
"Ikiwa tuko kwenye vita, na tunahitaji vifaru vya jeshi na tunahitaji meli na tunahitaji vitu vingine vinavyotengenezwa kwa chuma, tutafanya nini, kwenda China na kuchukua chuma?" Aliuliza. "Sibishi kuna tafauti kati yetu na China, lakini je, wagependa kutuuzia chuma?"
Baadhi ya masuala mazito zaidi kuhusu China wakati wa kongamano hilo yaliachiwa Richard Grenell, mjumbe wa na mshauri mkuu wa Mpango wa Kulinda Marekani.
Alionya kuwa nchi hiyo imefanya kazi "kimya kimya lakini kimkakati" dhidi ya Marekani- haswa wakati Wamarekani walipokerwa na masuala mengine ya ulimwengu.
“Wanawafuatilia wanasiasa wetu wa ndani na wa majimbo; wanafuatilia viwanda vyetu,” alisema. "Hakuna kingine wanchotafuta, wakati mwingine wanafanya hivyo kuimarisha uwekezaji wao."
Grenell, ambaye aliwahi kuwa balozi wa Marekani nchini Ujerumani na kaimu mkurugenzi wa ujasusi wa taifa wakati Trump akiwa madarakani, anachukuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje mtarajiwa - mwanadiplomasia mkuu wa Marekani - ikiwa Trump atashinda uchaguzi wa urais wa Novemba.
Iwapo Harris atashinda, kwa upande mwingine, huenda kusiwe na mabadiliko makubwa kutoka kwa utawala wa sasa wa Biden, hata kama rais wa sasa ametoa matamshi makali ya mara kwa mara dhidi ya ushindani kati ya Marekani na China.
Tangu kuanza kwa urais wake, Joe Biden ameitambua China kama moja ya nchi zenye mamlaka ya kidemokrasia zinazoshindana na nchi zinazoongoza kwa demokrasia duniani katika kile anachoeleza kuwa ni sehemu ya historia ya kimataifa.
Kulingana na kura ya maoni, China iko chini katika orodha ya masuala ambayo wapigakura wa Marekani wanajali - chini ya uchumi, uhamiaji na huduma za afya.
Katika uchunguzi wa hivi majuzi kuhusu suala la Usalama wa Kitaifa wa wapiga kura katika majimbo muhimu yenye ushindani mkali, ni 14% tu waliorodhesha China kama kipaumbele cha juu cha usalama wa kitaifa kwa rais ajaye. Uhamiaji uliongoza orodha hiyo kwa 38%, ikifuatiwa na vita vya Ukraine na Gaza, kwa 28% mtawalia.
Hiyo inaweza kwa kiwango fulani kuelezea kwanini Harris hana nia ya kuzungumzia suala la China jinsi alivyofafanua machoni pa wapiga kura wakati wa mjadala wa urais, akianisha jaribio la Trump kuunganisha sera zake za China, haswa ushuru kwenye mpango wa kiuchumi.
Baada ya tukio la Trump huko Smithton, Bill Bretz, mwenyekiti wa kamati ya kaunti ya eneo la Republican, alisema kwamba ingawa China sio miongoni mwa masuala makuu yanayowapa wasiwasi wapiga kura huko Pennsylvania, ilikuwa muhimu kwa Trump kuizungumzia.
Kama tuzo kubwa zaidi ya uchaguzi iliyonyakuliwa, Pennsylvania labda ndio jimbo kuu katika uchaguzi wa urais wa 2024. Trump na Harris watakuwa na kibarua kigumu kushinda mbio za Ikulu ya White bila uungwaji mko wa jimbo hilo. Kura za maoni kwa sasa zinaonyesha wagombea hao wawili wakiwa kwenye kinyang'anyiro kikali.
"Sehemu kubwa ya watu tayari wameamua watampigia kura mgombea yupi, lakini kuna kundi la watu ambao hawajaamua," alisema.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah