Malkia wa urembo aliyehatarisha maisha yake kuingia Uingereza

Malkia maarufu wa urembo kutoka eneo lililokumbwa na vita la Tigray nchini Ethiopia, Selamawit Teklay, ameelezea masaibu yake ya kuhuzunisha akivuka Bahari kuingia Uingereza kutafuta hifadhi nchini humo.
Bi Selamawit alielekea Ufaransa kwa mara ya kwanza mwaka jana, kabla ya kuhatarisha maisha yake kuvuka Bahari akiwa ndani ya mashua iliyojaa wahamiaji wenzake.
Tigray ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwishoni mwa mwaka 2020, na kusababisha mauaji ya watu wengi, ubakaji wa magenge, na kile ambacho maafisa wa Umoja wa Mataifa walielezea kama hali ya ‘’njaa’’ wakati chakula kinaendelea kuwa haba.
Aliambia Line Tsigab wa BBC Tigrinya kwa nini angewashauri wahamiaji wenzake wasijaribu kuvuka katika vivuko hatari: Nilikuwa na wakati mgumu na wa kutisha kufika Uingereza.
Nimeona ndugu wa Tigraya wakizama baharini.
Mimi ni manusura wa kivuko cha kuingia Uingereza.
Novemba mwka 2021 ni mwezi ambao sitausahau maishani mwangu.
Kwa mara ya kwanza tulilala huko Ufaransa usiku kucha.
Tulikaa vichakani huko Calais kwa takriban majuma mawili.
Baridi ilikuwa kali, hakuna chakula, hakuna maji ya kunywa.
Ilikuwa mateso - mateso yasiyo na mwisho.
Tulisubiri wasafirishaji waje.
Walikuja tofauti.
Tulijadili malipo.
Wanabeba wahamiaji usiku ili kuwatoroka polisi.

Chanzo cha picha, AFP
Katika raundi ya kwanza wakati baadhi ya raia wenzangu wa Tigray walipojaribu kuvuka kivuko hicho, mashua ilizama.
Asante Mungu, waliokolewa na waokoaji.
Wale ambao hatukuvuka tulisikia habari hizo mbaya.
Tulishtuka.
Lakini hatukuwa na chaguo jingine lolote.
Ilibidi twende tulipokusudia.
Katika siku chache, tukahama.
Kulikuwa na baridi kali na bahari ilikuwa hatari.
Tulipanda, kwa wingi, licha ya mashua kuwa ndogo.
Tuliruhusiwa tu kufanya kile ambacho wasafirishaji haramu walituambia.
Tulianza safari yetu ya kwenda Uingereza, ili kuokoa maisha yetu.
Lakini safari yetu haikuwa tu ya gizani.
Ilikuwa imetawaliwa na giza la mauti.
Ghafla injini ya boti ikaharibika na kuacha kufanya kazi tukiwa baharini.
Mwanamume Mwarabu tuliyekuwa naye aliruka baharini ili kujaribu kujiokoa.
Lakini hakuweza.
Kisha mmoja wa ndugu zetu wa Tigrayan akaingia.

Chanzo cha picha, SELAMAWIT TEKLAY
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hakurudi tena!
Tulimtafuta.
Tulimsikia akipiga kelele.
Hatukuweza kumpata.
Tulipiga simu za kukata tamaa kuomba msaada.
Hata hivyo, waokoaji walifika saa tatu baadaye.
Ndugu yetu alizama mbele yangu.
Niliona kifo chake kwa macho yangu.
Yule mwarabu alibahatika.
Alinusurika.
Alifanikiwa kurejea kwenye mashua.
Katika mashua hiyo, nilitambua kwamba uamuzi niliofanya haukuwa sahihi.
Mimi, na wengine walionusurika kwenye njia hiyo hatari, tulijisalimisha kwa walinzi wa pwani ambao baada ya masaa kadhaa hatimaye walitukuta tukielea baharini.
Siku tatu au nne baada ya kufika Uingereza, abiria wa awamu ya tatu walijaribu kuvuka kivuko hicho cha kuingia Uingereza.
Hatukusikia habari njema. Wote walikufa maji. Wenzangu wawili walikuwa miongoni mwa waliofariki.
Mmoja wao, nilimfahamu kutoka mji wangu wa nyumbani, Mekelle.
Nilijililia mwenyewe, nililia watu wangu, na nililia wazazi wangu.
Wazazi wangu hawakujua kwamba nilikuwa naenda katika nchi hii kwa njia hii.
Nilipoanza safari hii, nilijiambia kwamba haiwezi kuwa mbaya zaidi kuliko yale niliyoteseka huko Tigray.
Tumeona mambo ya kutisha nyumbani.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini, kuvuka bahari hii ni hatari sana kiasi kwamba hakuna mtu anayepaswa kujaribu.
Sikuwahi kufikiria kwamba ningeweza kuondoka katika nchi yangu.
Sikuwahi kuwa na hamu yoyote.
Nilipokuwa nikienda nje ya nchi kwa ajili ya mashindano ya urembo au kazi nyinginezo, nilirudi nyumbani kila mara.
Nilikuwa na biashara yangu mwenyewe huko Mekelle ambapo nilibuni na kuuza vitambaa vya asili na vya kisasa.
Wakati huo biashara huko Mekelle ilikuwa ikivuma, kwa hiyo nilikuwa nikifanya vizuri.
Kisha mnamo Novemba 2020, vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu vikaanza.
Tumepoteza sana kwa sababu ya vita hivi.
Imesababisha njaa, ubakaji na mateso yasiyoelezeka.
Akaunti za benki huko Tigray pia zimesimamishwa, na hakuna mtu anayeweza kupata pesa zake.

Uhamisho, taabu na dhiki zimeshuhudiwa katika kila eneo laTigray.
Ilinitokea mimi na familia yangu pia.
Kwa bahati nzuri, sikubakwa kama dada zetu wa Tigray, lakini nimejeruhiwa kisaikolojia.
Kulikuwa na mashambulizi makubwa ya mabomu kwa Mekelle wakati vita vilipoanza.
Tulilazimika kukimbia nyumbani kwetu, na kwenda kukaa katika kijijini.
Mjomba wangu aliuawa katika jiji la Aksum.
Baada ya hapo niliamua kuondoka.
Ninachotamani ni amani. Sijisikii vizuri.
Nimepoteza amani ya ndani.
Ikiwa kuna amani, kila kitu kipo, kila kitu kinaweza kutatuliwa.
Mimi ndiye binti pekee wa wazazi wangu.
Ninakumbuka nilipokuwa mtoto, jinsi nilivyokuwa nikijichagulia mavazi na mitindo ninayotaka.
Nakumbuka wakati nilivaa nguo za mama yangu na viatu vya ncha ndefu.
Nilipotamani kuwa mwanamitindo, wazazi wangu walikuwa wakiniambia niangazie zaidi masomo yangu.
Hata hivyo, tamaa yangu ya uanamitindo ilinishinda.
Nilipokuwa na umri wa miaka 16, nilishiriki katika shindano langu la kwanza la urembo, Miss Virgin Mekelle.
Hilo lilikuwa shindano la kupendeza la urembo.
Nilipokua, nilishiriki shindano kubwa la kitaifa la urembo, Miss World Ethiopia, mnamo 2015. Sikuishia hapo.
Mnamo mwaka 2017, niligombea Miss Grand kimataifa - wawaniaji 77 kutoka kote ulimwenguni walishindania taji huko Vietnam.
Ilikuwa mashindano yangu ya kwanza ya kimataifa ya urembo kuwakilisha nchi yangu.
Nilipata baadhi ya vikombe vya juu katika shindano hilo, ambalo lilifungua upeo mpya wa fursa kwangu.
Kisha nikashiriki katika shindano lingine la urembo duniani kote nchini Korea Kusini, Miss Beauty and Talent, mwaka wa 2018.
Na zaidi ya hayo, mwaka wa 2019 nilishiriki katika shindano la urembo na ujuzi maalum nchini China.
Lakini ndoto zetu zote zimekatishwa.
Sasa mimi ni mtafuta hifadhi nchini Uingereza.
Kwanza walitukaribisha hotelini na sasa walinipa nyumba ya pamoja na pesa za kulipia chakula.
Siruhusiwi kufanya kazi au kuhama nchi hii hadi kesi yangu itakaposhughulikiwa.
Nimeanza maisha upya.
Kila kitu hakikupangwa, kila kitu kinahisi kama mchezo wa kuigiza.
Hivi sasa serikali ya Uingereza inapanga kuwapeleka baadhi ya wanaume wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda.
Uamuzi huo ni wa kusikitisha.
Wahamiaji wamejitolea sana ili kupata maisha salama katika nchi hii.
Nimeona jinsi safari ya gizani inavyoonekana.












