Mtoto wa miaka mitano apatikana akiendesha gari la mzazi wake Utah

Japo malezi hutofautiana lakini ni kawaida kwa wazazi kuumizwa vichwa kwa tundu wa watoto wao. Aina na kiasi cha utundu ama wakati mwengine ukorofi wa watoto pia hutofautiana.

Nchini Marekani, mtoto wa miaka mitano ajulikanaye kama Adrian alichukua gari la nyumbani kawao na kuingia nalo barabarani akiliendesha kabla ya kukamatwa na askari wa barabarabi jimboni Utah.

Askari aliyekuwa doriani aliliona gari moja likiyumba kutoka upande mmoja wa barabara mpaka mwengine likiwa kwenye kasi ya kilomita 50 kwa saaa.

Askari huyo alitoa amri ya gari hilo kusimama, amri ambayo ilitekelezwa vilivyo na dereva wa gari hilo.

Alipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa aliyekuwa akiendesha ni ntoto mdogo, ambaye alimwambia kuwa alikuwa njiani kwenda kununua gari la kifahari la Lamborghini.

Mtoto huyo wa kiume aliwaambia polisi kuwa aliondoka nyumbani baada ya mama yake kukataa kumnunulia gari hilo la kifahari.

Lamborghini ya bei ya chini kabisa ni $180,000 (dola laki moja na themanini elfu) - na baada ya mama yake kusema hawezi kununua, ukatokea ubishani baina yao.

"Baada ya kushindwa kuelewana na mama yake akaamua kuendesha gari kwenda California kujinunulia mwenyewe,"Polisi walieleza kupitia mtandao wao wa Twitter. "Hata hivyo alikuwa na upungufu wa pesa ya kununulia, alikuwa na dola tattu mfukoni mwake."

Mkanda wa video uliochukuliwa kutoka kwenye gari ya polisi na kuoneshwa na runinga ya KSL-TV unaonesha gari hilo likiegeshwa pembeni kutii amri ya polisi.

Awali polisi walidhani dereva wa gari hilo ni mlemavu.

Katika mkanda huo, afisa wa polisi anasikika akiuliza baada ya kumuona mtoto huyo: "Una miaka mingapi? Unamiaka mitano?"

Mvulana huyo alikuwa amekaa ukingoni mwa kiti ili aweze kukanyaga mafuta na breki.

Mpaka anakamatwa alikuwa kashaendesha gari barabarani kwa muda wa dakika tano kutoka nyumbani kwao.

Pia unaweza kusoma:

Hakuna aliyeumia katika tukio hilo. Suala hilo limefikishwa kwa waendesha mashtaka kuamua kama wazazi watashtakiwa ama la, kwa mujibu wa KSL-TV.

Wazazi wote wawili walikuwa kazini wakati tukio hilo likitokea na mtoto huyo alikuwa chini ya uangalizi wa ndugu yake alipochukua gari.

Polisi jimboni humo wamewakubusha wazazi kuhakikisha kuwa funguo za magari haziwekwi katika maeneo ambayo watoto watazipata.