Msanii wa Tanzania aliyechoma picha ya rais afungwa jela

Na Wycliffe Muia

BBC

Msanii wa picha nchini Tanzania, aliyetuhumiwa kuchoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au faini ya $2,000 (£1,600) baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mtandaoni .

Shadrack Chaula alikamatwa kwa madai ya kurekodi video ya mtandaoni, iliomuonyesha akichoma picha ya Rais Suluhu huku akimtukana kwa maneno.

Mchoraji huyo mwenye umri wa miaka 24 alikiri kutenda uhalifu huo na kushindwa kutetea hatua yake mahakamani.

Kukamatwa kwake kulizua utata wa kisheria, huku baadhi ya mawakili wakisema kuwa hakuna sheria iliyovunjwa katika kuchoma picha hiyo.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamechangisha fedha ili kulipa faini ya Chaula ili aachiliwe kutoka jela.

Mnamo mwaka wa 2018, Tanzania ilitunga sheria kali dhidi ya kuenea kwa "habari za uwongo", ambazo wakosoaji wanaona kama njia ya kuminya uhuru wa kujieleza.

Polisi wanasema Chaula alitumia "maneno makali" dhidi ya rais katika video aliyoweka kwenye akaunti yake ya TikTok tarehe 30 Juni katika kijiji cha Ntokela, kusini-magharibi mwa jiji la Mbeya.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo Benjamin Kuzaga Jumanne aliwaambia waandishi wa habari kwamba makosa ya msanii huyo ni pamoja na kuchoma picha ya rais na kusambaza maudhui ya kuudhi mtandaoni.

"Sio utamaduni wa watu wa Mbeya kutukana viongozi wetu wa kitaifa," Bw Kuzaga alisema.

Baadhi ya mawakili walisema hakuna sheria inayoharamisha kuchoma picha ya rais.

“Hiyo picha ilipigwa na mpiga picha wa serikali? Wajitokeze hadharani na kueleza athari zao kwa jamii na taifa. Nani anaweza kuonyesha sheria kuwa kuchoma picha ni kosa?” wakili Philip Mwakilima aliliambia gazeti la Mwananchi.

Lakini kitendo hicho, ambacho kinaonekana kutokuwa na maadili nchini Tanzania, kilizua hasira za wananchi.

Siku ya Alhamisi, hakimu Shamla Shehagilo alimpata Chaula na hatia ya kusambaza video kwenye TikTok zilizokuwa na taarifa za uongo zinazokiuka sheria za mtandao za nchi.

Uamuzi wa mahakama

Mahakama iliamua kwamba matendo yake yalihusisha unyanyasaji wa mtandao na uchochezi.

Chaula alinyamaza alipopewa nafasi ya kujitetea dhidi ya mashtaka, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Mwendesha mashtaka alikuwa ameitaka mahakama kutoa adhabu kali dhidi yake ili kuwazuia wengine "kumvunjia heshima" rais.

Kesi hiyo imezua mjadala nchini huku wakosoaji wakisema hukumu hiyo ni kali mno na ni taswira ya hatua ya serikali ya kukabiliana na wapinzani.

Rais Hassan, aliyeingia madarakani mwaka wa 2021, ameanzisha mageuzi ambayo yamefungua uhuru wa kisiasa na kiraia.

Lakini upinzani na makundi ya kutetea haki yameelezea wasiwasi kuwa nchi inarudi nyuma kutokana na sera za ukandamizaji.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla