Nyaraka za siri zabainisha vitendo vya vikosi vya usalama vya Iran kuwanyanyasa na kuwaua vijana waandamanaji

Chanzo cha picha, Atash Shakarami
Binti wa Iran alidhalilishwa kingono na kuuawa na wanaume watatu wanaofanya kazi katika vikosi vya usalama vya Iran, hati iliyovuja inayoelezwa kuwa iliandikwa na vikosi hivyo inasema.
Imetupa ramani ya kile kilichotokea kwa Nika Shakarami mwenye umri wa miaka 16 ambaye alitoweka kwenye maandamano ya kupinga serikali mnamo 2022.
Mwili wake ulipatikana siku tisa baadaye. Serikali ilidai kuwa alijiua.
Tumewasilisha madai ya ripoti hiyo kwa serikali ya Iran na vikosi vyake vya ulinzi. Hawakujibu.
Imeandikwa "Siri kubwa", ripoti hiyo ni muhtasari wa kusikilizwa kwa kesi ya Nika iliyokuwa ikishikiliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kikosi cha usalama kinachotetea uanzishwaji wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini humo. Inajumuisha kile inachosema ni majina ya wauaji wake na makamanda wakuu ambao walijaribu kuficha ukweli.
Ina maelezo ya kutatanisha ya matukio nyuma ya gari la siri ambalo vikosi vya usalama vilikuwa vikimzuia Nika. Hizi ni pamoja na:
- Mmoja wa wanaume hao alimdhalilisha alipokuwa ameketi juu yake
- Licha ya kufungwa pingu na kuzuiliwa, alipambana, kurusha mateke na matusi
- Na kwamba hii liliwakasirisha na kumpiga kwa bakora
Kuna hati nyingi bandia za Iran zinazosambazwa, kwa hivyo BBC ilitumia miezi kadhaa kuangalia kwa undani vyanzo vingi.
Uchunguzi wetu wa kina unaonesha karatasi tulizopata zinaonesha mienendo ya mwisho ya binti huyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kutoweka na kifo cha Nika Shakarami kuliripotiwa sana, na picha yake imekuwa sawa na mapambano ya wanawake nchini Iran kwa ajili ya uhuru zaidi.
Maandamano ya mitaani yalipoenea kote Iran katika msimu wa vuli wa 2022, jina lake lilipigiwa kelele na umati wa watu uliokasirishwa na sheria kali za nchi juu ya vazi la lazima (hijab.)
Vuguvugu la Mwanamke, Maisha, Uhuru lilikuwa limechochewa siku chache tu zilizopita na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22, Mahsa Amini.
Alikufa kutokana na majeraha aliyopata akiwa chini ya ulinzi wa polisi kulingana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli baada ya kushutumiwa kwa kutovaa hijab yake ipasavyo.
Katika kisa cha Nika, familia yake iliupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti zaidi ya wiki moja baada ya kutoweka kwenye maandamano.
Lakini viongozi wa Iran walikanusha kuwa kifo cha Nika kilikuwa na uhusiano na maandamano hayo na, baada ya kufanya uchunguzi wao wenyewe, walisema kwamba alikufa kwa kujiua.
Muda mfupi kabla hajatoweka, Nika alirekodiwa jioni ya tarehe 20 Septemba karibu na Laleh Park katikati mwa Tehran, akiwa amesimama kwenye jalala lililokuwa linachoma hijab.
Wengine waliomzunguka waliimba "kifo kwa dikteta", wakirejelea Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Ikielekezwa kwa kamanda mkuu wa IRGC, inasema inatokana na mazungumzo ya kina na timu zake ambazo zilidhibiti maandamano hayo.
Kufuatilia maandamano kulikuwa na vitengo kadhaa vya usalama vya siri.
Hati inasema mmoja wa hawa, Timu ya 12, walimshuku kijana "kiongozi, kutokana na tabia yake isiyo ya kawaida na simu za mara kwa mara alizokuwa akizungumza na simu yake ya mkononi".

