Viumbe sita wanaolala jicho wazi

Kulala huku macho yakiwa wazi huwasaidia wanyama kuwa macho dhidi ya hatari zinazoweza kutokea, na kuwawezesha kujibu mapigo inapohitajika. Ni maisha ya kuvutia ambayo huwaruhusu kupata hitaji la kupumzika na hitaji la usalama katika eneo lao.

Pomboo

Pomboo ni mmoja wa mamalia wanaoishi baharini, anajua jinsi ya kufunga nusu ya ubongo wake. Maana yake ni kwamba analala kwa jicho moja tu huku jicho jingine likiwa wazi.

Pomboo hufanya hivyo ili kujikinga na mashambulizi ya baharini, hasa kutoka kwa sili, ambao wanaelezwa kuwa karibu na maeneo ambayo pomboo wapo. Pomboo ni kati ya wanyama wenye akili. Kwa hakika, viumbe hao wa baharini wanasemekana kuwa wenye akili zaidi baharini.

Mamba

Kundi la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha La Trobe cha Australia na Taasisi ya tafiti za ndege ya Max Planck, wamethibitisha mamba huacha wazi jicho moja na kulala kwa jicho jingine. Jambo ambalo hapo awali liliaminika kuwa hadithi tu.

Mamba hulala nusu ya ubongo jambo linalomwezesha kutazama vitu vinavyomzunguka, ili kupambana na hatari inayomkabili.

Nyangumi

Kulala na jicho moja wazi huruhusu nyangumi kuja juu inapohitajika ili kupata hewa. Pia, huwawezesha kuona na kufuatilia mazingira yao. Wakati jicho moja limelala, jicho jingine linatazama mazingira.

Sungura

Sungura ni wanyama wadogo ambao hulala kwa jicho moja tu, lakini pia hulala kwa macho yote mawili, lakini sio daima.

Wakiwa porini, usingizi wa kufumba jicho moja huwasaidia kuwa macho kujikinga na wanyama wanao wawinda, wakiwemo binaadamu.

Mwari

Ni aina ya ndege, hulala kwa jicho moja tu huku jicho jingine likitazama wawindaji au maadui. Lengo kuu ni kupumzika na kufahamu maadui ambao atakabiliana nao. Ndege wengine wanaolala na macho yao wazi ni njiwa.

Popo

Popo ni wanyama (mamalia), kundi la wanyama wenye uti wa mgongo. Ni mmoja wa wanyama wanaolala jicho likiwa wazi. Jambo jingine la ajabu ni kwamba - hulala mchana na kichwa chake kinaning’inia chini, na hupaa usiku jua linapotua.