Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Dunia ya Magari: Mercedes-Benz yazindua gari lenye nguvu zaidi na kasi katika historia yake
AMG, kitengo cha magari ya michezo ya Mercedes-Benz, kimezindua gari aina ya GT XX, ambayo inatarajiwa kuanza kuuzwa mwaka ujao. Gari ya umeme ya milango minne ambayo ina (Horsepower) kasi ya injini ya zaidi 1,360, kulingana na mtengenezaji, ni gari lenye kasi na nguvu zaidi la AMG kuwahi kutengenezwa.
Gari hii itachukua nafasi ya Coupe ya milango 4 inayotumia petroli. Toleo la sasa la GT 4 Coupe ina nguvu ya injini ya 843.
GT XX ina mota mbili za umeme nyuma na moja mbele. Mota ya mbele haitakuwa inatumika muda wote ili kupunguza matumizi ya nishati na itakuwa inawashwa tu katika hali maalumu, kama vile kuongeza kasi au kuendesha gari kwenye barabara zenye utelezi, ili kuhamisha nguvu zaidi kwa magurudumu ya mbele.
Mercedes-Benz inasema GT XX ina kasi ya juu ya kilomita 360 kwa sasa (360 km / h). Inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuongeza kasi hiyo kutoka 0 hadi 100 km / h chini ya sekunde mbili na nusu.
Mercedes-Benz inasema betri za gari hilo zimetengenezwa kwa teknolojia mpya inayoweza kuhifadhi nishati ya kutosha na kwenda kilomita 400 baada ya dakika tano za kuchaji.
Taa za nyuma ni seti ya taa sita za duara zinazofanana na injini yake inafanana na injini za ndege za kivita.
Gari hilo ambalo litazinduliwa mwaka ujao, litashindana na magari kama ya Porsche Taycan na gari la michezo la Lucid Air. AMG pia inapanga kuzindua SUV ya 2027.
Magari yanayotumia umeme ya AMG yatazinduliwa wakati ambapo baadhi ya magari kama vile Porsche, Lamborghini na Maserati, wamechelewesha kuzinduliwa kwa magari yao ya umeme kutokana na hali ya soko.
Tesla isiyo na dereva
Tesla limewasilisha gari jipya linalojiendesha lenyewe kwa mteja kwa mara ya kwanza. Katika video iliyotolewa na kampuni hiyo, Model Y inaonekana ikijiendesha kutoka kiwanda cha Tesla huko Austin, Texas, hadi nyumbani kwa mteja, mwendo wa nusu saa bila abiria yoyote.
Tesla haijatoa taarifa yoyote kuhusu programu au mfumo wa kujiendesha wa gari hilo. Katika mwongozo wa Model Y, uwezo wa Tesla wa kujiendesha unafafanuliwa kama "Fully Autonomous Driving. Lakini pia dereva anaweza kuchukua udhibiti wa gari hilo muda wowote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla Elon Musk alisema hakuna mtu aliyehusika katika kuendesha gari. Mwishoni mwa video, gari linasimama mbele ya jengo la ghorofa, ambapo mteja na wafanyakazi kadhaa wa Tesla wanalisubiri.
Elon Musk amekuwa akiahidi kwa miaka mingi kwamba magari yote ya Tesla siku moja yatajiendesha yenyewe. Mwaka 2019, alitangaza kwamba Tesla itakuwa na teksi milioni moja za kujiendesha kufikia 2020. Ahadi hiyo haijatimizwa, na Tesla inaonekana kuwa nyuma ya washindani wake katika kuendeleza magari ya kujiendesha.
Mini ya Dola laki moja
Kampuni ya Uingereza ya Wood & Pickett, kwa kushirikiana na mbunifu maarufu wa magari wa Uingereza Ian Callum, imerejesha gari la Mini.
Wood & Pickett ni kampuni kongwe ya magari Uingereza ambayo sasa inatazamia kulirejea gari hilo. Kampuni ilianza katika miaka ya 1960 kwa kuzalisha Mini na haraka ikapendwa na wateja wasanii na matajiri. Rolls-Royce, Jaguar na Range Rover ziliongezwa baadaye kwenye orodha ya magari ya Wood & Pickett.
Ian Callum, ambaye hapo awali alisimamia muundo wa Jaguar na Land Rover, anasema injini ya gari imeimarishwa hadi uwezo wa nguvu 110, na Wood & Pickett wanasema ni kasi na kufurahisha zaidi kuendesha kuliko mtindo wa awali.
Mini Classic ya kwanza iliundwa kwa ajili ya mwanamitindo na mtu mashuhuri wa Uingereza David Gandy. Gari hii pia ikawa inapatikana kwa wanunuzi wengine. Kwa sasa inagharimu bei ya kuanzia ya £75,000 (kama $103,000).
Kwaheri Luca
Luca Di Meo, Mkurugenzi Mtendaji wa Renault Group, alitangaza kuwa anajiuzulu. Ni mtengenezaji wa magari wa Ufaransa tangu 2020 katika kampuni hiyo, na anatazamiwa kuwa mkuu wa Kundi la Kering, linalomiliki Gucci na Saint Laurent.
Luca Di Meo alianza kazi yake Renault katika miaka ya 1990, kabla ya kuhamia Toyota na Fiat. Kabla ya kujiunga tena na Renault, alikuwa mkuu wa Volkswagen Group. Luca Di Meo alijiunga na Renault wakati kampuni hiyo ikiwa katika mzozo mkubwa, kwa sababu ya janga la Covid.
Bw. Di Meo alibadilisha muundo wa Renault na kuzalisha magari ya umeme na yale ya mafuta, alizindua bidhaa ambazo ziliisaidia Renault kufikia mauzo ya juu zaidi katika historia 2025, kutoka hasara ya euro bilioni 7.3 mwaka 2020.
Gari la kwanza kuzinduliwa chini ya uongozi wa Di Meo lilikuwa ni Megane ya umeme, ambalo lilikuwa gari la anasa zaidi kwa bidhaa za Renault. Ili kushindana na watengenezaji magari wa China, Di Meo alizindua Twingo, Renault 5, na Renault 4, ambazo ni kwa ajili ya Ulaya na zinauzwa kwa bei inayoweza kushindana na bidhaa za China.
Di Meo pia amefanya kazi na kampuni ya kutengeneza magari ya Kichina ya Geely. Pia alishirikiana na Google kuongeza mifumo ya Android kwenye magari ya Renault.
Bei ya hisa ya Renault imepanda kwa asilimia 80 katika miaka mitano chini ya Di Meo. Bodi ya Renault imesema inatafuta mrithi wa Di Meo, na ripoti za vyombo vya habari zimependekeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya atachaguliwa kutoka ndani ya kampuni hiyo.
DiMeo ndiye mtendaji mkuu wa hivi punde wa magari kujiuzulu, kufuatia kuondoka kwa Carlos Tavares, Mkurugenzi Mtendaji wa Stellantis, Makoto Uchida, Mkurugenzi Mtendaji wa Nissan, na Jim Rowan, Mkurugenzi Mtendaji wa Volvo.