Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa chama cha Upinzani Tanzania Chadema atekwa kisha kuuawa, Polisi yathibitisha
Jeshi la polisi nchini Tanzania limethibitisha taarifa za kuuawa kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Ally Mohamed Kibao.
Taarifa za kutekwa zilitolewa na viongozi wa chama cha upinzani siku ya Jumamosi na baadae kusambaa katika mitandao ya kijamii.
‘’Jana Septemba 7,2024 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa juu ya Ally Mohamed Kibao kushushwa kutoka kwenye basi la Tashrif na kuchukuliwa na watu ambao hawakuweza kutambulia na kwamba uchunguzi ulianza baada ya kupokelewa taarifa hiyo. Baada ya kutolewa taarifa za kuonekana mwili wa mtu mwanaume ambaye hakuweza kutambuliwa kwa wakati huo ni mwili wa nani huko Ununio Jijini Dar es Salaam, utambulizi umefanyika kwa mujibu wa taratibu na kubainika ni mwili wa Ally Mohamed Kibao.’’ Inaeleza taarifa ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa katibu wa chama hicho John Mnyika alisema kuwa Mzee Ali kibao alikua safirini aliekea mkoani Tanga kabla ya kuchukuliwa na watu wenye silaha na pingu kisha kumshusha kwa nguvu.
‘’Jana majira ya saa 12 jioni lilitokea tukio ninaliita la kutekwa siyo kukamatwa kwa Mzee Ali Mohamed Kibao ambaye ni mjumbe wa Sekretariati ya Chadema taifa, tukio hilo limetokea maeneo ya Kibo karibu na Tegeta, Mzee Kibao akiwa anasafiri kutoka Dar es salaam kwenda Tanga, basi hilo lilizuiwa na gari mbili, walishuka watu wakiwa na silaha na kumwambia dereva asiondoe basi, kisha kwenda kwenye kiti alichokaa na kumchukua kwa nguvu" Alisema Mnyika’’.
Rais Samia aagiza uchunguzi wa kina
Wakati huo huo rais Samia Suluhu Hassan ameagiza uchunguzi wa kina na wa haraka juu ya tukio hilo.
"Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,"anaandika katika ukurasa wake wa X.
Tukio linakuja huku bado wanaharakati wa watatu wa chama hicho wakiwa hawajulikani walipo.
Matukio ya utekaji yamekua yakiroitiwa kwa wingi katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania.
Tukio la kutekwa kwa kijana Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa mnamo tarehe 23 Juni 2024 na kupatikana siku nne baadae akiwa amejeruhiwa liliibua mjadala mkubwa katika mazungumzo ya ana kwa ana, mitandao ya kijamii na hata katika vyombo vya habari.