Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jesse Jackson: Mfuasi wa Martin Luther King aliyeipa sura mpya Marekani
- Author, Anthony Zurcher
- Nafasi, North America correspondent
- Author, Sam Woodhouse
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Jesse Jackson, mmoja wa watu muhimu wakati wa harakati za haki za kiraia za miaka ya 1960 nchini Marekani, alijulikana kwa kuwa Mwafrika-Mmarekani wa kwanza kuhamia kutoka uanaharakati hadi siasa za urais kupitia chama kikubwa cha kisiasa.
Akiwa mfuasi wa Martin Luther King Jr., Jackson alijenga kazi yake kwa kuandaa kisiasa na kuboresha maisha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, na akawa nguvu ya kitaifa wakati wa kampeni zake mbili za kuwania Ikulu ya White House.
Ingawa Wamarekani wenye asili ya Afrika wengine waliwahi kuwania urais wa Marekani, Jackson alikuwa wa kwanza kupata mafanikio makubwa katika kura, jambo lililofungua njia kwa waliokuja baadaye, wakiwemo Barack Obama na Kamala Harris.
Katika kipindi cha maisha yake ya kazi, Jackson alijenga harakati iliyolenga kuwaleta pamoja watu wa Marekani wenye asili mbalimbali, kwa ujumbe uliolenga hasa Wamarekani maskini na wafanyakazi wa kipato cha chini.
"Hakuna mwingine katika Democratic Party aliyekuwa akizungumzia demokrasia ya watu wa rangi na makabila mbalimbali," alisema Seneta wa Vermont Bernie Sanders katika tukio lililofanyika Chicago mwezi Agosti 2024 lililomuenzi Jackson. "Harakati hii haikuwa tu kuhusu kutuleta pamoja, bali pia kutuleta pamoja chini ya ajenda ya maendeleo."
Akiwa msemaji mahiri, Jesse Jackson aliwasilisha kwa ufasaha malalamiko ya watu waliokuwa wakijihisi kama raia wa daraja la pili katika demokrasia tajiri zaidi duniani.
Hotuba yake katika Democratic National Convention ya mwaka 1988, iliyomalizika kwa kauli mbiu "keep hope alive" (endelea kudumisha matumaini), baadaye iliakisiwa miongo kadhaa baadaye katika kauli mbiu ya "hope and change" ya kampeni ya urais ya mwaka 2008 ya Barack Obama iliyofanikiwa.
Baada ya kampeni zake za kihistoria za kuwania urais, Jackson alijiweka kama kiongozi mwenye heshima na uzoefu mkubwa ndani ya Democratic Party.
Hata hivyo, miaka yake ya baadaye ilikumbwa na kashfa mbalimbali, zikiwemo kufichuliwa kwa ukosefu wa uaminifu katika ndoa na makosa ya kifedha yaliyomhusisha mwanawe na mrithi wake wa kisiasa, Jesse Jackson Jr., ambaye aliwahi kuwa mbunge kutoka Illinois.
Mwaka 2017, Jackson aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa Parkinson na kwa kiasi kikubwa alijiondoa katika maisha ya umma. Baadaye, utambuzi huo ulibadilishwa na kuwa ugonjwa wa progressive supranuclear palsy, ambao ni ugonjwa wa ubongo unaodhoofisha mwili polepole na una dalili zinazofanana.
Jesse Jackson alizaliwa kwa jina la Jesse Louis Burns tarehe 8 Oktoba 1941 mjini Greenville, katika jimbo la South Carolina, akiwa mtoto wa Helen Burns mwenye umri wa miaka 16. Akiwa hajaoa, mama yake alifukuzwa kutoka kanisa lake la Kibaptisti la eneo hilo baada ya kupata ujauzito, uliotokana na uhusiano na jirani yake aliyeoa mwenye umri wa miaka 33, Noah Robinson.
Jackson alipokuwa na umri wa miaka miwili, mama yake aliolewa na Charles Jackson, ambaye baadaye alimlea kama mwanawe. Jesse Jackson aliendelea kuwasiliana na Robinson, na aliwaona wanaume wote wawili kama baba zake.
Charles Jackson alikuwa mtu wa dini, na mwanawe alilelewa kanisani, ambalo kwa muda mrefu limekuwa kitovu muhimu cha upinzani wa kisiasa wa Waafrika-Wamarekani tangu enzi za utumwa nchini Marekani.
Akiwa anakulia South Carolina, Jackson, kama Waafrika-Wamarekani wengine wote wakati huo, alitenganishwa na majirani zake wazungu kwa misingi ya rangi.
Alilazimika kusoma katika shule tofauti na kuruhusiwa tu katika maeneo maalum ya umma, kama mabasi au migahawa.
Mfuasi wa Martin Luther King
Akiwa shule ya sekondari, Jesse Jackson alifanya vizuri sana, alichaguliwa kuwa rais wa darasa na alifanya vizuri karibu katika kila aina ya michezo ya timu.
Ufadhili wa masomo ya mpira wa miguu katika Chuo Kikuu Illinois ulimsaidia Jackson kufuatilia ndoto zake na kujiondoa katika mazingira yake ya umaskini.
Hata hivyo, baadaye alihama kutoka chuo hicho kilichokuwa na wanafunzi wengi wazungu na kujiunga na chuo cha kihistoria cha watu weusi huko North Carolina, North Carolina A&T State University.
Alisema aliondoka Illinois kwa sababu makocha wake wazungu hawakumruhusu kucheza nafasi ya quarterback katika mpira wa miguu wa Marekani, ingawa maelezo hayo yanapingwa.
Rekodi zinaonesha kuwa timu tayari ilikuwa na quarterback mweusi na kwamba Jackson alikuwa kwenye onyo la kitaaluma kutokana na masomo.
Akiwa mwanafunzi katika North Carolina A&T, Jackson alianza polepole kujihusisha na harakati za haki za kiraia. Mwaka 1960, alikamatwa pamoja na wanafunzi wengine saba baada ya maandamano ya kimya katika maktaba ya umma iliyokuwa inaruhusu wazungu pekee, jambo lililosababisha kuondolewa kwa ubaguzi katika maktaba hiyo.
Miaka minne baadaye, Jackson alihitimu na kuhamia Chicago, ambako alipata mafunzo ya kuwa kiongozi wa kidini na alitambuliwa na Martin Luther King Jr., kiongozi maarufu zaidi wa harakati za haki za kiraia nchini humo.
Kupitia kongamano la Southern Christian Leadership, ambalo Martin Luther King Jr. alilianzisha mwaka 1957 ili kuhimiza hatua zisizo za vurugu katika kutafuta haki ya kijamii na kiuchumi, Jesse Jackson alianzisha mpango ulioitwa Operation Breadbasket. Mpango huo uliwahimiza Waafrika-Wamarekani kununua na kutumia huduma za biashara zilizowapa heshima ya msingi na nafasi za ajira, na kususia zile ambazo hazikufanya hivyo.
Akiwa bado katika miaka yake ya 20, Jackson aliombwa kwanza kuongoza tawi la mpango huo mjini Chicago na baadaye akapewa jukumu la uongozi wa kitaifa.
Mwaka 1968, maisha ya Jackson yalibadilika sana. Alikuwa pamoja na kiongozi wake katika Lorraine Motel huko Memphis, Tennessee, wakati King alipouawa. Muda mfupi kabla ya risasi, King alikuwa ameinama juu akizungumza kwa mzaha na Jackson, aliyekuwa amesimama katika eneo la maegesho chini.
Jackson aliwaambia waandishi wa habari kwamba alimshika kichwa King alipokuwa akifariki, ingawa mashahidi wengine hawakuthibitisha maelezo hayo. Siku iliyofuata, Jackson alionekana kwenye televisheni kwa utata akiwa bado amevaa nguo zilizokuwa na damu ya King, akijitokeza kama mmoja wa viongozi wa harakati za haki za kiraia.
"Tuliamua hatutaruhusu risasi hata moja kuua harakati hii," alisema baadaye.
Jackson, kama King alivyokuwa amefanya miaka kabla ya kifo chake, alianza kuzungumzia matatizo ya Marekani kama yanayotokana siyo tu na ubaguzi wa rangi bali pia na ukosefu wa usawa wa kiuchumi. Mgawanyiko mkubwa, alisema, ulikuwa kati ya wenye mali na wasio nayo.
"Tunapobadilisha tatizo la rangi kuwa mapambano ya tabaka la kijamii," aliwaambia New York Times, "basi mambo yanakwenda kubadilika kabisa."
Miaka mitatu baadaye, mizozo kuhusu uongozi ilisababisha Operation Breadbasket kuvunjika, na Jackson kuanzisha Operation PUSH (People United to Serve Humanity), kundi jipya la haki za kiraia lenye wigo mpana.
Katika miaka iliyofuata, Jackson alikua mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini Marekani. Shirika lake la PUSH liliungwa mkono katika elimu mijini na programu za 'affirmative action' ambazo ziliwahimiza wafanyabiashara kuajiri wafanyakazi weusi.
Kuwania urais
Hata hivyo, alibaki kuwa mtu wa utata, huku akikabiliwa na madai kwamba mara moja alikuwa ametoa maneno yenye chuki dhidi ya Wayahudi, na kama mhubiri aliyepewa cheo na kutokana na ujauzito usiotarajiwa, aliipinga utoaji mimba (abortion).
Suala hilo liliibua mijadala mikali katika siasa za Marekani baada ya uamuzi muhimu wa Mahakama Kuu katika kesi ya Roe v. Wade. Wademokrat, ambao kwa kawaida walishirikiana na harakati za haki za kiraia, kwa kiasi kikubwa waliunga mkono utoaji mimba kuwa halali.
"Binadamu hawawezi kutoa au kuunda maisha peke yao, ni zawadi kweli kutoka kwa Mungu," aliandika mwaka 1977. "Kwa hivyo, mtu hana haki ya kuondoa kile ambacho hana uwezo wa kutoa."
Mwenye utata
Mnamo 1991, Jackson alijaribu kurudia ushindi wake wa Syria, na akatembelea Iraq usiku wa kuamkia Vita vya Ghuba ili kumsihi Saddam Hussein awaachilie mateka wa Magharibi.
Mwaka mmoja baadaye, aliamua kutogombea urais kwa mara ya tatu na, licha ya kutilia shaka sera za Bill Clinton za mrengo wa kati, alimuunga mkono gavana wa zamani wa Arkansas.
Clinton alipojikuta katika hatari ya urais wake baada ya umma kujua kuhusu uhusiano wake na Monica Lewinsky, mwanafunzi wa Ikulu ya White House, alimwomba Jackson aishauri familia yake kuhusu mgogoro huo.
Jackson alisema kwamba, ingawa Clinton alikuwa amesema uwongo kuhusu uhusiano huo, hakustahili kushtakiwa kwa "uhalifu mkubwa". Clinton alikuwa amefanya "uhalifu mdogo", alisema.
Mnamo 2001, Jackson aliitwa hadharani kujibu kuhusu uhusiano wake, ilipobainika kuwa alikuwa na uhusiano na mfanyakazi wake na akazaa mtoto.
Jackson aliahidi kuchukua likizo ili "kufufua roho yangu na kuungana tena na familia yangu", lakini kasi aliyoitumia kurudi kwenye maisha ya umma iliharibu uaminifu wake na baadhi ya makasisi kote Amerika.
Alidumisha wasifu wake unaoonekana sana kwenye vyombo vya habari kuhusu vipindi vya televisheni na misheni za huruma, ambazo baadhi ya wakosoaji walizitaja kama kujitangaza.
Mnamo Machi 2007, Jackson aliahidi kuunga mkono kampeni ya Barack Obama ya kuwa Mwafrika-Mmarekani wa kwanza katika Ikulu ya White House.
Uhusiano kati ya wanaume hao wawili ulikuwa mgumu mwanzoni, baada ya Jackson kumkosoa Obama kwa "kuwadharau watu weusi".
Matamshi yake yalichukuliwa na kipaza sauti kilichokuwa karibu na baadaye Jackson aliomba msamaha kwa "matamshi yake yasiyo na adabu na ya kuumiza".
Lakini, muda mfupi kabla ya Obama kutoa hotuba yake ya ushindi huko Chicago Novemba iliyofuata, kamera ya televisheni ilimuonehsha Jackson akiwa kwenye hadhira huku machozi yakimtiririka.
Wengi wa wale waliotazama walidokeza kwamba mafanikio ya Jackson katika kuongeza idadi ya watu weusi waliojitokeza katika kampeni za awali za urais yalisaidia kuhakikisha ushindi wa Obama.
Baadaye aliunga mkono uamuzi wa rais mpya wa kuunga mkono ndoa za wapenzi wa jinsi moja, akilinganisha hali hiyo na mapambano ya awali dhidi ya sheria nchini ambayo yalikuwa yamezuia ndoa za rangi tofauti.
Ingawa aliendelea kuwa nguvu ya kisiasa, alikabiliwa na msongo wa mawazo nyumbani.
Mwaka 2013, mwanawe mkubwa ,Jesse Jackson Jr, alihukumiwa kwa kutumia pesa za kampeni kufadhili mtindo wake wa maisha na akahukumiwa kifungo cha miezi 30 jela.
Miaka mitano baadaye, Jackson aligunduliwa na ugonjwa wa Parkinson na ikabidi ajiuzulu kama kiongozi wa Rainbow/PUSH, shirika lililounganishwa la vikundi vyake viwili vya awali.
Hata hivyo, baada ya George Floyd, mwanamume Mwafrika-Mmarekani, kuuawa na maafisa wa polisi mwaka 2020, Jackson alisafiri hadi Minneapolis kuomba kufunguliwa mashtaka ya jinai dhidi ya maafisa.
Na alikuwa sauti kubwa akiunga mkono kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan, na ongezeko la mshahara.
Mwaka 2024, Jackson aliomba msamaha wa rais kwa ajili ya kuhukumiwa kwa mwanawe, lakini alikataliwa na Rais wa wakati huo Joe Biden.
Mwaka huo, mwanaharakati huyo mkongwe pia alirudi katika ulimwengu wa kisiasa alioupenda, akijitokeza mara chache katika mkutano wa chama cha Democratic huko Chicago, ambapo chama hicho kilimteua rasmi Kamala Harris kuwa rais.
Wajumbe mashuhuri walitoa heshima kwa mwanaume waliyesema amefanya mengi kuhakikisha mwanamke mweusi ana nafasi kubwa ya kufika Ikulu ya White House. Baadaye Harris alishindwa katika uchaguzi wa 2024 na Donald Trump.
"Tulijifunza kwake," alisema Al Sharpton, mwanaharakati mwenzake mkongwe wa haki za kiraia ambaye alikuwa amefanya kazi na Jackson katika Operesheni ya Breadbasket miongo kadhaa iliyopita.
Pramila Jayapal, mbunge kutoka jimbo la Washington, alihutubia alipokuwa akizungumza kwenye mkutano huo, akisema: "Kwa kila afisa aliyechaguliwa tutamwona kwenye jukwaa hilo, tuko hapa kwa sababu ulituwekea njia."