Maelezo rahisi kuhusu mapinduzi ya Gabon

Jeshi nchini Gabon limetwaa mamlaka na kumueka Rais Ali Bongo, 64, katika kizuizi cha nyumbani.

Unyakuzi huo ulikuja muda mfupi baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa kusema Bw Bongo amechaguliwa tena licha ya malalamiko ya upinzani ya udanganyifu.

Rais Bongo alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2009 kufuatia kifo cha baba yake, Omar Bongo Ondimba, ambaye alitawala nchi hiyo kwa miaka 41.

Gabon ni koloni la hivi punde la zamani la Ufaransa barani Afrika kuwa na mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni baada ya Mali, Burkina Faso, Guinea na hivi karibuni Niger.

Kwa nini kulikuwa na mapinduzi nchini Gabon?

Viongozi hao wa mapinduzi hawakukubaliana na matokeo rasmi ya uchaguzi huo yaliyosema Bw Bongo alishinda kwa takribani thuluthi mbili ya kura.

Upinzani Jumanne ulisema mgombea wake ndiye mshindi halali Albert Ondo Ossa alikuwa ameshinda, na pia walisema kumekuwa na wizi mkubwa.

Maafisa hao wa jeshi walisema wameamua "kulinda amani kwa kukomesha utawala uliopo" na kuongeza kuwa uchaguzi "haukukidhi masharti ya kura ya uwazi, ya kuaminika na jumuishi kiasi kinachotarajiwa na watu wa Gabon".

Baada ya tangazo hilo, mamia ya watu walijitokeza barabarani kukaribisha mapinduzi hayo.

Gabon iko wapi?

Iko kwenye pwani ya magharibi ya Afrika ya Kati na inajulikana kwa utajiri wake wa maliasili, haswa mafuta na kakao.

Licha ya kuwa na moja ya mapato ya wastani ya juu zaidi ya kila mwaka barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, karibu $9,000 (£7,000) mwaka 2022, kulingana na Benki ya Dunia, zaidi ya theluthi moja ya wakazi wake wanasemekana kuishi katika umaskini.

Kimsingi, utajiri mwingi wa mafuta nchini huenda kwenye mifuko ya watu wachache.

Gabon, nchi yenye ukubwa sawa na Uingereza, inakaliwa na watu milioni 2.4 tu na 90% ya nchi imefunikwa na misitu.

Chini ya Bw Bongo, imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupokea malipo ya kupunguza utoaji wa hewa ukaa kwa kulinda msitu wake wa mvua.

Mpango wa Misitu wa Afrika ya Kati (Cafi) unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa (Cafi) ulitoa zaidi ya $17m (£12m), sehemu ya kwanza ya mkataba wa $150m uliofikiwa mwaka 2019.

Ilikuwa koloni la Ufaransa hadi 1960 na imekuwa na marais watatu tu tangu wakati huo.

Chini ya rais wake wa pili, Omar Bongo, ilikuwa na uhusiano wa karibu sana na Ufaransa chini ya mfumo unaojulikana kama "Francafrique", ambapo serikali ya Gabon ilipata uungwaji mkono wa kisiasa na kijeshi badala ya kufanya biashara.

Lakini mahusiano yalipoa baada ya mwanawe Ali kushinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa mwaka 2009 na mamlaka ya Ufaransa ikaanzisha uchunguzi wa muda mrefu wa ufisadi katika mali ya familia ya Bongo, ingawa hii imetupiliwa mbali.

Mfahamu Ali Bongo

Ali Bongo , shabiki mkubwa wa soka na pia alitoa albamu ya muziki wa funk miaka ya 1970 , muda mrefu kabla ya kuwa rais.

Alizaliwa Alain Bernard Bongo katika nchi jirani ya Congo-Brazzaville mnamo Februari 1959.

Alikuwa bado katika shule ya msingi wakati baba yake, Omar Bongo, alipochukua udhibiti wa Gabon mwaka wa 1967.

Mnamo 1973, watu wote wawili walisilimu na Alain akawa Ali.

Aliandaliwa kurithi mamlaka na aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na mambo ya nje kabla ya kuwa rais baada ya baba yake kufariki.

Mnamo mwaka wa 2018, Ali Bongo alipata ugonjwa wa kiharusi ambao ulimuweka nje kwa karibu mwaka mmoja na kusababisha wito wa kujiuzulu.

Lakini aliwapuuza na akasimama kuchaguliwa tena, uamuzi ambao ulisababisha mgogoro wa sasa.

Je, kuna uhusiano na mapinduzi kwingine barani Afrika?

Ingawa inaonekana kuna kitu cha mtindo katika Afrika inayozungumza Kifaransa, jibu rahisi ni hapana.

Utekaji wa kijeshi huko Burkina Faso, Mali na hivi karibuni zaidi Niger, yote yalichochewa na uasi wa Kiislamu unaoendelea katika eneo la Sahel, zaidi ya maili elfu moja kaskazini.

Nchini Gabon, jeshi linasema liliingilia kati kwa sababu ya udanganyifu katika uchaguzi na rais kukaa madarakani kwa muda mrefu. Hapa, kuna mwangwi wa mapinduzi ya 2021 nchini Guinea.

Hata hivyo, kuona wanajeshi wakitwaa mamlaka mahali pengine kulitia moyo jeshi la Gabon kufanya vivyo hivyo.

Na kujua kwamba Ufaransa ilikuwa imesukumwa nyuma huko Sahel kungeweza kuwafanya wanajeshi kutambua kwamba Wafaransa hawangeingilia kijeshi kumuunga mkono Ali Bongo kama alivyofanya baba yake katika miongo kadhaa iliyopita.