Wamesubiri katika uwanja wa ndege lakini hawajui pa kwenda

- Author, Catherine Byaruhanga
- Nafasi, Mwandishi wa habari wa Afrika, BBC News,
- Akiripoti kutoka, Paloich
Ni uwanja wa ndege ambao kusubiri hapa ni kama jahanamu.
Uwanja wa ndege wa Paloich, ambao kwa kawaida hutumiwa na wafanyakazi wanaohudumia maeneo ya mafuta ya Sudan Kusini, umegeuka kuwa kambi ya maelfu ya watu wanaokimbia mzozo katika nchi jirani ya Sudan - sasa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Hakuna vyoo, hakuna maji ya mfereji, hakuna jikoni - ni umati wa watu tu wanaoishi karibu na mifuko yao, wamepumzika kwenye toroli za mizigo, au kulala chini ya hema za muda wakingojea kupanda ndege.
Wameishia hapa, saa nne kutoka mpaka na Sudan, kwa matumaini ya kutafuta njia ya kutoka.
Lakini kuna safari chache za ndege na habari ndogo kuhusu wakati ambapo watu wanaweza kuondoka.
Miongoni mwa wakimbizi hao ni raia wa Eritrea ambao wamefurushwa kwa mara ya pili baada ya hapo awali kuwasili Sudan kukwepa hali ngumu ya nyumbani. Na watu hawa wamekwama tena katika hali hii .
Kulingana na Umoja wa Mataifa, kulikuwa na zaidi ya wakimbizi 136,000 wa Eritrea na wanaotafuta hifadhi nchini Sudan kabla ya vita hivi.
Raia wengi wa Eritrea hawataki kutaja majina yao kwa waandishi wa habari kwa sababu wanaogopa kuadhibiwa na mamlaka ya Eritrea.
Eritrea ni nchi yenye vikwazo vya hali ya juu ambayo inadhibiti karibu ncha zote za maisha ya watu, na wengi wanataka kuepuka huduma ya kitaifa ya lazima.
Lakini Tesfit Girmay alikubali kuzungumza nami. Alikuwa amewasili Paloich siku tano mapema.
"Aina ya maisha ya huku, usingetamani hata yawe ya wanyama' alisema akitazama maskani karibu naye.
Akiwa mseja alijitambua kuwa alikuwa na bahati kuliko wengine.
"Labda naweza kustahimili. Kulala nje, kula mara moja kwa siku, labda naweza kuvumilia. Lakini shida kubwa, kuna watu wenye watoto. Kuna watu wenye watoto wanne au watano," Bwana Tesfit aliniambia.
Alikimbia uchumi uliozorota nchini Eritrea mwishoni mwa mwaka jana na kuelekea Sudan, akiwa na matumaini ya kupata kazi na pengine kusafiri hadi nchi nyingine.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini huko Sudan Kusini, Waeritrea wanajikuta wamenaswa.
Zaidi ya 700 wamewasili nchini humo.
Raia wengine waliokimbia mzozo nchini Sudan kama Wakenya, Waganda na Wasomali wamerejeshwa makwao na serikali zao. Lakini Waeritrea wengi huko Paloich walisema walikuwa na hofu ya kurudi nyumbani, au hawaoni mustakabali huko.
Bw Tesfit alisema kuwa raia wa Eritrea katika uwanja huo wa ndege walipigwa marufuku kupanda ndege kuelekea mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Wakati huo huo wamekataa kwenda kwenye kambi zilizotengwa za wakimbizi nchini humo.
Umbali wa saa tatu kwa gari kuelekea kaskazini, na karibu na mpaka na Sudan, ni kambi nyingine ya muda iliyofurika.
Viwanja vya zamani vya Chuo Kikuu cha Upper Nile huko Renk, ambacho kilitelekezwa, sasa kinakaliwa na zaidi ya watu 6,000. Hata vichaka vilivyo upande mwingine wa barabara vinakatwa ili kutoa nafasi kwa wengi wa wanaowasili.
Hapa ndipo nilipokutana na mkimbizi mwingine kutoka Eritrea.
Aliketishwa kwenye ngazi za darasa na watoto wake watatu na kuniambia kuwa mumewe alikuwa ameenda mjini kutafuta chakula.
"Singeweza kuishi katika nchi yangu kwa sababu nisingeweza kumwabudu Mungu wangu jinsi nilivyopenda. Nisingeweza kuishi huko," alisema mwanamke huyo ambaye alitaka kubana jina lake.
Alieleza kwamba yeye alikuwa Mkristo wa kiinjilisti na alikuwa na matatizo nchini Eritrea, ambako dini inadhibitiwa sana na watu wa dini ambazo hazijaidhinishwa rasmi wamepelekwa gerezani.
Baada ya kutoroka Khartoum, alisema alikuwa na matumaini ya kwenda katika mji mkuu wa Sudan Kusini lakini hiyo ilikuwa ni changamoto.
"Hakuna mtu anayeweza kupita hadi Juba. Barabara imefungwa kwa Waeritrea pekee. Sijui nini kitakachofuata."
Kaimu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Sudan Kusini Deng Dau Deng aliambia BBC kwamba ofisi yake imewasiliana na balozi zote za kigeni zikiwemo za Eritrea, ili kuhakikisha raia wao wamerudishwa makwao.
Lakini alikiri kwamba hali ya Waeritrea ilikuwa ngumu kutokana na ukweli kwamba wapo ambao hawataki kurejea nyumbani na hawataki kuwasiliana na ubalozi wao.
Bw Deng hakanushi madai kwamba baadhi ya Waeritrea waliofika Juba walilazimika kurudi Paloich. Kwa vile ubalozi wa Eritrea haungewasafirisha kwa ndege kurudi Asmara na hakukuwa na kambi ya wakimbizi huko Juba kwa ajili yao, basi ilibidi waende kwingine, alisema.
Kwa upande wake, Rais wa muda mrefu wa Eritrea Isaias Afwerki aliambia televisheni ya taifa kuwa nchi yake itamkaribisha yeyote anayekimbia mzozo wa jirani yake.
"Eritrea ina mipaka iliyo wazi na bila shamrashamra itaendelea kupokea raia wa Eritrea na Sudan pamoja na wengine walioathiriwa na mzozo wa sasa na kushiriki nao chochote walicho nacho," rais alisema.

Serikali inaendesha safari za ndege za bure kwa ndege za mizigo kutoka Paloich na imesafirisha zaidi ya watu 7,000. Lakini ni sehemu ya wale wanaoingia.
Mkakati wake ni kutoa kila mtu kutoka Renk na Paloich hadi maeneo ambayo wanaweza kupata chakula, dawa na kujaribu kujenga upya maisha yao.
Lakini Sudan Kusini haina barabara zenye lami, safari chache za ndani na sehemu za nchi bado zinakabiliwa na machafuko tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018.
Ni changamoto kubwa kwa nchi yoyote ile na huku vita vya jirani yake vikiendelea idadi ya watu, raia na wageni, wanaoingia Sudan Kusini inazidi kuongezeka.
















