Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran-Pakistan: Mambo matatu kuuwelewa mvutano wa nchi hizo mbili
- Author, Jose Carlos Cueto
- Nafasi, BBC
Mvutano mpya ulizuka wiki iliopita barani Asia, kati ya Iran na Pakistan, nchi mbili jirani zenye nguvu kubwa za kijeshi, zilishambuliana katika mipaka yao, na kuzua wasiwasi wa kimataifa kuhusu mzozo mpya katika eneo hilo.
Mvutano huo umezuka baada ya Iran kufanya operesheni za kijeshi katika nchi tatu tofauti: Syria, Iraq na Pakistan.
Kwa nini mvutano kati yao umeongezeka?
Mapambano kati ya Iran na Pakistani yalianza Jumanne iliyopita, wakati Iran iliposhambulia maeneo yenye makundi yenye silaha katika jimbo la Balochistan, magharibi mwa Pakistan.
Watoto wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulio hilo, kulingana na maafisa wa Pakistan.
Iran ilisisitiza lengo lake si raia wa Pakistan, bali ni Jaish al Adl pekee – wanamgambo wa Sunni wa Baloch ambao wamefanya mashambulizi nchini Iran na dhidi ya vikosi vya serikali ya Pakistan hapo awali.
Jaish al Adl limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama vya Iran katika mkoa wa Sistan-Baluchistan, na Iran inadai kuwa kundi hilo linaungwa mkono na Marekani na Israel.
Lakini serikali ya Pakistan ilichukulia operesheni ya anga ya Iran kuwa "kitendo haramu na uvamizi usio na msingi wa anga yake." Ilionya inaweza kusababisha "matokeo makubwa."
Aidha, ilimuondoa balozi wake nchini Iran na wakati huo ikampigia kura ya turufu balozi wa Iran kurejea nchini mwake.
Alhamisi hii, Pakistan ilijibu kwa kurusha makombora katika "maficho ya magaidi" ndani ya ardhi ya Iran, katika mkoa wa Sistan na Balochistan - takribani watu tisa waliuwawa kwa mujibu na ripoti za vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
Jeshi la Pakistan limesema kwa kuzingatia taarifa za kijasusi, limeshambulia vituo vya Jeshi la Ukombozi la Balochistan na Balochistan Liberation Front nchini Iran, makundi yanayotuhumiwa kufanya shughuli za kigaidi ndani ya Pakistan.
Walieleza kuwa ndege zisizo na rubani, roketi na silaha nyingine zilitumika katika operesheni hii, na tahadhari kubwa zilichukuliwa ili kuepuka kushambulia raia.
Kama ilivyosema Iran, Pakistan nayo ilieleza madhumuni ya mashambulizi yake ni kwa ajli ya usalama wake na maslahi ya taifa" na "inaheshimu mamlaka na ardhi ya jirani yake.
Uhusiano kati ya Iran na Pakistan ukoje?
Shambulio la Iran lilitokea siku ileile ambayo waziri mkuu wa Pakistan na waziri wa mambo ya nje wa Iran walikutana mjini Davos, huku majeshi ya Iran na Pakistan yakifanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja huko Ghuba.
Iran na Pakistan zina mpaka wa kilomita 900 na kuna wasiwasi wa muda mrefu kutoka serikali zote mbili juu ya masuala ya usalama katika mpaka wao.
Katika mahojiano na BBC, Robert Macaire, balozi wa zamani wa Uingereza nchini Iran, alielezea eneo la Balochistan, liko kati ya nchi hizo mbili na ni eneo lisilo na sheria na makundi ya usafirishaji wa madawa ya kulevya yanahusika na mauaji ya maelefu ya watu.
Iran na Pakistan zimekuwa zikishutumiana katika siku za nyuma kuyahifadhi makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali ambayo yanafanya mashambulizi katika maeneo yao ya mpakani.
Mwaka 2017, Pakistan ilisema ndege isiyo na rubani ya Iran ilidunguliwa kwa sababu ilikuwa ndani ya ardhi ya Pakistan. 2014 vikosi vya usalama vya Iran vilivuka mpaka kuwafuata watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye itikadi kali.
"Kufuatia operesheni hizo, pande zote mbili zilisisitiza kuwa haya sio mashambulizi dhidi ya taifa jirani," anasema mwandishi wa diplomasia wa BBC, Paul Adams.
Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Pakistan kama taifa huru mwaka 1947 na Tehran iliiunga mkono Pakistan katika vita vyake dhidi ya India mwaka 1965.
"Kuna uhusiano wa kitamaduni na kihistoria kati ya pande zote mbili, na uhusiano mkubwa wa kibiashara," Michael Kugelman, mkurugenzi wa Kituo cha Wilson, ameambia BBC.
"Na pia kumekuwa na mipango (ambayo haijatimizwa) kujenga bomba la pamoja la gesi. Na Iran inaunga mkono msimamo wa Pakistan kuhusu mzozo wa Kashmir na India," Kugelman anasema.
Lakini kufuatia mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Pakistan ilisogea karibu na Saudi Arabia, mpinzani wa Iran.
Na hili limeleta kizuizi panapohusika upanuzi wa ushirikiano kati ya Iran na Pakistan," anaeleza Kugelman.
"Katika miaka michache iliyopita, Iran pia imeshutumiwa na Pakistani kwa kuajiri vijana ili kueneza madhehebu yake," iliripoti idhaa ya BBC ya Urdu.
Iran inataka kuonyesha nini?
Wachambuzi wanasema jibu la Pakistan kwa hatua za Iran si jambo la kushangaza. "Jibu la Pakistan linaongeza hatari ya mvutano kukuwa lakini pia linatoa fursa ya mapatano," anasema Kugelman.
Wachambuzi wengine wanasema mashambulizi ya Iran huko Syria, Iraq na Pakistan yalichochewa na hali ya mambo ya Mashariki ya Kati.
Jiyar Gol, mwandishi wa habari wa Idhaa ya BBC ya Kiajemi, anasema huu ni wakati ambapo Iran ina nia ya kuonyesha nguvu zake: "Iran inatuma ujumbe kuwa vitendo vya kuishambuliwa vitajibiwa."
Kadhalika, akieleza juu ya mashambulizi ya Iran huko Iraq na Syria, Gol anasema Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran linataka kudhihirisha uwezo wa makombora yake kwamba yanaweza kuzifikia kambia za Marekani, Israel na majeshi mengine ya kigeni katika eneo hilo.
Shashank Joshi, mhariri wa jarida la The Economist la Uingerezam aliiambia BBC ingawa "hii si mara ya kwanza kuwa na mvutano wa mpakani (Iran na Pakistan) lakini huu ndio mvutano mkubwa zaidi katika kumbukumbu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah