Je, Iran inaonyesha uwezo wake wa makombora kwa mashambulizi ya kikanda?

Mashambulizi ya Iran katika maeneo ya Iraq, Syria na Pakistan, kutoka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yanaonyesha nguvu za jeshi la Iran katika eneo hilo.

IRGC inasema kambi za Marekani katika Mashariki ya Kati, pamoja na kambi za Israel huko Tel Aviv na Haifa, zinaweza kufikiwa na makombora yake ya balistiki.

Katika muda wa saa 24 tu, ilionyesho wazi uwezo wake kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani katika nchi tatu tofauti.

Kushambulia Pakistan

Siku ya Jumanne jioni IRGC ilishambulia maeneo mawili ndani ya nchi jirani ya Pakistan, vyombo vya habari vilivyo karibu na kikosi hicho viliripoti mashambulizi hayo yaliharibu ngome mbili za kundi la wanamgambo wa Jaish al-Adl na kulipiza kisasi mauaji ya walinzi wa mpakani wa Iran wiki zilizopita.

Jaish al-Adl, kundi la Sunni ambalo linasema linapigania haki za watu wa jamii ya Baloch kusini-mashariki mwa Iran, lilisema nyumba mbili za familia ya wanachama wake ziliathirika.

Pakistan ilisema shambulio hilo "halikubaliki kabisa," ikisema kuwa lilisababisha vifo vya watoto wawili, na kuonya "itajibu vikali."

Kushambulia Iraq

Kulikuwa na lawama kama hizo kutoka Iraq, jirani wa magharibi wa Iran, baada ya IRGC kurusha makombora 11 ya balestiki huko Irbil, mji mkuu wa Mkoa wa Kurdistan wenye mamlaka ya ndani.

Takriban raia wanne waliuawa, kulingana na serikali ya eneo hilo. Waziri Mkuu, Masrour Barzani aliliita shambulio hilo "uhalifu dhidi ya watu wa Kikurdi."

Shirika la habari la Fars, ambalo liko karibu na IRGC, lilidai "makao makuu" ya shirika la kijasusi la Israel la Mossad yaliharibiwa katika mashambulizi hayo.

Baraza la Usalama la Mkoa wa Kurdistan lilikataa kabisa "kisingizio kisicho," huku Israel ikikaa kimya.

Makombora manne ya IRGC yaliharibu nyumba ya mfanyabiashara mashuhuri wa Kikurdi, Peshraw Dizayee. Aliuawa katika shambulio hilo pamoja na bintiye wa miezi 11.

Mshauri wa Barzani alisema ni "upuuzi kabisa kupendekeza [Dizayee] alihusika katika ujasusi wa aina yoyote, kwamba alifanya kazi na Israel," lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian alisisitiza Jumatano kwamba IRGC haikufanya makosa.

Dizayee mwasisi na mmiliki wa kampuni mbili - Falcon Group na Empire World; ni kutoka familia yenye nguvu ya Barzani, ambayo inaongozwa na babake, waziri mkuu na kiongozi wa Kurdistan Democratic Party, Massoud Barzani.

Kampuni ya Falcon inafanya kazi katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usalama, ujenzi, mafuta na gesi. Kitengo chake cha usalama kimetoa msaada kwa makampuni ya Magharibi nchini Iraq.

Shambulio la Irbil ni ujumbe kwamba sio tu IRGC inaweza kufanya mashambulizi sahihi, pia ina uwezo wa kupiga mitambo ya kijeshi karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Irbil, ambako Marekani na vikosi vingine vya kigeni viko.

Madai ya IRGC ya kulenga vituo vya Israel huko Irbil pia yana madhumuni ya kisiasa, kufuatia shambulio linaloshukiwa kuwa la Israel huko Syria 25 Disemba na kumuua kamanda mkuu.

Kushambulia Syria

Jumatatu usiku IRGC ilirusha makombora ya balestiki katika kile ilichosema ni ngome za kundi la Islamic State (IS) na "makundi ya kigaidi" katika mkoa wa kaskazini-magharibi wa Idlib nchini Syria.

Idlib ni ngome ya mwisho iliyosalia ya upinzani wa Syria baada ya miaka 12 ya vita dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad, ambaye ameweza kusalia madarakani kwa uungwaji mkono wa jeshi la Urusi na Iran.

Kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sharm (HTS) linatawala Idlib, ingawa IS na al-Qaeda pia wapo huko.

IRGC ilisema mashambulizi ya Idlib yalifanyika ili kulipiza kisasi mashambulizi mawili ya bomu ya kujitoa muhanga ya IS huko Kerman, kusini mwa Iran, Januari 3, ambayo watu 94 waliuawa.

Washambuliaji hao walilenga umati uliokusanyika karibu na kaburi la Kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi, Qasem Soleimani kuadhimisha mwaka wa nne wa kuuawa kwake katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani.

IRGC ilisema ilitumia kombora la Kheibar Shekan (Castle Buster), ambalo linaweza kusafiri hadi kilomita 1,450 (maili 900), kulenga Idlib.

Pia, imesema kombora hilo lilirushwa kutoka mkoa wa kusini wa Khuzestan, ingawa ingeweza kulirusha kutoka mkoa wa magharibi wa Azerbaijan, ambao uko karibu zaidi na Syria.

Uchaguzi kuhusu eneo la kurushia makombora unaonyesha Iran inataka kuufahamisha ulimwengu uwezo wake wa kufika maeneo mbalimbali nchini Israel, ambayo inapakana na Syria.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah