Je unafahamu ni wakati gani mafuta yanayeyuka mwilini unapofanya mazoezi?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Giulia Granchi
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Watu wengi hufanya mazoezi wakiwa na lengo moja akilini: kuondoa mafuta. Lakini mwili haubadiliki ghafla na kuanza kuyeyusha mafuta papo hapo. Badala yake, unafuata mchakato mrefu wa kutumia nishati ya mwili na hilo hutegemea ukubwa wa mazoezi, muda na mafuta yaliyomo mwilini.
"Hifadhi ya nishati ya mwili ni glycojeni, aina ya glukozi itokanayo na kabohaidreti (wanga), iliyohifadhiwa kwenye misuli na ini," anaelezea Paulo Correia, profesa wa fiziolojia kutoka Chuo Kikuu cha Shirikisho cha São Paulo, huko Brazil.
"Glycojeni inatoa nguvu ya haraka kwa kwa shughuli zinazotumia nguvu za ghafla, kama vile kukimbia mita 100 au kuinua vyuma," anasema Prof Correia.
Glycojeni hutokana na vyakula vya wanga tunavyotumia—ikiwa ni pamoja na vyakula vyenye afya kama vile matunda, mboga mboga na nafaka, na vilevile vyakula visivyo vya afya kama vile vitafunio vyenye sukari, mkate mweupe na soda.
Ingawa aina zote mbili za vyakula hutoa nishati, lakini vyakula visivyo vya afya huwa na kalori nyingi na virutubisho kidogo.
Mafuta hutumika kama hifadhi tunapokula kalori nyingi kuliko tunazotumia. Na huchukua muda mrefu kwa mwili kuvunja kalori hizo ili kuwa nishati inayoweza kutumika.
Ed Merritt, profesa wa mwenendo wa mwili wa binadamu katika Chuo Kikuu cha Southwestern, Texas, anatumia mlinganisho wa mshumaa na kipande cha mti kuelezea mchakato huu:
"Mshumaa unawakilisha mafuta/kalori - unawaka polepole na kwa muda mrefu – kipande cha mti huwaka moto mkali na haraka lakini humaliza haraka. Mwili wetu unafanya kazi kama hivyo. Ikiwa tunahitaji nishati ya haraka, mfano wakati wa mazoezi makali, tunachoma kabohaidreti/glycojen. Lakini ikiwa mahitaji ya nishati ni ya chini, tunachoma zaidi mafuta."
Prof Merritt anasema, mwili hutumia mafuta kama nishati ya kuzalisha nguvu wakati wa kiwango cha chini na cha wastani cha mazoezi.
Mazoezi gani ni bora?
Dhana potofu ni kwamba mazoezi ya kutoa jasho ndiyo njia pekee na ya ufanisi ya kupoteza mafuta. Ingawa ni kweli mazoezi kama vile kukimbia na kuendesha baiskeli huchoma kalori, lakini mazoezi ya kujenga misuli ni muhimu vile vile.
Kujenga uzito wa misuli ni muhimu kwa afya yako jumla, husaidia kuzuia magonjwa sugu kama vile ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa moyo, na mifupa dhaifu.
Ikiwa unafanya mazoezi, ufunguo wa kupoteza mafuta ni kuchoma kalori/mafuta. Mwili huhifadhi mafuta wakati ulaji wa kalori unapozidi zile zinazotumika. Na unapochoma kalori zaidi kuliko unazoingiza mwilini, utapoteza uzito.
"Baada ya kusitisha mazoezi, matumizi ya nishati yanaendelea. Mwili unaendelea kutumia glycogen kutoka katika misuli na ini hadi shughuli mwilini zirudi katika hali ya kawaida," anasema Prof Correia.
Sababu binafsi, kama vile maumbile, umri, na kiwango cha siha, huchangia pakubwa jinsi mtu anavyochoma mafuta kwa ufanisi.
Mazoezi na chakula

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ingawa mazoezi ni muhimu ili kupoteza mafuta, jinsi unavyoongeza mafuta baada ya mazoezi pia inaweza kuwa na athari kubwa.
"Baada ya mazoezi, mwili wako hufanya kazi ya kurudisha glukozi iliyotumia. Usipokula mara moja, mwili wako unaweza kuchukua mafuta yaliyohifadhiwa ili kurejesha kiwango cha mafuta," Prof Merritt aeleza.
Hata hivyo, ikiwa lengo lako ni kuongeza utendaji kazi—iwe ni kuinua uzito zaidi, kukimbia haraka, au kuboresha mazoezi —kula mara tu baada ya mazoezi ni muhimu.
"Inasaidia kwa uponaji, hivyo unaweza kufanya mazoezi kwa bidii tena wakati ujao. Kutegemeana na lengo lako," anaongeza.
Kupunguza ulaji wa wanga kunaweza kusaidia uchomaji wa mafuta na kuleta ufanisi kwa baadhi ya watu. Hata hivyo, ukipunguza wanga wakati unafanya mazoezi utapata matokeo tofauti.
Kiwango cha chini cha wanga kinaweza kusababisha uchovu, udhaifu wa misuli, na hata kupoteza misuli, kwani mwili unaweza kuanza kuvunja tishu za misuli ili kupata glucose wakati mafuta pekee hayawezi kukidhi mahitaji ya nishati ya mwili.
Hilo pia linaweza kudhoofisha mfumo wa kinga, kwani glycogen ina jukumu muhimu katika kutoa kutoa kinga ya mwili.
Kufanya mazoezi hufanya iwe vigumu mwili kuhifadhi mafuta, lakini mazoezi yana mipaka katika uchomaji wa kalori. Kuzingatia ulaji ni jambo muhimu.
"Mafuta huhifadhiwa wakati nishati ya ziada inapoachwa bila kutumika," asema Prof Correia.
Ili kuweka hili katika muktadha, pauni moja ya mafuta ni sawa na kalori 7,000.
Kuendesha baiskeli kwa dakika 30 kunaweza kuchoma hadi kalori 300, lakini kalori hizo zinaweza kurudi kwa urahisi kwa kula tu kipande kimoja cha pizza au keki moja ya choklate.
"Mazoezi ni muhimu kwa afya kwa ujumla, lakini kalori zinazochomwa wakati wa mazoezi zinaweza kurudishwa kwa urahisi na chakula," anahitimisha Prof Merritt.















