Israel-Gaza: Raia wa Palestina na wanamgambo wauawa huku mapigano yakizuka

Chanzo cha picha, Getty Images
Hali ya taharuki imesalia baada ya usiku wa mapigano makali ya silaha kali kati ya Ukanda wa Gaza na Israel.
Makumi ya makombora yaliyorushwa kutoka Gaza yaliangaza angani, kufuatia mauaji ya takriban watu 10 katika mashambulizi ya anga ya Israel.
Kiongozi wa wanamgambo Tayseer Jabari alikuwa miongoni mwa waliofariki. Israel ilisema mashambulizi hayo yalifuatia "tishio la " kutoka kwa kundi la Palestinian Islamic Jihad (PIJ).
Msichana wa miaka mitano huko Gaza pia alikufa, maafisa wa afya wa eneo hilo walisema, na makumi ya wengine walijeruhiwa.
PIJ ilijibu kwa kurusha zaidi ya roketi 100 ndani ya Israeli usiku mmoja "katika jibu la awali".
Nyingi zilinaswa na ngao ya ulinzi ya makombora ya Iron Dome ya Israeli, lakini ving'ora vilisikika katika miji kadhaa ya Israeli usiku kucha.
Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kimesema kimeanza tena mashambulizi ya roketi dhidi ya maeneo mengi ya wanamgambo huko Gaza, na kuendeleza mashambulizi hadi Jumamosi asubuhi.
Majibizano ya moto ya usiku mmoja yanaashiria ongezeko kubwa zaidi la ghasia tangu vita vya siku 11 vya Mei 2021, ambavyo viliacha zaidi ya Wapalestina 200 na Waisraeli kadhaa kuuawa kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Misri, ambayo imekuwa mpatanishi kati ya pande hizo mbili siku za nyuma, inaripotiwa kujitolea kufanya kazi kama mpatanishi kwa mara nyingine tena ili kuzuia kuongezeka zaidi kwa mapigano.
Maafisa wa Cairo walikuwa wakijiandaa siku ya Jumamosi kukaribisha ujumbe unaowezekana wa wawakilishi wa PIJ kama sehemu ya mchakato huo, vyombo vya habari vya Misri vilisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akizungumzia shambulizi la awali siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid alisema: "Israel ilifanya operesheni sahihi ya kukabiliana na ugaidi dhidi ya tishio la mara moja."
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani Ayelet Shaked alisema: "Hatujui jinsi hali hii itakavyokuwa ... lakini hii inaweza kuchukua muda ... hii inaweza kuwa duru ndefu [ya mgogoro] na ngumu."
IDF ilisema mashambulizi yake yalilenga maeneo yanayohusishwa na PIJ, ikiwa ni pamoja na Mnara wa juu wa Palestina katika Jiji la Gaza ambao ulipigwa siku ya Ijumaa katika mlipuko mkubwa ambao uliacha moshi ukimwagika kutoka kwenye jengo hilo.
Msemaji wa jeshi la Israel anakadiria "takriban wanamgambo 15" waliuawa katika operesheni hiyo.
Maafisa wa afya wa eneo la Gaza wanasema wanamgambo wanne wa PIJ, akiwemo Tayseer Jabari, wameuawa tangu mashambulizi kuanza.
IDF ilisema Tayseer Jabari alikuwa "kamanda mkuu" katika PIJ, na kumshutumu kwa kufanya "mashambulio mengi ya kigaidi" dhidi ya raia wa Israeli.
Alaa Kaddum mwenye umri wa miaka mitano alikuwa miongoni mwa waliouawa katika mashambulio hayo, maafisa wa eneo hilo pia walisema.
Mamlaka ya Gaza ilisema watu wengine 79 pia walijeruhiwa, shirika la habari la AFP linaripoti.
Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa safarini kuelekea mji mkuu wa Iran Tehran, katibu mkuu wa PIJ Ziyad al-Nakhala alisema: "Tutajibu kwa nguvu uchokozi huu, na kutakuwa na mapambano ambayo watu wetu watashinda."
"Hakuna mstari mwekundu kwa vita hivi... na Tel Aviv itakuwa chini ya roketi za upinzani".

Hamas, ambayo inatawala Ukanda wa Gaza, ilisema makundi yenye silaha "yameungana" katika vita na hayatanyamaza.
Mzozo wa hivi punde unafuatia Israel kumkamata Bassem Saadi, aliyeripotiwa kuwa mkuu wa PIJ katika Ukingo wa Magharibi, Jumatatu usiku.
Alishikiliwa katika eneo la Jenin ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa operesheni za kuwakamata watu baada ya wimbi la mashambulizi ya Waarabu na Wapalestina wa Israel na kusababisha vifo vya Waisrael 17 na Waukraine wawili. Wawili kati ya washambuliaji walitoka wilaya ya Jenin.
Baada ya kukamatwa kwa Bassem Saadi, Israel ilionya kuwa PIJ inakusudia kushambulia raia na wanajeshi kwa kulipiza kisasi - na hivyo kuongeza hatua za usalama kwa jamii zinazoishi karibu na mpaka na Gaza.
PIJ, ambayo ni moja ya makundi yenye nguvu zaidi ya wanamgambo wanaoendesha harakati zao huko Gaza, inaungwa mkono na Iran na ina makao yake makuu katika mji mkuu wa Syria Damascus.
Imehusika na mashambulizi mengi, ikiwa ni pamoja na roketi na risasi dhidi ya Israeli.
Mnamo Novemba 2019, Israeli na PIJ walipigana katika mzozo wa siku tano kufuatia mauaji ya Israeli ya kamanda wa PIJ ambaye Israeli ilisema alikuwa akipanga shambulio. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya Wapalestina 34 na wengine 111 kujeruhiwa, huku Waisrael 63 wakihitaji matibabu.
Israel ilisema 25 kati ya Wapalestina waliouawa walikuwa wanamgambo, wakiwemo wale waliogongwa waliokuwa wakijiandaa kurusha roketi.
















