Falun Gong: China yapiga marufuku madhehebu yasiyoamini dawa

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Danny Vincent
- Nafasi, BBC
Mwanamke aliyesimama bila viatu juu ya mfuko wa plastiki chini ya mwanvuli. Muziki wa ibada, hotuba za kiroho zinasikika katika vipaza sauti wakati yeye akiwa katika taamuli (meditation).
Ni muandamanaji pekee wa madhehebu ya Falun Gong kusimama kupinga wanavyotendewa watu wa madhehebu hayo huko China. Kasimama mbele ya jengo la ofisi ya serikali ya China huko Hong Kong.
Hapo awali, watu wengi walikuwa wakikusanyika hapa kufanya maandamano. Lakini 2020, China ilianzisha sheria ya usalama wa kitaifa huko Hong Kong, ambayo inaruhusu serikali kuwashtaki waandamanaji.
Kwa hivyo, wanachama wa Falun Gong hawathubutu kuandamana hapa. Unapaswa kwenda nje ya nchi ili kupata watu wanaojiita wanachama wa Falun Gong.
Madhehebu ya Falun Gong ni nini?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Wanachama wa Falun Gong wameketi wamekunja miguu kwenye ghorofa ya juu nje kidogo ya Taipei, mji mkuu wa Taiwan.
Wanasoma kwa sauti mafundisho ya Lee Hong Shi, mwanzilishi wa madhehebu haya. Picha ya mwanzilishi huyo inaning'inia ukutani. Maneno yake yanajirudia vinywani mwao.
Katika kisiwa kinachojitawala cha Taiwan, wanachama wa Falun Gong wako huru kutekeleza imani yao bila woga wa kukamatwa.
Lakini Chama cha Kikomunisti cha China kimepiga marufuku madhehebu hayo ya kiroho na kuliita vuguvugu hili kama madhehebu maovu. Ni miongoni miwili imepita tangu tangazo hilo.
Falun Gong inadai wanachama wake wanakabiliwa na mateso nchini China. Wanalazimishwa kufanya kazi na hata kuuawa na kuvunwa viungo. Utawala wa China umekanusha madai hayo, lakini mahakama huru ya kimataifa imeona yana ukweli.
Taarifa ya mahakama hiyo ya mwezi Disemba 2018 inasema, "uvunaji wa viungo vya wafungwa umefanywa kwa muda mrefu nchini China na idadi ya waathiriwa ni kubwa."
Falun Gong inasemekana kuwa ni vuguvugu kubwa zaidi la upinzani dhidi ya serikali ya China.
Dai la Miujiza

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwalimu wa Falun Gong, Liao Wang kutoka Taiwan anasema, "hii ni harakati ya kiroho. Inajumuisha mazoezi na kutafakari."
"Tunamwona kama Mungu," anasema Wang, kuhusu mfanyabiashara mstaafu na mkuu wa madhehebu hayo, Li Hong Zhi. ''Ni kama Yesu au Mtume Muhammad. Tunaamini ana ujuzi mwingi."
Wang na mkewe Chen wamekuwa wafuasi wa Falun Gong kwa zaidi ya muongo mmoja. Chen anasema, "Falun Gong ina miujiza."
Anasema, "nilipata upele mwekundu katika mwili wangu wote, lakini upele ule uliondoka na uchungu ukapotea." Chen anasema, "ninahisi Mwalimu Li ameutakasa mwili wangu. Ninamshukuru sana Mwalimu Li kwa kuponya ugonjwa wangu. Wagonjwa wengi, hata wenye saratani, wameponywa na Falun Gong."
Lakini hakuna ushahidi huru juu ya madai hayo.
Chen anasema, "wanachama wa Falun Gong hawaugui. Mwalimu Lee alituambia ukiugua ni matokeo ya matendo yako. Huna haja ya kunywa dawa kwa kuugua."
Chama cha Kikomunisti cha China kinasema mafundisho hayo ndiyo yanayofanya Falun Gong kuwa hatari. Lakini kundi la Falun Gong linasema serikali imeendesha kampeni ya propaganda ili kuharibu harakati zao.
Wakosoaji wa Falun Gong

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Lakini pia kuna wakosoaji wa mwanzilishi Li Hong Zi na mafundisho ya afya ya madhehebu yake.
Sam (jina limebadilishwa), mshiriki wa zamani wa ibada hiyo, aliambia BBC kwa sharti la kutotajwa jina, "wanajionyesha kama matabibu. Wanatumia ugonjwa kama kipimo cha maisha na kifo ili watu wawaamini.''
Wakati mtu anapopona, husema anapona kimiujiza na mgonjwa huaminishwa hivyo pia. Watu wanapokufa, imani yao huongezeka na wanakuwa waraibu wa ibada hii."
Anasema, "nawajua watu wengi waliokufa bila matibabu. Watu walioponywa au walio hai si kwa sababu ya mafundisho ya Falun Gong, bali ni kwa sababu yao wenyewe."
Wakati Falun Gong ilipoanza kuenea Kaskazini-mashariki mwa China mwaka 1992, mamlaka ya China iliona madhehebu hayo ni muhimu kwa afya ya umma.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, Falun Gong ilidai kuwa ina wafuasi wengi kuliko Chama cha Kikomunisti. 1999, mwanzilishi wake alikadiria kutakuwa na wafuasi milioni 10 ulimwenguni.
Kwa mujibu wa Freedom House, shirika la Marekani, kati ya watu milioni 2 na 4 nchini China wanafuata imani hiyo kwa siri.
Maelfu ya watu waliandamana kupinga uingiliaji kati wa serikali na wakidai serikali inakandamiza wanachama wake. Maandamano hayo yalifuatiwa na msako mkali wa wanachama wake.
Chama cha Kikomunisti kilidai maandamano hayo ni hatari kwa jamii. Lakini wakosoaji wanasema chama hicho kilitishwa na umaarufu na ushawishi wa Falun Gong na kikaazimia kuliondoa kundi hilo.
Utata wa Falun Gong

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Falun Gong inadaiwa kuwa na wafuasi katika nchi 70 duniani kote na mafundisho yake yametafsiriwa katika lugha 40. Lakini hakuna ushahidi kamili wa mahali ilipotokea.
Wang anasema, "tunaamini Chama cha Kikomunisti ni kibaya. Ndiyo maana wanakandamiza sauti ya madhehebu ya Falun Gong."
Chama cha Kikomunisti cha China kimedai madhehebu haya yanakataza kunywa dawa. Lakini kundi hili limekanusha madai haya.
Liao anasema, "katika madhehebu yetu, tunaamini watu tofauti wana sababu tofauti za magonjwa. Hatuwaambii hata kidogo watu wasiende hospitali."
Anaendelea, "ugonjwa ni matokeo ya matendo yetu mabaya. Matendo mabaya hutokana na tabia mbaya za watu. Yaani, jambo ambalo hupaswi kulifanya kimaadili."
Wang anasema, "watu hufariki. Haijalishi wewe ni rais au mtu mwenye madaraka, kila mtu anaumwa. Unakapokuja duniani ndipo inaamuliwa ikiwa utakuwa mgonjwa au la. Kwa hiyo hakuna maana katika kutumia dawa."
Sam anasema, "ukosoaji wa Chama cha Kikomunisti kwa Falun Gong unaweza kuzingatiwa kuwa wa kweli kwa kiasi fulani. Kwa sababu ni vigumu kuamini aina ya mambo wanayoyafanya."
"Falun Gong hujiita kundi la watu wanaojali afya zao na wanataka kufanya mambo yao wenyewe. Wanataka kufanya maendeleo ya kiroho. Lakini Falun Gong ni madhehebu tofauti."
Pia, anamkosoa mwanzilishi wa madhehebu hayo, Hong Zhi, ambaye inaaminika yuko Marekani. Sam sio mkosoaji pekee. Watu wengine wanadai riwaya zao za kisayansi zimechukuliwa na kundi hilo.
Mafundisho ya Falun Gong yanazungumzia juu ya maisha ya nje ya dunia. Wanataka kwenda kwenye ulimwengu wa nje ya dunia.
Liao anasema, "tunaamini tunatoka sehemu mbalimbali. Na makusudio ya kuja hapa ni kufanya mazoezi ili tuweze kurejea tulikotoka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah








