Mzozo wa Israel na Palestina: Maoni ya Salah yaonesha mfano kwenye michezo

Chanzo cha picha, BBC Sport
- Author, Kevin Hand
- Nafasi, BBC Sport Africa
Majibu ya Mohamed Salah kuhusu mzozo wa Israel na Gaza yanapaswa kuweka mwelekeo wa michezo kusonga mbele, kulingana na wakala wa zamani wa PR na kitaaluma.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool na Misri alitoa wito kwa "viongozi wa dunia kukutana ili kuzuia mauaji zaidi ya roho zisizo na hatia" baada ya mlipuko mbaya katika hospitali ya Gaza City mwezi uliopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ni mmoja wa wanamichezo wengi walio na wafuasi wengi sana kwenye anuani zao za mtandao wa kijamii kutoa maoni yao kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas, ambayo imetajwa kuwa shirika la kigaidi na serikali za Uingereza na Marekani.
Mzozo wa sasa ulikuja baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia Israeli kutoka Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, na kuua zaidi ya watu 1,400, na Jeshi la Ulinzi la Israeli likifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi huko Gaza tangu wakati huo, na kusababisha vifo vya zaidi ya 10,000, kwa mujibu wa Wizara ya Afya katika eneo linalodhibitiwa na Hamas.
"Salah ni mfano wa mtu ambaye alikuwa chini ya shinikizo kubwa la kuonesha upande kwa sababu ya utaifa wake," Ian Bayley, ambaye sasa ni mhadhiri mkuu wa uandishi wa habari za michezo katika Chuo Kikuu cha Staffordshire, aliiambia BBC Sport Africa.
"Lakini alirudi nyuma na kusema: 'Ninachosimamia ni amani na mwisho wa mateso'."
Bayley anasema kwamba kauli ya Salah "haijawaridhisha baadhi ya watu" ambao wanahisi Mwanasoka Bora wa Afrika mara mbili anapaswa kutumia ushawishi wake mkubwa kuonesha "msimamo wa kisiasa zaidi".
"Hatimaye alipotoa ujumbe, alisifiwa na wengi kwa sauti yake ya kibinadamu na bado alikosolewa na wengine ambao walidhani msimamo wake unapaswa kuwa wa kuunga mkono zaidi Waarabu na Palestina," Bayley alielezea.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Lakini hawezi kufanya hivyo kwa sababu ya sera ya mitandao ya kijamii na klabu yake."
Wakati nyota wa tenisi wa Tunisia Ons Jabeur alipozungumza kuhusu suala hilo mapema mwezi huu, msimamo wake haukuwa na utata.
"Nimeamua kutoa sehemu ya pesa zangu za zawadi kuwasaidia Wapalestina," mchezaji huyo nambari saba duniani alisema kwenye fainali za WTA za kumaliza msimu nchini Mexico.
"Sio ujumbe wa kisiasa, ni ubinadamu. Nataka amani katika ulimwengu huu."
Bayley pia alikaribisha ujumbe wa Jabeur, akisema "ishara yoyote ambayo inachangia kupunguza mateso ya wanadamu inapaswa kupongezwa, mradi tu inafanywa kwa misingi ya ubinadamu na sio ya kisiasa".
"Suala gumu zaidi ni kwamba mzozo huo umegawanya maoni kiasi kwamba ishara yoyote, hata iwe yenye nia njema, bila shaka italeta sifa na ukosoaji," aliongeza.
Kwa hivyo majibu ya Salah, Jabeur na Waafrika wakuu yanatuambia nini kuhusu nafasi ya kisiasa wanamichezo wanayojikuta nayo ? Na ni hatari gani zinazohusika katika kutumia majukwaa yao kutoa maoni yao kuhusu masuala makubwa?
'Mabadiliko makubwa' katika mitandao ya kijamii
Tangu vita vilipoanza tarehe 7 Oktoba, kumekuwa na uungaji mkono mkubwa kwa ajili ya Palestina miongoni mwa vilabu vya michezo, wachezaji na wafuasi kote barani Afrika, hasa Afrika Kaskazini.
Kabla ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cape Verde tarehe 12 Oktoba, timu ya soka ya Algeria iliingia uwanjani ikiwa imevalia keffiyeh, vazi la kichwani linalohusishwa na upinzani wa Wapalestina, huku nahodha Riyad Mahrez akiwa miongoni mwa wachezaji waliopeperusha bendera ya Palestina baadaye uwanjani.
"Kwa kweli hakujawa na watu mashuhuri wa Algeria ambao hawajazungumza angalau kuonesha huruma kuhusu mateso yanayoendelea Palestina," mwandishi wa habari wa kandanda wa Algeria Maher Mezahi alisema.
"Unachopaswa kuelewa ni kwamba Algeria ilitawaliwa na Wafaransa kwa miaka 132 na Wazungu zaidi ya milioni moja walikuwa wamekaa Algeria kufikia 1962, hivyo Waalgeria wengi wanaona hali ya Palestina kuwa sawa na maisha yao ya zamani."
Mezahi aliita kauli ya Salah kuwa yenye "mvuto zaidi katika suala la mtu mashuhuri kushinikizwa kuzungumza" na Carole Kimutai, mtaalamu wa mikakati wa vyombo vya habari vya kidijitali nchini Kenya, akisema shinikizo hilo linatokana na ulimwengu wa kisasa.
"Masuala kama vile ubaguzi wa rangi, ujinsia, migogoro, dini, uavyaji mimba na kadhalika yanapoibuka, nyota wa michezo wanaweza kuchagua kuzungumza hadharani au kutojihusisha," aliiambia BBC Sport Africa.
"Lakini suala linapokuwa karibu na nyumbani, umma utatarajia mtu huyo kuzungumza. Gaza iko karibu na Salah. Hii inadhihirisha wazi maslahi mengi ambayo wachezaji kama Salah wanapaswa kuhangaika katika maisha yao ya michezo."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa hivyo kutokana na nyota huyo wa Liverpool, ambaye nyumbani kwake ni Nagrig nchini Misri uko umbali wa chini ya kilomita 350 kutoka Gaza, baada ya kuhimiza kujizuia ili kulinda maisha ya Wapalestina, je, ilishangaza klabu ya Ligi Kuu ya Crystal Palace ilipojitokeza kuunga mkono Israel?
Sio hivyo kwa maoni ya profesa mkuu wa michezo na uchumi wa kijiografia.
"Wamiliki wao wawili ni Wayahudi na wa tatu ni Mmarekani aliye na uhusiano mkubwa na jamii ya Wayahudi wa Marekani," alisema Simon Chadwick wa Shule ya Biashara ya Skema.
"Umiliki na tamaduni za vilabu ni muhimu sana, na kwa hivyo tunapata maoni tofauti." kuhusu masuala haya.
Nchini Israel, mshindi wa medali ya Olimpiki ya 2012 wa Brazil, Felipe Kitadai alieleza kuonesha "upendo na msaada wangu wote" licha ya kuripotiwa kuwa anataka kuondoka katika taifa ambalo limekuwa kituo chake hivi karibuni huku mchezaji wa kimataifa wa soka Manor Solomon akiwa miongoni mwa wale waliokosoa Hamas kwenye mitandao ya kijamii.
Akiwa na uzoefu wa vita baada ya kuwa huko Kyiv siku ambayo Urusi ilivamia Ukraine, Solomon wa Tottenham Hotspur alisimulia jinsi familia yake na marafiki walivyopitia "magumu" kwa sababu ya mzozo unaoendelea wa Israeli na Gaza.
"Mitandao ya kijamii ndio badiliko kubwa," alisema Bayley.
"Kama mzozo huu ungekuwa miaka 30 iliyopita, ni sawa kusema kwamba wanasoka hawangekuwa kwenye shinikizo walilonalo kama matokeo ya moja kwa moja ya kile kinachotoka kwenye mitandao ya kijamii."
"Ni hali isiyowezekana, ya hali ya juu na ngumu kwa mwanasoka yeyote katika hali kama tuliyo nayo sasa, ambayo haijawahi kutokea."
