'Polisi Tanzania haihusiki na utekaji na mauaji'

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika hali inayoendelea kuzua mijadala mikubwa nchini na kimataifa, Jeshi la Polisi Tanzania limesisitiza kutohusika kwake na matukio ya utekaji na mauaji yanayoripotiwa mara kwa mara kutoka nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, jeshi hilo limeeleza kuwa limekuwa likifuatilia kwa karibu taarifa zinazoripotiwa kuhusu watu kutekwa na kupotea huku likihusishwa kuhusika na matukio hayo. Misime amebainisha kuwa uchunguzi wao umeonyesha picha tofauti na madai hayo.

"Katika matukio ambayo yameripotiwa katika vituo vya polisi na uchunguzi wa kina kufanyika na walioripotiwa kupotea kupatikana wakiwa hai au wengine wakiwa wamekufa, hadi sasa ushahidi kwa baadhi ya matukio umeonyesha sababu zake ni kujiteka," amesema Misime.

Misime pia ametaja sababu nyingine za kupotea kwa watu kuwa ni "wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, kugombea mali, kulipiza kisasi, kwenda nchi nyingine kujifunza misimamo mikali, na kukimbia mkono wa sheria baada ya kufanya uhalifu."

Kama mfano halisi, Misime alitaja tukio la Sheikh Zuberi Said wa Singida (53), mwalimu wa dini na kiongozi wa taasisi ya dini iitwayo Islam Foundation, ambapo taarifa zilisambaa kuwa alitekwa na watu waliotajwa kuwa ni askari polisi tarehe 2 Juni 2025 saa 5 usiku akiwa na shilingi milioni 42. Taarifa ya kupotea kwake iliripotiwa polisi.

"Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa Sheikh Zuberi Said hakuwa ametekwa, bali alitengeneza tukio la uongo la kutekwa ili kukimbia madeni aliyokuwa akidaiwa na watu mbalimbali, yenye jumla ya fedha za Kitanzania 521,500,000," alifafanua Misime. Aliongeza kuwa Sheikh Zuberi atafikishwa Mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Historia ya matukio na madai ya wakosoaji

Kwa takribani miaka kadhaa sasa, kumekuwa kukiripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kuhusu matukio mbalimbali ya utekaji na watu kupotea, huku Jeshi la Polisi likihusishwa.

Mbunge wa Kawe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Josephat Gwajima, hivi karibuni alisema kuwa amefanya utafiti wa kibinafsi na kubaini kuwa takribani watu 83 wametekwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Baadhi ya matukio maarufu yaliyoripotiwa hivi karibuni ni pamoja na:

Mdude Nyagali: Mwanaharakati na mfuasi wa Chadema, alivamiwa nyumbani kwake Mbeya Mei 2 na watu wanaodaiwa walijitambulisha kuwa askari polisi, kisha wakamchukua. Hajapatikana hadi sasa.

Edgar Mwakabela (Sativa): Alitekwa mnamo Juni 23, 2024, na kupatikana siku nne baadaye akiwa amejeruhiwa, tukio lililoibua mjadala mkubwa. Mwenyewe akidai Polisi kuhusika, ingawa Polisi inakana.

Ally Mohamed Kibao: Septemba 2024, kiongozi wa Chadema, alichukuliwa kutoka kwenye basi akiwa safarini kwenda Tanga akitokea Dar es Salaam. Alichukuliwa na watu wenye silaha, na baadaye kukutwa ameuawa Dar es Salaam.

Matukio haya ni miongoni mwa yale yanayopigiwa kelele na vyama vya upinzani na wanaharakati, wakieleza yanakiuka haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi na kujieleza, kutokana na baadhi ya wanaotajwa kupotea au kutekwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), na mashirika mengine ya Tanzania na Kenya yamekuwa yakinyooshea kidole Tanzania likiwemo Jeshi lake la Polisi, kuhusu matukio ya utekaji na kupotea kwa watu, ikiwemo wanaharakati na wakosoaji wa serikali. Pia wamezungumzia kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa watu kujieleza, na masuala ya demokrasia.

Mtandao huo pia uliwasilisha kwenye vyombo vya kimataifa visa vya kutoweka kwa wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya, Boniface Mwangi, na Agatha Atuhaire wa Uganda, wakiwa jijini Dar es Salaam kuhudhuria kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, na baadaye kuokotwa kwenye mipaka ya nchi zao.

Serikali yakanusha madai haya kimataifa

Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Balozi Abdallah Possi, amekanusha taarifa hizo akisema ni za upotoshaji na uzushi. Alisisitiza kuwa Tanzania imejidhatiti kulinda haki za binadamu na utawala wa sheria.

Akihutubia wiki hii Mkutano wa tano wa kikao cha 59 cha Baraza hilo, Balozi Possi alisema Tanzania inaheshimu kikamilifu wajibu wake unaotokana na Katiba na mikataba ya kikanda na kimataifa ya haki za binadamu, na kwamba wananchi wana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni hata kama ni kinyume cha msimamo wa serikali.

"Baraza linapaswa kuwa makini dhidi ya madai yasiyo na msingi yanayoelekezwa kwa nchi mwanachama (Tanzania)," Balozi Possi alihoji.

Kauli hizi za serikali na Jeshi la Polisi zinatolewa huku shinikizo la ndani na kimataifa likiongezeka juu ya masuala ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania