Unene unahitaji maana mpya - inasema ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Philippa Roxby
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ripoti kutoka kwa wataalamu inasema, madaktari wanapaswa kuzingatia afya jumla ya wagonjwa wenye mafuta mengi, badala ya kuzingatia tu uzito wa mwili wao.
Ripoti hiyo iliyochapishwa katika jarida la Lancet Diabetes & Endocrinology, inaungwa mkono na zaidi ya wataalam 50 wa matibabu duniani kote.
Ripoti inasema, wale walio na magonjwa sugu yanayosababishwa na uzito wao (clinical obesity), wanapaswa kutambuliwa tofauti na wale wazito lakini hawana matatizo ya kiafya (pre-clinical obesity).
Zaidi ya watu bilioni moja wanakadiriwa kuishi na unene wa kupindukia duniani kote na dawa za kupunguza uzito zinahitajika sana.
Kuunda maana mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
"Unene ni suala mtambuko," anasema Prof Francesco Rubino, kutoka Chuo cha King's College London, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikundi hicho.
"Wengine ni wanene na wanaweza kuishi maisha ya kawaida, na kufanya kazi kama kawaida.
"Wengine hawawezi kutembea vizuri au kupumua vizuri, au wanatumia viti vya magurudumu na wana matatizo mengine makubwa ya kiafya."
Ripoti hiyo inataka "kurekebishwa maana ya" unene wa kupindukia ili kutofautisha kati ya wanene walio na magonjwa na wale ambao ni wanene lakini wana afya zao, ingawa wana hatari ya kupata magonjwa katika siku zijazo.
Katika nchi nyingi, unene unafafanuliwa kwa kutumia kipimo cha BMI (Body Mass Index) - kipimo hicho kinakadiria mafuta ya mwili kwa kuzingatia urefu na uzito.
Ripoti hiyo inasema, kipimo cha BMI hakielezi chochote kuhusu afya jumla ya mtu, na kinashindwa kutofautisha kati ya misuli na mafuta ya mwili au mafuta hatari kwenye kiuno na viungo.
Wataalamu hao wanataka mtindo mpya unaoangalia unene na namna unaoathiri viungo vya mwili - kama vile ugonjwa wa moyo, kushindwa kupumua, kisukari cha aina ya 2 au maumivu ya viungo - na athari ya magonjwa hayo katika maisha ya kila siku.
Wale walio na unene lakini hawana magonjwa, badala ya dawa na upasuaji, wanapaswa kupewa ushauri wa kupunguza uzito, na ufuatiliaji ili kupunguza hatari ya kupata matatizo ya kiafya. Na matibabu pia yanaweza kuhitajika.
Kuuelewa unene
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Unene ni hatari kwa afya," anasema Prof Rubino.
Kuufafanua upya ni jambo jema ili kuongea uelewa kuhusu hatari yake kwa idadi kubwa ya watu.
Kipimo cha unene wa kiuno na urefu wa mtu au kipimo cha moja kwa moja cha mafuta, pamoja na historia ya kina ya mgonjwa, yanaweza kutoa picha iliyo wazi zaidi kuliko kukisia mafuta kutokana na uzito na urefu tu, inasema ripoti hiyo.
Mtaalamu wa masuala ya unene wa kupindukia kwa watoto Prof Louise Baur, kutoka Chuo Kikuu cha Sydney, ambaye alihusika katika ripoti hiyo, anasema mbinu hiyo mpya itawawezesha watu wazima na watoto walio na unene wa kupindukia "kupata huduma zinazofaa zaidi," huku ikipunguza idadi ya watu kupewa matibabu yasiyo ya lazima.
Chuo cha Madaktari cha Royal kinasema ripoti hiyo imeweka msingi thabiti ili unene utibiwe sawa na magonjwa mengine sugu.
Kutofautisha kati ya watu wanene wasio na ugonjwa na watu wanene wenye magonjwa, ni "hatua muhimu" ili kutambua na kuingilia kati mapema" katika kutoa huduma sahihi kwa watu.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












