Sio 2024 kwa kila mtu: Nani anayefuata kalenda nyingine na kwa nini?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Mwaka Mpya 2024 umewadia kwa watu wengi, lakini kwa wengine, haujafika au umeshapita. Ukweli ni kwamba tunaingia mwaka 2024 kulingana na kalenda ya Gregorian.
Watu wengi wanasherehekea kuwasili 2024, lakini kuna kalenda nyingine zinazotumika duniani ambazo zinaonyesha mwaka tofauti.
Kalenda ya Gregorian inayokubalika katika nchi nyingi - inafuata mzunguko wa jua, ilianzishwa na Papa Gregory 13 mwaka 1582.
Iliibuka kama marekebisho ya kalenda ya Julian, iliyoundwa na kiongozi wa Kirumi Julius Caesar, ambayo ilikuwa inafuata mzunguko wa dunia kuzunguka Jua, lakini haikuwa sahihi.
Wakati huo nchi nyingi za Kikristo zilisherehekea Mwaka Mpya Machi 25, tarehe ambayo inaashiria kuonekana kwa malaika Gabrieli kwa Bikira Maria, lakini Papa Gregory alianzisha Januari 1 kama mwanzo rasmi wa mwaka mpya.
Hata hivyo, zipo kalenda nyingine zinazotumika duniani.
Kalenda ya Kiyahudi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwa mujibu wa kalenda ya Kiyahudi, tuko mwaka 5784. Mwaka Mpya huadhimishwa mwishoni mwa mwezi Septemba, wakati wa mwezi unaojulikana kama Tishrei.
Kuna kalenda nne tofauti katika Uyahudi, moja imewekwa kwa ajili ya miti. Tishrei inarejelea kumbukumbu ya kuumbwa kwa ulimwengu.
Kalenda ya lunisolar, inazingatia mzunguko wa Jua na Mwezi. Ni desturi ya Wayahudi kuzamisha kipande cha tunda katika asali wakati wa Mwaka Mpya. Lakini pia ni wakati wa toba na kutafakari.
Moja ya mila, inayoitwa Tashlich, inajumuisha kutupa makombo ya mkate ndani ya maji yanayotiririka ili kuashiria utakaso wa dhambi.
Kalenda ya Kiislamu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kulingana na kalenda ya Kiislamu au Hegyric, tuko mwaka wa 1445, ambao ulianza Agosti.
Kalenda ya Kiislamu inaanzia pale Nabii Muhammad alipokimbia mji wa Makka kuelekea Madina.
Ni kalenda inayozingatia mzunguko wa Mwezi. Ndio maana tarehe za ibada zote za Kiislamu zinatofautiana.
Ingawa watu husherehekea Mwaka Mpya wa Kiislamu, kalenda ya Gregorian ndio kalenda rasmi katika nchi nyingi za Kiarabu.
Kalenda ya Kichina

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kama kalenda ya Kiyahudi, kalenda ya jadi ya Kichina pia ni ya jua. Na Mwaka Mpya wa China huangukia tarehe tofauti kila mwaka.
Mwaka 2024, kwa mfano, itaadhimishwa Februari 10. Kila mwaka una jina la mmoja wa wanyama 12 katika mchora wa zodiaki wa Kichina. Mchoro huo una jukumu muhimu katika utamaduni wa China.
Mwaka ujao utakuwa mwaka wa dragoni. Mwaka Mpya wa Kichina pia hujulikana kama tamasha la Spring. Kunakuwa na likizo ya wiki nzima ambayo ilianza zamani sana.
Kalenda ya Korea Kusini
Mwaka Mpya wa Lunar huadhimishwa katika nchi nyingi za Asia, kama vile Korea Kusini. Wakorea Kusini husherehekea Mwaka Mpya mara mbili.
Siku ya kwanza ya kalenda ya jadi ya Kikorea inaitwa Seollal. Kama ilivyo nchini China, ni moja ya likizo kubwa zaidi ya mwaka na itaadhimishwa Februari 10.
Lakini Wakorea Kusini pia husherehekea Januari 1 kama Mwaka Mpya kulingana na kalenda ya Gregorian, iliyopelekwa nchini Korea mwishoni mwa karne ya 19.
India
Nchini India, miaka mipya mingi. Wahindu katika sehemu tofauti za nchi husherehekea mwaka mpya kulingana na kalenda zao - ambazo zinaweza kufuata mizunguko ya jua, mwezi au zote mbili.
Mwaka Mpya wa Kitamil, ambao huadhimishwa hasa katika jimbo la kusini mwa India la Tamil Nadu, kwa kawaida huwa Aprili 14.
Na kwa kawaida huwa karibu au tarehe sawa na Mwaka Mpya wa Kibengali, Kiburma na Kisinhala. Kalenda ya kawaida ya Kitamil inajumuisha mizunguko ya miaka 60.
Kiajemi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwa Wairani, tuko mwaka 1402. Mwaka Mpya wa Kiajemi huadhimishwa siku ya kwanza ya msimu - wakati mwanga wa jua unapopita katika njia ile ile kwenye vizio vyote viwili, na kuufanya mchana na usiku kuwa na urefu sawa (saa 12 kila moja).
Kalenda hii inategemea mzunguko wa dunia kuzunguka jua. Na Mwaka Mpya au Nowruz, ambayo ina maana ya siku mpya katika Kiajemi, kwa kawaida huangukia karibu na Machi 20.
Nowruz imesherehekewa kwa zaidi ya miaka elfu 3, sio tu na Wairani, bali na jamii zingine pia .
Wanaposherehekea wanatayarisha meza iliyopambwa kwa taala saba, na vijana huwatembelea wazee wa familia kwa ajili ya kuwasalimia na kuonyesha heshima.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Esther Namuhisa