Hatari ya kuchapisha mtandaoni
Miaka mitatu iliyopita, Jabeur alipokea vitisho vya kuuawa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuchagua kuweka siasa kando kwa kuichezea Israel, nchi ambayo serikali yake haiitambui, katika mashindano ya kimataifa ya tenisi kwa niaba ya Tunisia.
Kuingia katika nyanja ya kisiasa, iwe ya kimataifa au vinginevyo, hivi karibuni imeonekana kuwa hatari kwa wengine pia.
Mwanasoka mashuhuri wa mpira wa kikapu Lebron James alikosolewa na wengi baada ya kuchapisha akiunga mkono Israel baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Baada ya kujitokeza kuiunga mkono Israel, bondia nguli Floyd Mayweather naye amepitia changamoto sawa na hiyo, halafu kuna wanasoka kadhaa wa sasa ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu na vilabu vyao.
Mlinzi wa Algeria Youcef Atal alisimamishwa kucheza na Nice, huku klabu hiyo ya Ufaransa ikiwa haijafurahishwa na chapisho, ambalo amelifuta na kuomba radhi, alipoonesha kuwa ni chuki dhidi ya Wayahudi. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 hatimaye alipigwa marufuku ya mechi saba na bodi inayosimamia Ligue 1, ligi kuu ya Ufaransa.
Noussair Mazraoui alikosolewa baada ya kuchapisha video inayoiunga mkono Palestina kwenye Instagram yake, huku klabu yake ya Bayern Munich ikiwa na "mazungumzo ya kina na" na mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco ambaye baadaye alisema "daima atakuwa dhidi ya kila aina ya ugaidi, chuki na vurugu" .
Nchini Ujerumani wiki iliyopita, mlinzi wa Uholanzi Anwar El Ghazi alikatishwa mkataba na Mainz kwasababu ya chapisho la mtandao wa kijamii kuhusu mzozo wa Israel na Gaza ambao klabu hiyo ya Bundesliga iliona kuwa linaunga mkono Palestina.

"Kile ambacho hatujaona Uingereza hadi sasa ni aina ya vipindi ambavyo tumeona huko Ufaransa au Ujerumani ambapo wachezaji wa Kiislamu wametoa kauli za kuunga mkono Palestina na kusimamishwa," alisema Chadwick.
“Lakini kadiri hali inavyoendelea ndivyo masuala haya yanavyozidi kuwa nyeti, kuna uwezekano wa klabu, mchezaji, mfadhili au shirika kutoa tamko, upande mmoja au mwingine.
"Kwa kuongezea katika karne ya 21, tunaonekana kutoweza kuachana au kutenganisha soka kutoka kwa muktadha mpana."
Ni maoni ambayo maneno ya Bassil Mikdadi, mhariri wa tovuti ya Football Palestine, yalionekana kutilia nguvu alipotokea kwenye podikasti ya BBC ya The Sports Desk.
"Tuko katika hali ya mzozo mbaya wa kibinadamu ambao kwa kweli kuna kitu kinachoweza kutekelezeka ambacho tunaweza kuwataka watu wafanye, ambacho ni kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, ambayo ni msimamo usio na upendeleo," alisema.
"Wachezaji kandanda ni sehemu ya jumuiya zetu, hivyo inaleta maana kwao kuuomba."
Hata hivyo wale wanaoshinikizwa kusema hawafanyi hivyo sikuzote. Kwa wale wenye ujasiri wa kutosha kutoa maoni ya umma, Bayley ana ushauri huu.
"Lazima tukumbuke nguvu ya wanamichezo wa hali ya juu kushawishi," mwandishi huyo wa habari wa zamani mwenye shauku kubwa ya uhusiano kati ya michezo na vyombo vya habari alisema.
"Ikiwa wanataka kusema kitu, ni juu ya wachezaji kushauriana na vilabu vyao na kuhakikisha kuwa wanaweka wazi kabisa kuhusu kile wanachoweza na wasichoweza kusema."















