Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jenerali Brice Oligui Nguema: Kiongozi wa mapinduzi Gabon ni nani?
Baada ya kumuondoa madarakani Rais wa Gabon Ali Bongo, Jenerali Brice Oligui Nguema alibebwa barabarani na wanajeshi wake huku wakiimba waliimba "Oligui, rais! Oligui, rais!".
Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 48 hakika anaonekana kuwa mtu ukizingatia jinsi alivyoinuliwa juu na shangaliwa na askari. Lakini kwa wengi, ni kiongozi asiyetarajiwa.
Miaka mitano iliyopita, hakujulikana na vile nchini Gabon, kwa sababu alikaa miaka 10 nje ya nchi hiyo baada ya kutimuliwa na familia ya Bongo, ambayo hadi Jumatano ilikuwa imetawala Gabon kwa karibu miaka 56.
Jenerali Nguema aliporudi, alipandishwa madaraka kimya kimya hadi kwenye nafasi ya juu kabisa ya jeshi. Hapa alijitolea siku zake kudumisha utawala wa Rais Ali Bongo.
Kiongozi huyu mpya alizaliwa katika mkoa wa Haut-Ogooué nchini Gabon. Eneo hilo ni ngome ya familia ya Bongo na wengine hata wanasema Jenerali Nguema ni binamu wa Ali Bongo.
Jenerali Nguema alifuata nyayo za babake na kujiunga na taaluma ya kijeshi. Akiwa na umri mdogo sana, alijiunga na kikosi chenye nguvu cha Walinzi wa Republican cha Gabon, baada ya kupata mafunzo ya kwanza katika Chuo cha Kijeshi cha Kifalme cha Morocco cha Meknes.
Afisa huyo kijana aliyejizatiti haraka alivutia umakini wa wakuu wa jeshi na kuwa msaidizi wa rais wa wakati huo Omar Bongo, ambaye alikuwa babake Ali Bongo.
Inasemekana Jenerali Nguema alikuwa karibu sana na Omar Bongo - alihudumu hadi kifo chake mnamo 2009.
"Yeye ni mtu ambaye hakutarajiwa [kuongoza Gabon] kwa wakati huu," Edwige Sorgho-Depagne, mchambuzi wa siasa za Afrika ambaye anafanya kazi na Amber Advisers, aliambia kipindi cha Newsday cha BBC.
"Katika miaka ya 2000, alikuwa mbali na nchi kwa muda... alikuwa karibu kusahaulika."
Ali Bongo alipochukua nafasi ya babake mwaka wa 2009, Jenerali Nguema alifukuzwa kazi. Alianza kile ambacho vyombo vya habari vya ndani vinaonyesha kama "maficho", akihudumu karibu miaka 10 kama afisa wa balozi za Gabon nchini Morocco na Senegal.
Mwanajeshi huyo mwenye bidii alionekana tena kwenye uwanja wa kisiasa wa Gabon mnamo 2018, alipochukua nafasi ya kaka wa kambo wa rais kama mkuu wa ujasusi wa walinzi wa taifa.
Baada ya kuhudumu kwa miezi sita katika nafasi hiyo, Jenerali Nguema alipandishwa cheo na kuwa mkuu wa Walinzi wa Taifa. Alianzisha mageuzi ya kuimarisha kitengo hicho,dhamira yake ya msingi: kudumisha utawala.
Mshiriki wa zamani wa karibu aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba jenerali huyo alikuwa "mtu mwenye maelewano, ambaye hatoi sauti yake, anayesikiliza kila mtu na kutafuta maelewano kwa utaratibu".
Muda mfupi baada ya kuchukua jukumu hilo jipya, Jenerali Nguema alianzisha operesheni dhidi ya ufisadi maarufu "mikono safi", ambayo ililenga kukabiliana na madai ya ubadhirifu unaoongozwa na serikali.
Hata hivyo, Jenerali Nguema mwenyewe alishutumiwa kwa kutumia vibaya pesa za umma.
Katika uchunguzi wa mwaka wa 2020, shirika la kupambana na rushwa la Marekani OCCRP lilidai kuwa Jenerali Nguema na familia ya Bongo walinunua mali ghali nchini Marekani na fedha taslimu. Jenerali huyo alisemekana akutumia dola milioni moja kununua majengo matatu.
Majibu ya Nguema kwa ripoti hiyo? "Nadhani iwe nchini Ufaransa au Marekani, maisha ya kibinafsi ni maisha ya kibinafsi ambayo [yanapaswa] kuheshimiwa".
Miezi minane iliyopita, shirika la habari la taifa la Gabon liliripoti kwamba Jenerali Nguema alithibitisha hadharani uaminifu wake kwa urais wa Ali Bongo, ambao umedumu kwa miaka 14.
Lakini siku ya Jumatano, saa chache baada ya Ali Bongo kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata, jeshi lilitangaza kufuta matokeo na kuchukua hatamu.
Rais akiwa chini ya kifungo cha nyumbani, Jenerali Brice Clothaire Oligui Nguema aliteuliwa kuwa kiongozi wa mpito wa Gabon.
Jenerali huyo ameliambia gazeti la Le Monde la Ufaransa kwamba watu wa Gabon wametosheka na utawala wa Ali Bongo, na kwamba rais huyo hakupaswa kuwania muhula wa tatu.
"Kila mtu analalamikia hili lakini hakuna anayechukua jukumu," alisema. "Kwa hiyo jeshi liliamua kufungua ukurasa."
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Ufaransa zimelaani mapinduzi hayo - ambayo ni ya nane kufanyika Afrika Magharibi na Kati tangu mwaka 2020.
Lakini Jenerali Nguema anaonekana kuungwa mkono na sehemu kubwa ya umma. Pia amefanikiwa kuunganisha jeshi, ambalo limegawanyika kwa misingi ya kikabila.
Akiwa mtu ambaye ametuhumiwa kwa rushwa na kufanya kazi kwa muda mrefu katika utawala wa Bongo, huenda asiwe mwanzo mpya ambao watu wa Gabon wanatazamia.
Hata hivyo, ataandikwa katika vitabu vya historia ya nchi kama mtu "aliyefungua ukurasa".