Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea

sdx
Maelezo ya picha, Naibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, ameiambia BBC hatari ya mzozo wa kikanda ni ya kweli wakati huu vita vya Israel-Hamas vikiendelea

Kamanda wa pili wa Hezbollah - wanamgambo wenye nguvu wanaoungwa mkono na Iran nchini Lebanon - amesema mauaji ya Israel ya raia huko Gaza yanahatarisha vita kuenea Mashariki ya Kati.

Sheikh Naim Qassem aliiambia BBC "matukio makubwa na ya hatari sana yanaweza kutokea katika eneo hilo, na hakuna mtu ambaye ataweza kuzuia athari zake."

Naibu kiongozi wa Hezbollah alikuwa akizungumza katika mahojiano mjini Beirut, wakati wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza ikisema zaidi ya watu 10,000 wameuawa hadi sasa.

Mashambulio ya Israel yamekuja baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba ambayo yaliua watu 1,400 - 1,000 kati yao raia.

Hatari ni ya Kweli

"Hatari ni ya kweli," alisema, "kwa sababu Israel inaongeza uchokozi dhidi ya raia na kuua wanawake na watoto. Je, inawezekana hali hii kuendelea bila ya kuleta hatari katika eneo hili? Nadhani hapana."

Hezbollah ni kundi la Waislam wa Shia - ambalo limeainishwa kama shirika la kigaidi na Uingereza, Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu. Ndilo kundi kubwa zaidi la kisiasa na kijeshi nchini Lebanon.

Majibu ya kundi hilo kwa vita vya Gaza yamehusisha kurusha makombora lakini kundi hilo liwekuwa na uangalifu juu ya vitendo vyake.

Shambulio la Israel lililomuua mwanamke na watoto watatu kusini mwa Lebanon siku ya Jumapili, Hezbollah ilirusha makombora ya Grad kwa mara ya kwanza katika mzozo huo, na kumuua raia wa Israel.

Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, ametishia kwamba kila kifo cha raia nchini Lebanon kitalipwa kwa kifo chengine Israel. Lakini hajatishia kuingia vitani moja kwa moja na Israel.

Kundi hilo linasisitiza "chaguzi zote zinazingatia." Zaidi ya wapiganaji wake 60 wameuawa, lakini ina wapiganaji wengi zaidi wa kuchukua nafasi zao.

Katika mahojiano yetu na naibu kiongozi wa kundi hilo - alijaribu kuonyesha Hezbollah kama kundi la kujihami - ingawa limeapa kuiharibu Israeli.

Mwaka 2006 iliingia katika vita na Israel baada ya kuwateka nyara wanajeshi wawili katika uvamizi wa kuvuka mpaka.

Atetea mashambulizi ya Hamas

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

BBC ilipodokeza kuwa ni Hamas ndio walioishambulia Israel tarehe 7 Oktoba, alitetea mashambulizi hayo kama jibu lisiloepukika kwa uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina.

Alirudia madai kwamba vikosi vya Israel ndivyo viliuwa raia, na sio Hamas. Lakini vipi kuhusu kamera – zilizovaliwa na wanamgambo wa Hamas wenyewe – zinazowaonyesha wakiwa kwenye mauaji?

Aliuliza swali. "Kwa nini tusiangalie kile ambacho Israel imefanya ndani ya Gaza," alisema. "Wanaua raia na kubomoa nyumba."

‘Vipi kuhusu Wagaza 10,000 ambao wameuawa? "Mauaji yaliyofanywa na Israel yanawahamasisha Wapalestina zaidi na zaidi kushikamana na ardhi yao," alijibu.

Alikubali kwamba Iran "inaunga mkono na kufadhili" Hezbollah lakini alidai haikutoa amri. Lakini wataalamu wanasema ni Tehran ndio itaamua ikiwa Hesbullah itainga katika vita na Israel au la.

Na kama wanajeshi wa Israel watalazimika kupigana na Hezbollah, watakuwa wanakabiliana na adui mwenye silaha nyingi kuliko Hamas. Kundi hilo la wapiganaji linaunga mkono Hamas. Linakadiriwa kuwa na takribani makombora 150,000.

Lina wapiganaji 60,000, ikiwa ni pamoja na vikosi maalumu, wapiganaji wa kawaida, wapiganaji wa dharura - kulingana na Nicholas Blanford, mshauri wa ulinzi na usalama wa Beirut, ambaye ameisoma Hezbollah kwa miongo kadhaa.

Mwaka 2006 kundi hilo lilipigana na Israel lakini Lebanon ilipoteza watu wengi zaidi. Zaidi ya watu 1,000 waliuawa, wengi wao wakiwa raia, na vitongoji vizima vilisambaratishwa katika ngome za Hezbollah. Israel ilipoteza wanajeshi 121 na raia 44.

Lebanon iko tayari kwa vita?

Raia wengi wa Lebanon hawana hamu ya vita. Wengi wana wasiwasi kwamba mashambulizi ya Hezbollah ya kuvuka mpaka yanaweza kuiingiza nchi hii kwenye vita isivyoweza kuvimudu.

Sheikh Qassem anasema. "Ni haki ya Mlebanon yeyote kuogopa vita. Hilo ni jambo la kawaida. Hakuna anayependa vita. Iambie Israel isimamishe uchokozi, ili vita visipanuke."

"Ikiwa vita na Hezbollah vitazuka,'' anasema Blanford, ''kile kinachoendelea Gaza kitakuwa kidogo. Waisraeli hawatotoka nje kwa muda wote wa mzozo. Wengi wa wakazi wake watalazimika kusalia katika mahandaki."

"Hakutakuwa na usafiri wa anga au usafiri wa baharini. Makombora makubwa zaidi ya Hezbollah yanaweza kulenga shabaha za kijeshi kote Israel."

Ameongeza, ''na jibu la Israel litakuwa baya kwa Lebanon. Kwa sasa, Hezbollah, Israel, na Iran zote zinajizuia, maadui wa zamani wanaotathmini uhalisia.''