Chanzo cha picha, EPA
Timu hiyo ilimtuma mmoja wa watendaji wake kwenye umati, akijifanya kama muandamanaji, ili kuthibitisha kuwa kweli Nika alikuwa mmoja wa viongozi wa maandamano hayo. Kisha, kulingana na ripoti, aliita timu yake kumkamata. Lakini alikimbia.
Shangazi yake hapo awali aliiambia BBC Persian kwamba Nika alimpigia simu rafiki yake usiku huo kumwambia alikuwa akifukuzwa na vikosi vya usalama.
Takribani saa moja ilipita kabla ya kuonekana tena, inasema ripoti hiyo, wakati alipowekwa kizuizini na kuwekwa kwenye gari la timu hiyo, gari ambalo lilikuwa limefunikwa nyuma na halikuwa na alama yoyote.
Nika alikuwa katika sehemu ya nyuma na wanaume watatu wa Timu ya 12, Arash Kalhor, Sadegh Monjazy, na Behrooz Sadeghy.
Kiongozi wa timu yao Morteza Jalil alikuwa mbele na dereva.
Kikundi kisha kilijaribu kutafuta mahali pa kumpeleka, ripoti inasema.
Walijaribu kambi ya polisi ya muda iliyokuwa karibu lakini walikataliwa kwa sababu ilikuwa imejaa.
Kwa hivyo waliendelea hadi kituo cha kizuizini, umbali wa dakika 35 kwa gari, ambao kamanda wake alikubali kumpokea Nika. Lakini basi alibadili mawazo yake.
"Mshtakiwa [Nika] alikuwa akila kiapo kila mara na kuimba," aliwaambia wachunguzi wa ripoti hiyo.
"Wakati huo, kulikuwa na wafungwa wengine 14 wa kike kwenye kituo hicho na maoni yangu ni kwamba anaweza kuwasumbua wengine.
"Nilikuwa na wasiwasi angeweza kusababisha ghasia".
Morteza Jalil kwa mara nyingine tena aliwasiliana na Makao Makuu yake ya IRGC kwa ushauri, inasema ripoti hiyo, na akaambiwa aelekee katika Gereza la Evin la Tehran.
Akiwa njiani, alisema alianza kusikia kelele nyuma yake zikitoka kwenye sehemu ya nyuma ya gari hilo.
Tunajua alichokuwa anasikia, kutokana na ushuhuda ulioainishwa kwenye hati kutoka kwa wanaume wanaomlinda Nika nyuma.
Mmoja wao, Behrooz Sadeghy, alisema mara tu aliporudishwa ndani ya gari baada ya kukataliwa na kituo hicho, Nika alianza kupiga kelele.
"Arash Kalhor aliziba mdomo wake kwa soksi lakini akaanza kuhangaika. Kisha Sadegh [Monjazy] akamlaza na kumkalia. Hali ikatulia," aliwaambia wachunguzi.
"Sijui nini kilitokea, lakini baada ya dakika chache alianza kutukana. Sikuweza kuona chochote, nilisikia tu vishindo vya kupigana."
Lakini Arash Kalhor alitoa maelezo zaidi ya kutisha.
Anasema kwa muda mfupi aliwasha tochi ya simu yake na kumuona Sadegh Monjazy "ameingiza mkono ndani ya suruali yake".
Arash Kalhor alisema baada ya hapo walipoteza udhibiti.
"Hajui ... ni nani aliyekuwa akifanya hivyo, lakini alisikia ... fimbo ikimpiga mshtakiwa [Nika] ... 'Nilianza kupiga teke na ngumi lakini sikujua kama nilikuwa napiga vijana wetu au mtuhumiwa.'"
Lakini Sadegh Monjazy alipinga kauli ya Arash Kalhor, ambayo alisema ilichochewa na wivu wa kitaaluma. Alikanusha kuweka mkono wake katika suruali yake, lakini alisema hawezi kukataa kwamba "alisisimka" alipokuwa ameketi juu yake na kugusa makalio ya Nika.
Alisema hili lilimkasirisha Nika, licha ya ukweli kwamba mikono yake ilikuwa imefungwa nyuma ya mgongo wake, akijaribu kumtingisha ili aanguke.
"Alinipiga teke usoni, kwa hivyo nililazimika kujitetea."
Kutoka kwenye kibanda cha gari, Morteza Jalil aliamuru dereva aondoke.
Alifungua mlango wa nyuma na kugundua mwili wa Nika.
Alisema alisafisha damu kutoka kwenye uso na kichwa chake, "hazikuwa katika hali nzuri".
Hii inalingana na hali ambayo mama yake Nika anasema hatimaye alimpata bintiye katika chumba cha kuhifadhia maiti, na cheti cha kifo cha Nika, kilichopatikana na BBC Persian mnamo Oktoba 2022, ambacho kinasema aliuawa na "majeraha mengi yaliyosababishwa na vipigo na kitu kigumu".
Kiongozi wa timu Morteza Jalil alikiri kuwa hakujua kilichotokea.
"Nilikuwa nikifikiria tu jinsi ya kumhamisha na sikuuliza maswali yoyote kwa mtu yeyote. Niliuliza tu: 'Je, anapumua?' Nadhani ni Behrooz Sadeghy aliyejibu, 'hapana, amekufa'."
Jalil alipiga simu kwa Makao Makuu ya IRGC kwa mara ya tatu.
Mara hii, alizungumza na afisa mkuu zaidi, aliyeitwa "Naeem 16".
"Tayari tulikuwa na vifo katika vituo vyetu, na sikutaka idadi iongezeke hadi kufikia 20," Naeem 16 aliuambia uchunguzi. "Kumleta kwenye kambi hakungetatua matatizo yoyote."
Alimwambia Jalil "kumtupa mitaani". Jalil alisema waliuacha mwili wa Nika katika barabara tulivu chini ya barabara kuu ya Yadegar-e-Emam ya Tehran.
Ripoti hiyo inahitimisha kuwa unyanyasaji wa kijinsia ulisababisha mapigano katika sehemu ya nyuma ya gari, na kwamba mashambulio kutoka kwa Timu ya 12 yalisababisha kifo cha Nika.
"Fimbo tatu na Tasers tatu zote zilitumika. Haijabainika ni pigo gani kati ya hizo lilikuwa baya," inasema.
Ripoti hiyo inapingana na maelezo ya serikali ya kile kilichotokea kwa Nika. Karibu mwezi mmoja baada ya mazishi yake, televisheni ya serikali ilitangaza matokeo ya uchunguzi rasmi, ambao ulisema Nika aliruka kutoka kwenye jengo na kufa.
Picha ya CCTV Ilionesha mtu ambaye ilidaiwa kuwa ni Nika akiingia kwenye jengo la ghorofa, lakini mama yake Nika aliiambia BBC Persian katika mahojiano ya simu kwamba hawezi "kwa hali yoyote ile, kuthibitisha kuwa mtu huyo ni Nika".
"Sote tunajua kwamba wanadanganya," Nasrin Shakarami baadaye aliuambia waraka wa BBC, akijadili madai ya mamlaka kuhusu vifo vya waandamanaji.
Uchunguzi wa BBC Eye haukuhusika tu na maudhui ya ripoti hiyo, lakini kama inaweza kuaminiwa kama kazi ya sanaa.
Wakati mwingine, kile kinachoonekana kuwa nyaraka rasmi za Iran na nyenzo nyingine zinazozunguka kwenye mtandao hubainika kuwa zimeghushiwa.
Hati hizi ghushi nyingi, hata hivyo, ni rahisi kutambua kwa sababu zinatofautiana kwa uwazI, zinaonesha nafasi zenye makosa ya vichwa , herufi zenye makosa makubwa ya kisarufi au tahajia.
Wanaweza pia kujumuisha kauli mbiu rasmi au nembo isiyo sahihi ya mwaka wanaodai kuwa inatoka, au jina la wakala wa serikali au idara, kwa mfano.
Kiashiria kingine ni lugha ambayo hailingani na mtindo mahususi unaoelekea kutumiwa na vyombo rasmi vya Iran.
Hati ambayo uchunguzi wetu ulizingatia ilikuwa na mambo machache kama haya.
Kwa mfano, jeshi la polisi la "Naja" lililonukuliwa katika ripoti hiyo lilijulikana kama "Faraja" wakati huo.
Kwa hivyo, ili kupima zaidi ukweli wa hati hiyo, tulimpa afisa wa zamani wa ujasusi wa Iran ambaye ameona mamia ya hati halali.
Alipigia simu hifadhi ya kumbukumbu ya IRGC, kwa kutumia nambari rasmi inayotolewa kila siku kwa maafisa wakuu wa kijasusi nchini Iran, ili kuangalia kama faili ya kesi ni ya kweli na inahusu nini.
Alipata uthibitisho kwamba kwamba nambari ya ripoti hiyo ilionesha kuwa ni sehemu ya jalada la kurasa 322 kuhusu waandamanaji wanaopinga serikali mnamo 2022.
Ingawa hatuwezi kamwe kuwa na uhakika wa 100%, hii ilitupa imani kuwa ni ya kweli.
Ufikiaji wake wa kipekee kwa IRGC pia ulitusaidia kufafanua fumbo jingine, utambulisho wa "Naeem 16", mtu ambaye aliiambia timu kuutupa mwili wa Nika.
Afisa huyo wa zamani wa ujasusi alifanya hivyo kwa kupiga simu nyingine , wakati huu kwa mtu ndani ya kijeshi la Iran. Aliambiwa Naeem 16 ni ishara ya wito kwa Kapteni Mohammad Zamani, anayehudumu katika IRGC.
Jina hilo limeorodheshwa kama mmoja wa waliohudhuria kikao cha saa tano kuhusu kifo cha Nika ambacho ripoti hiyo inatoa muhtasari.
Tunaweka madai hayo kwa IRGC na serikali ya Iran, lakini hawakujibu chochote.
Tunafahamu kuwa wanaume waliohusika na kifo cha Nika hawakuadhibiwa.

Chanzo cha picha, Social media
Kidokezo cha kwa nini inaweza kuwa hivyo kinaweza kupatikana katika hati yenyewe. Wote wa Timu 12, ambao walikuwa kwenye kikao, wameorodheshwa katika ripoti na kulia kwa majina yao ni kundi ambalo wanatoka: "Hezbollah".
Hili ni wanamgambo wa Iran, Hezbollah, lisilohusiana na kundi la Lebanon.
Hutumiwa na IRGC lakini wakati mwingine hufanya kazi nje ya mamlaka yake, kama ambavyo ripoti inavyoonesha:
"Kwa vile watu waliotajwa hapo juu walikuwa wa vikosi vya Hezbollah, kufuatilia kesi hii zaidi ya kupata ahadi zinazohitajika na dhamana ya usalama haijawezekana," inasema.
Afisa wa IRGC Naeem 16, kwa upande mwingine, alipewa karipio la maandishi, inaongeza.
Takribani waandamanaji 551 waliuawa na vikosi vya usalama wakati wa vuguvugu la Mwanamke, Maisha, Uhuru wa Iran, wengi wao kwa kupigwa risasi, kulingana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli.
Maandamano hayo yalipungua baada ya miezi michache kutokana na ukandamizaji wa umwagaji damu wa vikosi vya usalama.
Kulifuata utulivu wa shughuli za polisi wa maadili wa Iran, lakini msako mpya dhidi ya uvunjaji wa kanuni za mavazi ya Kiislamu ulianza mapema mwezi huu.
Miongoni mwa waliokamatwa ni dada mkubwa wa Nika, Aida.















