Sarafu iliyoporwa yenye thamani ya $1m yarudishwa Israel baada ya kusakwa kwa miaka 20

Coin

Chanzo cha picha, MIRI BAR, ISRAEL ANTIQUITIES AUTHORITY

Ilichukua karibu miaka 20 ya kazi kubwa ya upelelezi na jaribio lililovuka mabara kabla ya suala la kupotea kwa sarafu ya enzi na enzi iliyosalia yenye thamani ya $1m kufungwa.

"Kipande cha historia kinachopendwa [hatimaye] kinarudi nyumbani," afisa mmoja wa Marekani alisema katika hafla ya kuadhimisha tukio hilo. Sehemu hiyo ya historia ni sarafu ndogo ya fedha yenye ishara nyingi, iliyotengenezwa wakati wa uasi wa Wayahudi karibu miaka 2,000 iliyopita.

Iliporwa nchini Israel mwaka 2002, hatimaye ilifuatiliwa, ikakamatwa na inarudishwa ilikotoka. Sakata hilo lilianza pale Mamlaka ya Mambo ya Kale ya Israel (IAA) ilipopata habari kutoka kwa watoa habari kwamba sarafu hiyo ilichukuliwa na Wapalestina kutoka kwenye ghala lililofukuliwa katika Bonde la Ella, kusini mwa Jerusalem.

IAA inasema ilitumia muongo mmoja na nusu uliofuata kujaribu kuitafuta sarafu hiyo, ambayo ilipitia katika masoko haramu ya bidhaa za kale nchini Israel, Jordan na Uingereza. Hatimaye ilisafirishwa kwenda Marekani kwa ajili ya kuuzwa katika mnada huko Denver, Colorado, mwaka wa 2017.

coin

IAA ilikifahamisha Kitengo cha Uchunguzi wa Usalama wa nchi ya Marekani (HSI), ambao kilichukua dhamana ya kiutawala ya sarafu hiyo.

Uchunguzi ukafanyika na kuwasilishwa kwa Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan kupitia Kitengo cha Usafirishaji wa Bidhaa za Kale cha (ATU), ambacho kilipokea amri ya mahakama ya kurejesha sarafu hiyo kulingana na maelezo kutoka kwa watoa taarifa kutoka nchi tano pamoja na usaidizi kutoka kwa mamlaka za Ulaya na Mashariki ya Kati.

Sarafu hiyo ilikabidhiwa siku ya Jumatatu katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan iliyohudhuriwa na maafisa wa Marekani na Israel, akiwemo balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan.

"Leo tunaungana na washirika wetu kurudisha kipande cha nadra sana cha historia ya Israeli, robo ya sarafu ya shekeli, ishara ya uhuru kutoka wakati wa uwepo wa Warumi katika eneo ambalo sasa ni Israeli ya kisasa," afisa wa HSI , Ricky J Patel aliiambia hadhira iliyohudhuria.

Sarafu ya fedha, iliyochorwa kwa michoro ya Kiyahudi, ni moja kati ya sarafu nne tu za aina yake zinazofahamika kuwahi kuwepo. IAA iliipa tarehe ya 69 AD - mwaka wa nne wa vita vya Warumi na Wayahudi (Great Revolt)

Utengenezaji wa sarafu kama hiyo "kwa kweli ilikuwa tangazo la uhuru wa Wayahudi katika ardhi ya Israeli, kauli dhidi ya dola kubwa iliyosimama mbele yao", alisema Ilan Hadad wa IAA.

Vita vya kwanza vya Warumi na Wayahudi vilishuhudia uasi wa Wayahudi dhidi ya utawala dhalimu wa Warumi, ambao walikuwa wamemaliza uhuru wa Wayahudi karne moja nyuma.

Inakadiriwa idadi ya Wayahudi waliouawa katika vita hiyo ilitoka mamia ya maelfu hadi zaidi ya watu milioni moja.