HRW yaituhumu China kwa kufunga na kuharibu misikiti

TH

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Kelly Ng
    • Nafasi, BBC NEWS

China inafunga, kuharibu na kubadilisha misikiti, shirika la Human Rights Watch (HRW) linaeleza katika ripoti mpya.

Ukandamizaji huo ni sehemu ya "juhudi za kimfumo" za kukomesha desturi za Kiislamu nchini China, HRW inasema.

Kuna Waislamu wapatao milioni 20 nchini China - chini ya serikali ambayo haiamini uwepo wa Mungu lakini inasema inaruhusu uhuru wa kidini.

Hata hivyo, waangalizi wanasema kumekuwa na ongezeko la ukandamizaji dhidi ya dini katika miaka ya hivi karibuni - Beijing ikitafuta kuzidhibiti dini zaidi.

Kaimu mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Maya Wang, amesema serikali ya China kufunga, kuharibu na kujimilikisha misikiti ni sehemu ya juhudi za kimfumo za kukomesha desturi za KIislamu nchini humo.

Ripoti hiyo imekuja wakati ushahidi unaoongezeka wa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa Uyghur katika eneo la kaskazini-magharibi la Xinjiang nchini China.

Lakini Beijing inakanusha tuhuma za unyanyasaji. Waislamu wengi wa China wanaishi kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo - Xinjiang, Qinghai, Gansu na Ningxia.

Katika kijiji chenye Waislamu wengi cha Liaoqiao katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Ningxia, misikiti mitatu kati ya sita ilivunjwa minara na makuba yake, kwa mujibu wa HRW. Na misikiti mengine imeharibiwa kumbi za kuswalia – imeongeza ripoti hiyo.

Picha za satelaiti zilizopatikana na HRW zilionyesha kuba la msikiti katika kijiji cha Liaoqiao likibadilishwa na kujengwa kama mnara wa majengo ya zamani ya Kichina kati ya Oktoba 2018 na Januari 2020.

Takriban misikiti 1,300 mjini Ningxia imefungwa au kubadilishwa mwonekano tangu 2020.

Msomi wa masuala ya Waislamu wa China, Hannah Theaker, aliiambia BBC, “idadi hiyo inawakilisha theluthi moja ya misikiti yote katika eneo hilo.”

Unaweza pia kusoma

Ni sehemu ya Sera

dxc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wakitembea mbele ya msikiti usiotumika Xinjiang
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

China ya Rais Xi Jinping na Chama cha Kikomunisti imejikita kuoanisha dini na itikadi yake ya kisiasa na utamaduni wa China.

2018, kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China ilichapisha ikieleza ujumuishaji wa misikiti. Ilizitaka serikali za majimbo "kubomoa zaidi na kujenga michache, na kufanya juhudi kupunguza idadi jumla ya majengo ya aina hiyo.”

Ujenzi, mpangilio na ufadhili wa misikiti lazima yafuatiliwe kwa ukaribu, kwa mujibu na hati hiyo.

Kuna jamii kuu mbili za Waislamu wa China. Huis wametokana na Waislamu waliofika China katika Karne ya 8 wakati wa Enzi ya Tang. Jamii ya pili ni la Uyghur, wengi wao wanaishi Xinjiang.

Takribani theluthi mbili ya misikiti huko Xinjiang imeharibiwa au kubomolewa tangu 2017, kulingana na ripoti ya Taasisi huru ya Sera kutoka Australia.

"Kwa ujumla, Ningxia imekuwa eneo la majaribio la utekelezaji wa sera hii," anasema Dk Theaker. "Ni juhudi za Xi za kubadilisha imani za kidini ili ziakisi utamaduni na jamii ya Wachina.’’

Serikali ya China inadai kupunguzwa kwa misikiti - ambapo mara nyingi hutokea wakati wanavijiji wanapohamishwa au kuunganishwa vijiji - kunasaidia kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa Waislamu.

Lakini baadhi ya Waislamu wa Hui wanaamini ni sehemu ya jitihada za kusimamia uaminifu wao kwa Chama. Baadhi ya wakazi wamepinga hadharani sera hizi, lakini upinzani wao umeambulia patupu. Wengi wamefungwa au kuzuiliwa baada ya kuzozana na viongozi kuhusu kufungwa au kubomolewa kwa misikiti.

"Watu wanapoacha kwenda [misikitini, mamlaka] hutumia hilo kama kisingizio cha kufunga misikiti," anasema Theaker katika ripoti ya Human Rights Watch.

Video nyingine iliyothibitishwa na HRW inaonyesha eneo la kutia udhu katika msikiti wa Liujiaguo kusini mwa Ningxia likibomolewa muda mfupi baada ya kuondolewa kwa minara yake miwili na kuba.

Katika mkoa wa Gansu, unaopakana na Ningxia, maafisa wametoa matangazo ya mara kwa mara ya misikiti kufungwa, kuunganishwa na kubadilishwa mwonekano.

Unaweza pia kusoma

'Chuki dhidi ya Uislamu'

saz

Chanzo cha picha, Getty Images

2018 mamlaka ilipiga marufuku watoto walio chini ya umri wa miaka 16 kushiriki katika shughuli za kidini au kusoma katika mji wa Linxia, mjio huo awali ulijulikana kama Makka Ndogo ya China.

Ripoti ya 2019 ya kituo cha televisheni ya ndani ilisema mamlaka ilibadilisha misikiti kadhaa kuwa "maeneo ya kazi" na "vituo vya kitamaduni."

"Kampeni imepunguza kwa kiasi kikubwa nafasi ya kuwa Mwislamu nchini China, na kuwa na maono ya kizalendo wakati unafuata dini yako.”

"Kampeni inaakisi mwelekeo wa serikali wa chuki dhidi ya Uislamu, kwa kuwa inawahitaji Waislamu kuonyesha uzalendo kupita kitu chochote, na jambo lolote lenye ushawishi wa 'kigeni' linaonekana kama tishio," anasema Dkt. Theaker.

Viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kote ulimwenguni wanapaswa "kuhoji na kueleza wasiwasi wao," anasema mkurugenzi wa Human Rights Watch upande wa Asia, Elaine Pearson.

Jamii nyingine ndogo pia zimeathiriwa na kampeni ya serikali. Mfano; hivi karibuni China imebadilisha jina la "Tibet" na kuweka "Xizang" kwenye hati rasmi za kidiplomasia.

Mamlaka pia imeondoa misalaba katika makanisa, kuwakamata wachungaji na kuziondoa Bibilia katika maduka ya mtandaoni.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah