Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa Iran aapa kujibu vikali mashambulizi ya mabomu yaliyoua watu 84
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa "jibu kali" kwa shambulio la bomu dhidi ya umati wa watu waliokuwa wakiadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya jeneralu Qasem Soleimani yaliyofanywa na Marekani.
Shambulio la Kerman kusini mwa Iran lilisababisha vifo vya watu 84 na wengine wengi kuwajeruhi.
Idadi ya waliofariki ilirekebishwa Alhamisi asubuhi na mkuu wa huduma za dharura za Iran kutoka idadi ya awali ya 95.
Bado hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
"Wahalifu wakatili lazima wajue kwamba watakabiliwa vikali kuanzia sasa na bila shaka kutakuwa na jibu kali," Khamenei alisema katika taarifa yake Jumatano jioni.
Naibu wa kisiasa wa Rais Ebrahim Raisi, Mohammad Jamshidi, aliilaumu Israel na Marekani. Hata hivyo Marekani ilisema haina taarifa zozote kwamba Israel ilihusika na kupuuzilia mbali madai kwamba Washington ilihusika.
Huenda tuhuma zikawakumba Waarabu wanaotaka kujitenga na makundi ya wanajihadi wa Kisunni kama Islamic State (IS), ambao wamefanya mashambulizi dhidi ya raia na vikosi vya usalama nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Wakati huo, IS ilikapongeza hatua ya kuuawa kwa jenerali wa Iran Qasem Soleimani, ambaye wanamgambo wake walipigana na kundi hilo nchini Iraq kwa miaka mingi.
Soleimani alionekana kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Iran baada ya kiongozi mkuu kabla ya kuuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani katika nchi jirani ya Iraq mnamo 2020.
Shambulio la Jumatano linakuja huku kukiwa na mvutano mkubwa katika eneo hilo baada ya naibu kiongozi wa kundi la Kipalestina la Hamas linaloungwa mkono na Iran, kuuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani za Israel nchini Lebanon.
Picha zilizorushwa na Televisheni ya Taifa ya Iran zilionyesha umati mkubwa wa watu waliokuwa wakishiriki maandamano kando ya barabara iliyo na mabango yaliyokuwa na jina la Qasem Soleimani wakati milipuko hiyo ilipotokea.
Watu walisikika wakipiga kelele na kisha kuonekana wakikimbia kwa hofu baada ya milipuko hiyo.
Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa bomu la kwanza lililipuliwa mwendo wa saa 15:00 kwa saa za Iran (11:30 GMT), karibu mita 700 kutoka kwenye msikiti wa Saheb al-Zaman, nje kidogo ya mashariki mwa Kerman.
Mlipuko wa pili ulitokea kama dakika 15 baadaye, karibu kilomita 1 kutoka kwenye kaburi, likilenga watu ambao walikuwa wamekimbia mlipuko wa kwanza, walisema.
Gavana wa jimbo la Kerman aliliambia shirika la habari la serikali Irna kwamba milipuko yote miwili ilitokea nje ya vituo vya ukaguzi vya usalama na kwamba mamlaka walikuwa na uhakika kuwa ilisababishwa na mabomu. Lakini alisema bado haijabainika iwapo zililipuliwa kwa mbali au na washambuliaji wa kujitoa mhanga.
Shirika la habari lenye misimamo mikali ya Tasnim, ambalo lina uhusiano na Jeshi la Mapinduzi ya Iran, awali lilinukuu vyanzo vikisema kwamba "mifuko miwili iliyobeba bomu" huenda ililipuliwa "kutoka mbali".
"Tulikuwa tukielekea makaburini wakati gari liliposimama ghafla nyuma yetu na pipa la taka lililokuwa na bomu lililipuka," mashuhuda alinukuliwa na shirika la habari la Isna akisema.
Tulisikia tu sauti ya mlipuko na kuona watu wakianguka."
Shirika la Red Crescent la Iran limesema waliofariki ni pamoja na angalau mhudumu mmoja wa afya ambaye alitumwa kwenye eneo la mlipuko wa kwanza na kabla mlipuko wa pili kutokea.
Rais Ebrahim Raisi aliyataja mashambulio hayo ya mabomu kuwa ni "kitendo cha woga" kilichofanywa na "wahalifu wanaoichukia Iran na wafuasi wa ugaidi na giza".
Aliyekuwa balozi wa Uingereza nchini Iran, Rob Macaire, aliambia BBC kwamba haijabainika ni nani aliyehusika na mashambulizi hayo ya mabomu.
"Ni wazi kuna vikundi vya upinzani ambavyo vina uwezo, ingawa wamebanwa kabisa, kufanya mashambulizi ya kikatili," alisema. "Sidhani kama ni mashambulizi yanayotishia serikali, lakini hakika yatakuwa na athari."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio hilo na kutoa "rambirambi zake kwa familia zilizofiwa na wapendwa wao na serikali" ya Iran, msemaji wake alisema.
EU ilisema inalaani shambulio hilo "vikali sana" na kuelezea "mshikamano wake na watu wa Iran", wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin amelitaja shambulio hilo "kuwa la kushtua na la kikatili".
Nchi kadhaa za Ghuba na Uturuki, zimelaani mashambulizi hayo huku Rais wa China Xi Jinping akituma rambirambi zake kwa rais wa Iran.
Kiongozi wa vuguvugu la Hezbollah la Lebanon - kikundi chenye silaha ambacho kama Hamas kinaungwa mkono na Iran - alisema waathiriwa walikuwa "watetea imani ambao walikufa katika njia moja, sababu na vita ambavyo viliongozwa na" Soleimani.
Alikuwa mkuu wa operesheni za siri za Kikosi cha Quds na utoaji wake wa miongozo, ufadhili, silaha, ujasusi, na usaidizi wa vifaa kwa serikali washirika na makundi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na Hizbullah na Hamas.
Rais wa Marekani wa wakati huo waDonald Trump, ambaye aliamuru shambulio la ndege zisizo na rubani mwaka wa 2020, alimtaja Soleimani kama "gaidi nambari moja duniani" na alidai kuwa wanajeshi waliokuwa chini yake wamewaua mamia ya raia na wanajeshi wa Marekani katika miongo miwili iliyopita.
Serikali ya Iran ilishutumu Marekani kwa kitendo cha ugaidi cha kimataifa na kutoa wito wa kukamatwa kwa Bw Trump na maafisa wengine.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi