Jinsi watoto walivyonusurika kwa siku 40 katika msitu wa Colombia

vv

Chanzo cha picha, Reuters

Siku ya Ijumaa, usiku wa manane katikati ya msitu wa Colombia, redio za jeshi zilisikika na ujumbe ambao taifa lilikuwa likiomba: "Muujiza, muujiza, muujiza, muujiza."

Kanuni za kijeshi zilifichua kuwa watoto wanne waliopotea msituni kwa siku 40 wote wamepatikana - wakiwa hai.

Vijana hao, wote ni watu wa asili ya kabila la Huitoto, walikuwa wametoweka tangu ndege ndogo waliyokuwa wakisafiria kuanguka kwenye msitu wa Amazon tarehe moja mwezi Mei.

Mkasa huo ulimuua mama yao na kuwaacha watoto hao wenye umri wa miaka 13, tisa, minne na mmoja wakiwa wamekwama peke yao katika eneo lililojaa nyoka, wanyama hatari na mbu.

Hapo awali waokoaji walihofia hali mbaya zaidi, lakini nyayo za miguu, matunda ya mwituni yaliyoliwa kiasi, na vidokezo vingine vya hivi karibuni viliwapa matumaini kwamba watoto hao wanaweza kuwa hai baada ya kuondoka eneo la ajali kutafuta msaada.

Katika muda wa wiki sita zilizofuata watoto walipambana na mambo - yasiyo ya kawaida - katika kile Rais wa Colombia Gustavo Petro alichoita "mfano wa kuishi kiajabu ambao utabaki katika historia".

'Watoto wa jangwani'

Ikiwa kulikuwa na watoto waliotayarishwa vyema kukabiliana na hali kama hiyo, basi ilikuwa watoto wa familia ya Mucutuy.

Watu wa jamii ya Huitoto hujifunza uwindaji na uvuvi tangu wakiwa wadogo, na babu yao Fidencio Valencia aliwaambia waandishi wa habari kwamba watoto wakubwa, Lesly na Soleiny, waliufahamu vizuri msitu huo.

Akiongea na vyombo vya habari vya Colombia shangazi wa watoto hao, Damarys Mucutuy, alisema familia ilicheza "mchezo wa kujinusuru msituni" mara kwa mara kwa pamoja wakikua.

"Tulipocheza, tuliweka kama kambi ndogo," alikumbuka. Lesly mwenye umri wa miaka 13, aliongeza, "alijua ni matunda gani hawezi kula kwa sababu kuna matunda mengi yenye sumu msituni. Na alijua jinsi ya kumtunza mtoto".

Fidencio Valencia aliwaambia waandishi wa habari kwamba watoto hao walikua na ujuzi wa kujitunza msituni.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Fidencio Valencia aliwaambia waandishi wa habari kwamba watoto hao walikua na ujuzi wa kujitunza msituni.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya ajali, Lesly alijenga malazi ya muda kutoka na matawi yaliyounganishwa pamoja kwa kutumia nywele zake.

Pia alipata Fariña, aina ya unga, kutoka kwenye mabaki ya ndege ya Cessna 206 waliyokuwa wakisafiria.

Watoto hao walinusurika kwa unga huo hadi ukaisha wakaanza kula matunda, Edwin Paki, mmoja wa viongozi wa wazawa walioshiriki katika juhudi za kuwatafuta, aliwaambia waandishi wa habari.

"Kuna matunda, sawa na pasheni ichure," alisema. "Walikuwa wakitafuta matunda ya kula kutoka kwa mti wa avichure takriban kilomita moja na nusu kutoka eneo la ajali ya ndege."

Astrid Cáceres, mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Familia ya Colombia, alisema muda wa masaibu yao ulimaanisha "msitu ulikuwa kwenye mavuno" na wanaweza kula matunda ambayo yalikuwa yamechanua.

Lakini bado walikabiliwa na changamoto kubwa za kuishi katika mazingira duni.

Akiongea na BBC Mundo siku ya Jumamosi, mtaalamu wa kiasili Alex Rufino alisema watoto hao walikuwa "katika msitu wenye giza nene sana, ambapo miti mikubwa zaidi katika eneo hilo iko".

Na wakati kuna majani ambayo watoto wanaweza kusafisha maji, alionya kwamba "mengine ni sumu".

"Ni eneo ambalo halijachunguzwa. Miji ni midogo, na iko karibu na mto, sio msituni," aliongeza.

Mbali na kuwaepuka wanyama hatari, watoto hao pia walivumilia dhoruba kali za mvua na huenda walilazimika kukwepa vikundi vilivyojihami vinavyosemekana kuwa na shughuli msituni.

Wakati mmoja, watoto hao walilazimika kujikinga na mbwa mwitu, Rais Petro alisema.

vv

Chanzo cha picha, Reuters

Lakini Bw Rufino alibainisha kuwa mtoto wa miaka 13 aliyelelewa katika jamii ya kiasili atakuwa tayari ana ujuzi mwingi unaohitajika ili kustawi katika mazingira kama hayo.

