Watu 77 waokolewa kanisani Nigeria wakisubiri ujio wa Yesu

Polisi wa Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polisi wa Nigeria

Polisi nchini Nigeria wamewaokoa watu 77 wakiwemo watoto kutoka kanisa walimokuwa wamefungiwa katika jimbo la Ondo kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Baadhi yao wanaaminika kuwa huko kwa miezi kadhaa.

Msemaji wa polisi alisema wengi wao walikuwa wameambiwa kutarajia Ujio wa Pili wa Yesu Kristo mnamo Aprili na waliacha shule ili kushuhudia tukio hilo.

Uvamizi huo ulijiri baada ya mama mmoja kulalamika kuwa watoto wake hawapo na alidhani walikuwa kanisani.

Polisi wanasema kuwa wanachunguza tuhuma za utekaji nyara wa watu wengi baada ya uvamizi wa Kanisa la Whole Bible Believers katika eneo la Valentino katika Mji wa Ondo.

Mchungaji wa kanisa la Pentekoste David Anifowoshe na naibu wake wametiwa mbaroni huku waathiriwa wakipelekwa chini ya uangalizi wa mamlaka.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mchungaji mmoja kwa jina Josiah Peter Asumosa ambaye ni Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo ndiye aliyewaambia waumini hao kuwa Unyakuo utafanyika Aprili, lakini baadaye akasema umebadilishwa hadi Septemba 2022 na kuwaambia waumini hao watii. wazazi wao pekee katika Bwana," afisa wa habari wa polisi Funmilayo Odunlami alisema.

Kwa ujumla, polisi waliwaokoa watoto 26, vijana wanane na watu wazima 43, aliongeza.

Kuja Mara ya Pili ni imani ya Kikristo katika kurudi kwa Yesu Kristo baada ya kupaa kwake mbinguni kwa Biblia. Unyakuo ni wazo kwamba waumini wa Kikristo watachukuliwa kwenda Mbinguni katika Ujio wa Pili.

Wasiwasi umekuwa mkubwa miongoni mwa Wakristo katika jimbo hilo tangu shambulio baya dhidi ya kanisa lingine.

Takriban watu 50 waliuawa katika shambulizi la risasi na bomu katika kanisa katoliki la St Francis katika mji wa Owo tarehe 6 Juni.

Mamlaka ya shirikisho inashuku wapiganaji wa kiislamu wa Jimbo la Afrika Magharibi kwa walitekeleza mauaji hayo.