Kiongozi wa Hamas akana kuwa kundi hilo lilitekeleza mauaji ya raia nchini Israel

Na Feras Kilani
BBC News, Arabic
Kiongozi mkuu wa Hamas amekataa kukiri kuwa kundi lake liliua raia nchini Israel, akidai kuwa ni makurutu waliosajiliwa kujiunga na jeshi ndiyo waliolengwa .
Moussa Abu Marzouk aliambia BBC kwamba "wanawake, watoto na raia hawakulengwa " katika mashambulizi ya Hamas.
Madai yake ni kinyume kabisa na ushahidi wa video ya wanaume wa Hamas wakiwapiga risasi watu wazima na watoto wasio na silaha.
Israel inasema zaidi ya watu 1,400 waliuawa na Hamas katika mashambulizi ya Oktoba 7, wengi wao wakiwa raia.
Bw Marzouk, naibu kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo, ambaye mali yake imezuiwa nchini Uingereza chini ya kanuni za kukabiliana na ugaidi , alihojiwa Jumamosi katika Ghuba. Yeye ndiye mwanachama mkuu zaidi kuzungumza na BBC tangu mauaji ya Oktoba 7.
BBC ilimshinikiza Bw Marzouk juu ya vita dhidi ya Gaza, haswa juu ya idadi kubwa ya mateka wanaoshikiliwa ndani ya eneo hilo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alijibu kwamba hawakuweza kuachiliwa wakati Israel ilikuwa ikishambulia kwa mabomu Gaza. Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema watu 10,000 wameuawa tangu Israel ianze operesheni mwezi uliopita.
"Tutawaachilia. Lakini tunahitaji kusitisha mapigano," alisema.
Bw Marzouk hivi majuzi alisafiri hadi Moscow kujadili kuhusu raia wanane wa wenye uraia wa nchi mbili -za Urusi na Israel waliotekwa tarehe 7 Oktoba na Hamas, shirika lililopigwa marufuku la kigaidi katika nchi nyingi zikiwemo Uingereza na Marekani.
Alisema wanachama wa Hamas huko Gaza "wametafuta na kupata mateka wawili wa kike" kutoka Urusi lakini hawakuweza kuwaachilia kwa sababu ya mzozo huo.
Wataweza tu kuwaachilia mateka, alisema, ikiwa "Waisraeli watasimamisha mapigano ili tuweze kuwakabidhi kwa Msalaba Mwekundu".
Alipobanwa na BBC kuhusu shambulio la Oktoba 7, Bw Marzouk alidai kuwa Mohamed el-Deif, kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas la Qassam Brigades, alikuwa amewaamuru wapiganaji wake kutowashambulia raia
"El-Deif aliwaambia wazi wapiganaji wake 'msiue mwanamke, msiue mtoto na msiue mzee'," alisema.
Askari wa akiba walikuwa, alisema, "walilengwa". Alisisitiza kwamba ni "majeshi [...] au askari" pekee waliuawa.
Lakini wanawake, watoto na raia "waliepushwa", alisema.
BBC ilihoji madai yake kiongozi huyo kuhusu video zilizonaswa kutoka kwa kamera za kofia ya wapiganaji wa Hamas, ambazo zinaonyesha raia wasio na silaha wakipigwa risasi kwenye magari na nyumba zao.
Bw Marzouk, ambaye alionekana kujidhibiti wakati wa mahojiano wakati mwingine iliteleza na hasira kuonekana katika uso wake , hakujibu swali moja kwa moja.
Alipoulizwa kama mrengo wa kisiasa wa Hamas ulijua kuhusu maandalizi ya shambulio hilo, naibu kiongozi huyo alisema kuwa mrengo huo wenye silaha "sio lazima kushauriana na uongozi wa kisiasa. Hakuna haja."
Mrengo wa kisiasa, wenye makao yake nchini Qatar, mara nyingi hujionyesha kuwa mbali na vikosi vya kijeshi huko Gaza.
Serikali ya Uingereza haioni tofauti - ilipiga marufuku mrengo wa kisiasa wa Hamas kama shirika la kigaidi mnamo 2021, ikisema kuwa "mbinu ya kutofautisha kati ya sehemu mbali mbali za Hamas ni ya juu tu. Hamas ni shirika gumu lakini moja la kigaidi " .
Bw Marzouk pia ameorodheshwa kama gaidi maalum wa kimataifa aliyetajwa na Idara ya Hazina ya Marekani, na anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya kuratibu na kufadhili shughuli za Hamas.
Mgogoro wa mateka
Mahojiano hayo siku ya Jumamosi yalikuja baada ya Israel kukataa ombi la Marekani la "kusitisha vita kwa ajili ya misaada ya kibinadamu" huko Gaza kuruhusu msaada na kuwaondoa baadhi ya mateka 240 waliotekwa na Hamas tarehe 7 Oktoba.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema siku ya Ijumaa mateka wote lazima waachiliwe kabla ya mapatano yoyote ya muda kuafikiwa.
Bw Marzouk alidai kuwa Hamas haikuwa na orodha ya wale wote aliowataja kuwa "wageni", wala hajui waliko wengi, kwa sababu walikuwa wakishikiliwa na "makundi tofauti".
Kuna makundi kadhaa ndani ya Gaza yakiwemo Palestina Islamic Jihad, ambayo yanafanya kazi kwa karibu na Hamas lakini yanajitegemea.
Alisema kusitishwa kwa mapigano kulihitajika ili kukusanya taarifa - kulikuwa na vipaumbele vingine wakati eneo hilo likikumbwa na mashambulizi ya mabomu.
Bw Marzouk atakuwa na jukumu muhimu katika jinsi mzozo na Israel unavyoendelea , na kuna uwezekano mkubwa akawa mkuu katika mazungumzo juu ya mateka.
Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel na Palestina
Mauaji ya Kibbutz:Jinsi Hamas walivyofanya shambulio lisilofikirika
Kiini cha mzozo:Fahamu chanzo cha uhasama kati ya Israel na Palestina