John Moreno, kiongozi wa kikundi cha Guanano huko Vaupes, kusini-mashariki mwa Colombia ambako watoto hao walilelewa, alisema "wamelelewa na nyanya yao", mzee wa kiasili anayeheshimika sana.

“Walitumia yale waliyojifunza katika jamii, wakitegemea maarifa ya mababu zao ili waendelee kuishi,” alisema.

Uokoaji wa kipekee

Wakati msako ukiendelea, maafisa wa Bogota walipata shinikizo kutokana na ucheleweshaji wake. Rais Petro alikabiliwa na ukosoaji baada ya ofisi yake kuchapisha kwa uwongo ujumbe wa Twitter ukisema watoto hao wamepatikana.

mamlaka ziliangusha vipeperushi 10,000 vilivyo na vidokezo vya jinsi ya kuishi vilivyoandikwa kwa Kihispania na lugha ya asili ya Huitoto, na helikopta zilituma ujumbe kutoka kwa nyanya yao kutoka kwa wazungumzaji ili kuwapa hakikisho watoto waliokuwa wanatafutwa.

Lakini bila vyombo vya habari kujua, jeshi lilikuwa likikaribia kuipata familia hiyo. Mara kadhaa timu za uokoaji zilipita kati ya mita 20 hadi 50 (futi 66 hadi 164) kutoka mahali ambapo watoto walipatikana, kamanda wa utafutaji Jenerali Pedro Sánchez alisema.

Kufikia wakati watoto hao walipopatikana takriban wanajeshi 150 na watu wa kujitolea 200 kutoka vikundi vya wenyeji wa eneo hilo walihusika katika operesheni hiyo, ambayo ilikuwa ikihusisha eneo la zaidi ya kilomita 300 za mraba (maili za mraba 124).

"Huku sio kutafuta sindano kwenye mhimili wa nyasi, ni kiroboto kidogo kwenye zulia kubwa, kwa sababu wanaendelea kusonga," Jenerali Sanchez aliwaambia waandishi wa habari wakati wa msako.

Lakini siku ya Ijumaa, baada ya msako wa mwezi mzima, mbwa mabingwa wa kuwaokoa walipata watoto hao.

Maneno ya kwanza kutoka kwa binti mkubwa Lesly, ambaye alikuwa amemshika mtoto mikononi mwake, yalikuwa "Nina njaa", mmoja wa waokoaji aliambia RTVC ya Colombia. Mmoja wa wavulana, ambaye alikuwa amelala, aliinuka na kusema: "Mama yangu amekufa".

Baadaye iliibuka kuwa mama wa watoto hao alinusurika msituni kwa siku nne baada ya ajali hiyo ya ndege. "Kabla hajafa, mama yao aliwaambia kitu kama, 'Nyie ondokeni hapa'," baba wa watoto hao, Manuel Ranoque alisema.

Video iliyosambazwa na wizara ya ulinzi ya Colombia ilionyesha watoto hao wakiinuliwa hadi kwenye helikopta kwenye giza juu ya miti mirefu. Wamesafirishwa hadi mji mkuu wa taifa hilo Bogota, ambako magari ya kubebea wagonjwa yamewapeleka hospitalini kwa matibabu zaidi.

Familia ya watoto hao imelishukuru jeshi hilo kwa kuendelea na msako licha ya kuwa na uwezekano mdogo wa kuishi, hivyo wakaiomba serikali kuwarudisha nyumbani watoto hao haraka iwezekanavyo.

"Sikupoteza matumaini, siku zote nilikuwa nikiunga mkono msako huo. Najisikia furaha sana, namshukuru Rais Petro na 'wananchi' wangu ambao walipitia matatizo mengi," bibi yao aliviambia vyombo vya habari vya serikali.

Rais Petro pia alipongeza juhudi za jeshi na watu wa kujitolea, na kusifu "mkutano wa ujuzi: Asili na kijeshi", akiongeza kwamba "hii ndiyo njia ya kweli ya amani".

Lakini alihifadhi sifa maalum kwa watoto na uhusiano wao na mazingira.

"Hao ni watoto wa msituni, na sasa wao pia ni watoto wa Colombia," alisema.

Ingawa wengi katika jimbo katoliki la Colombia wametaja uokoaji wa watoto hao kama "muujiza", Bw Rufino, mtaalamu wa kiasili, alisema kisa cha kweli kinatokana na "uhusiano wao wa kiroho na asili".

"Msitu sio tu wa kijani kibichi, lakini kuna nguvu za zamani ambazo watu wanahusiana nazo, kujifunza na kusaidiana," alisema.

"Ni vigumu kuelewa hili, najua, lakini hii ni fursa nzuri kwa jamii, wanadamu, kujifunza kuhusu mitazamo tofauti ya ulimwengu iliyopo katika maeneo.

“Mama huyohuyo ambaye alikuja kuwa mzimu baada ya ajali hiyo akawalinda,” alisema. "Na sasa tu ataanza kupumzika."