Kipi hutokea unapoacha kutumia dawa za kupunguza uzito?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dawa za kupunguza uzito zimesaidia mamilioni ya watu kupunguza uzito. Lakini unapoacha kuzitumia, uzito unarudi. Je, hii ina maana gani kwa afya za watumiaji?
Tafiti mbalimbali zimejaribu kuchunguza swala hili, na zote zinaonekana kuelekea kwenye jibu moja, unapoacha kuzitumia uzito hurudi kwa haraka.
Katika utafiti mmoja, karibu watu 800 walichoma sindano za kila wiki za kupunguza uzito zikiambatana na marekebisho ya lishe, mazoezi na ushauri wa kisaikolojia, yote hayo yaliwasaidia kupoteza karibu 11% ya uzito wao kwa miezi minne.
Lakini wakati theluthi moja ya washiriki walipoacha sindano hiyo kwa mwaka mmoja, uzito wa 7% uliopotea ulirudi.
Katika jaribio jingine la 2021. Baada ya wiki 68 za sindano za kupunguza uzito, uzito ulipotea kwa 15%, lakini ndani ya miezi 12 baada ya matibabu kumalizika, uzito wa theluthi mbili kati ya uliopotea ulirudi.
"Kutakuwa na idadi ndogo ya watu, 10% ambao wanaweza kudumisha uzito ambao wameupoteza," anasema Alex Miras, Profesa wa tiba na dawa katika Chuo Kikuu cha Ulster.
Uzito hurudi haraka zaidi kuliko kuondoka. Uzito hurudi katika miezi mitatu hadi sita ya kwanza," anasema Profesa Miras.
Miras anasema hali hii hutokea kwa matatizo yote sugu, kuanzia pumu hadi shinikizo la damu, ugonjwa kwa kawaida hurudia mara tu matibabu yanapokoma.
Tatizo la uzito kurudi

Chanzo cha picha, Getty Images
Nadharia ya kwa nini wagonjwa wengi hupata uzito haraka wanapoacha kutumia dawa ni kwa sababu maeneo ya ubongo yanayohusiana na hamu ya kula bado hayajadhibitiwa, na hivyo kumfanya mtu ale kupita kiasi.
Athari za kisaikolojia za uzito kurudi - kwa sasa ni moja wapo ya jambo linaloumiza vichwa wataalamu kwenye uwanja huu.
Uzito unaporudi na mafuta kuongezeka - yanahusishwa na matatizo mengi kuanzia ugonjwa wa moyo hadi upinzani wa insulini na ugonjwa wa ini.
Miras anasema watu wengi wanaopata uzito baada ya dawa au kubadili mlo hupata mabadiliko katika miili yao na mabadiliko hayo yanaweza kuleta shida zaidi kwa afya kuliko ikiwa wangebaki katika uzito uleule.
Kuuelewa unene
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini sio kila mtu anafaidika na dawa za kupunguza uzito. Utafiti wa 2021 uligundua, karibu 14% ya washiriki walishindwa hata kupoteza 5% ya uzito wao wa mwili, hata baada ya kutumia dawa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Baadhi ya watu wanaweza kupata uzito baada ya kuacha matibabu, lakini bado wanaweza kupata baadhi ya manufaa ya kiafya yatokanayo na kupunguza uzito, kama vile udhibiti wa sukari,” anasema Mkurugenzi wa kituo cha Kudhibiti Uzito na Utafiti, huko Washington, Marekani, Domenica Rubino.
Mara nyingi udhibiti wa sukari utaendelea kwa muda hadi miaka mitatu kulingana na utafiti, na hilo linaweza kuchangiwa na sababu nyingi, anasema Rubino.
"Mtu huyo anaweza kuwa na shughuli zaidi baada ya kupoteza uzito, labda analala vizuri na hayo humfanya kupunguza hatari ya kupata kisukari," anasema.
Utafiti mmoja uliofanywa kwa wanawake walio na shida ya mvurugiko wa homoni na unene wa kupindukia - walitibiwa kwa sindano kwa wiki 16, pamoja na dawa ya kisukari Metformin.
Wakati wa matibabu, wanawake hao walipoteza uzito na kisukari kupungua – na mvurugiko wa homoni zao kukaa sawa.
Miaka miwili baada ya kuacha matibabu, viwango vya homoni zisizohitajika vilibakia chini sana. Hata hivyo, uzito wa washiriki ulirudi kama walivyokuwa wakati utafiti ulianza.
Habari Njema

Chanzo cha picha, Getty Images
Muungano wa Kuboresha Tiba ya Unene huko Ulaya, unaoongozwa na wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Dublin, sasa unajaribu kuchunguza kwa undani zaidi suala hili.
"Iwe ni vipimo vya damu au vipimo vya kisaikolojia - ambavyo vinaweza kutusaidia kuelewa jinsi mgonjwa anavyoweza kutumia dawa hizi kwa usahihi zaidi," anasema Miras.
Jambo moja linaonekana kuwa la hakika, watu wengi walio na unene wa kupindukia - hatimaye watalazimika kuendelea kutumia dawa bila kuacha ili unene usirudi.
Ingawa wasiwasi umeibuliwa juu ya gharama kubwa ya kutibu unene kwa mfumo wa huduma ya afya wa Uingereza.
Lakini kwa kipindi cha miaka miwili ijayo – huku tafiti na uzalishaji ukiongezeka njia mbadala na za bei ya chini zinaweza kufanya tiba hii kuwa rahisi na inayowezekana.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla












