Baba kutoka Israel na Palestina waungana kwa huzuni juu ya vifo vya binti zao

Chanzo cha picha, Rami Elhanan
- Author, Na Suneth Perera
- Nafasi, BBC World Service
Bassam Aramin, Mwislamu wa Kipalestina, na Rami Elhanan, Myahudi wa Kiisraeli, walipoteza binti zao wachanga katika vita vya Mashariki ya Kati.
Wote wawili wanaishi Israeli, ambako watu wengi wangetarajia wawe kama maadui baada ya msiba huo.
Lakini badala ya kulipiza kisasi, Bassam na Rami walichagua njia tofauti: amani na urafiki.
Polisi wa Israel alimpiga risasi binti wa Bassam, Abir, na kumjeruhi vibaya akiwa na umri wa miaka 10. Binti ya Rami, Smadar, aliuawa katika shambulio la kujitoa mhanga la Hamas, akiwa na umri wa miaka 14.
Wanasema "maumivu yasiyovumilika" yamewafanya wajenge urafiki usioweza kutenganishwa kati ya "ndugu" - jinsi wanavyoita uhusiano wao.

Chanzo cha picha, Bassam Aramin / Rami Elhanan
"Sisi si wanyama, na tunaweza kutumia akili zetu. Na unaanza kujiuliza maswali kama haya - je, kuua mtu yeyote kutamrudisha binti yangu?" Rami alihoji.
"Hata kama utaua Wayahudi wengine wote duniani - sio tu Waisraeli - hautawahi kukutana na binti yangu tena," alisema Bassam.
Kikundi cha wazazi
Baada ya binti zao kuuawa, baba wote wawili walijiunga na The Parents Circle Families Forum, kikundi cha amani na maridhiano kwa watu ambao wamepoteza watoto wao kwenye vita.
Rami, ambaye alikuwa mwanajeshi katika Jeshi la Israel, anamtazama Bassam kama kiongozi.
"Yeye ndiye mtu wa karibu zaidi kwangu Duniani... Hatuhitaji maneno kuelewana... Ninamtegemea. Nachukua nguvu kidogo [kutoka] kwake," Rami aliiambia BBC.
Bassam, ambaye alifungwa jela kwa kuwarushia Waisraeli gurunedi katika ujana wake, sasa anamchukulia Rami kama ndugu yake mwenyewe.
"Sisi ni ndugu. Uhusiano wetu uko juu ya mzozo kwa sababu tunashiriki maadili ya aina moja. Tunajali kuhusu wanadamu, tunajali kuhusu raia, tunajali kuhusu demokrasia na uhuru," Bassam aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Rami Elhanan
'Msururu wa ghasia'
Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu Gaza tangu mashambulio ya Oktoba 7 ya Hamas yaliyoua watu 1,400 nchini Israel, huku wengine wasiopungua 239 wakichukuliwa mateka.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema zaidi ya Wapalestina 10,000 wameuawa tangu mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel kuanza.
Ni mwendelezo wa "msururu wa ghasia " wa miongo kadhaa, kama wawili hao wanavyotaja mzozo unaoendelea.

Chanzo cha picha, Bassam Aramin
Kifo cha Smadar
Ilikuwa tarehe 4 Septemba 1997. Smadar alikuwa akinunua vitu na marafiki zake huko Jerusalem wakati bomu lilipolipuka.
Rami na mke wake, Nurit, walitumia saa nyingi kumtafuta sana.
"Unatoka hospitali hadi nyingine kutoka kituo cha polisi hadi kituo kingine " Rami alikumbuka.
"Hadi hatimaye, baadaye usiku huo, unajikuta katika chumba cha kuhifadhia maiti na ndivyo hivyo. Unaona jambo ambalo hutaweza kusahau kwa maisha yako yote."
"Hasira haiwezi kuvumilika. Na ukweli kuhusu maumivu haya, hayaondoki. Yako nawe kwa sekunde 59 kwa kila dakika.'
Bomu la Hamas na risasi ya Israel
Rami na Bassam walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2005 katika mkutano wa Wapiganaji wa Amani, shirika la wapiganaji wa zamani kutoka pande zote mbili, wote wakitafuta amani.

Chanzo cha picha, Bassam Aramin
Tarehe 6 Januari 2007, binti wa Bassam mwenye umri wa miaka 10, Abir, alijeruhiwa vibaya wakati risasi ya mpira iliyopigwa na afisa wa mpaka wa Israel ilipompiga nje ya shule yake kwenye Ukingo wa Magharibi.
Alikufa siku mbili baadaye hospitalini.
"Ninahisi hasira, na bado nina hasira hadi leo, kwa sababu sisi sote ni wanadamu, na ni kawaida kuwa na hasira," Bassam alisema.
'Kisasi hakitapunguza maumivu yako'
"Lakini mimi ni muumini, na ninajua kwamba kulipiza kisasi sio jibu. Haitamrudisha binti yangu."
Rami na mkewe walikuwa wamesimama kando ya Bassam na familia yake hospitalini, wakiwakilisha The Parents Circle.

Chanzo cha picha, Rami Elhanan
"Kwangu mimi, ilikuwa kama kumpoteza binti yangu kwa mara ya pili," Rami alisema.
Siku mbili baadaye Bassam pia alijiunga na The Parents Circle.
Kuvunja 'mzunguko wa vurugu'
Bassam na Rami sasa wanazungumza kwenye mikutano na makongamano kama timu.
"Kama [hakungekuwa] kukaliwa kwa Palestina [hatungehitaji] kuuana. Hatuhitaji kupigana sisi kwa sisi na ni wimbi baada ya wimbi baada ya wimbi. Ni bahari ya damu. Inatosha sasa," Bassam alisema, akizungumzia kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948 kwenye ardhi ambayo hadi wakati huo ilikuwa nchi ya Palestina.
Katika hali isiyo ya kawaida kwa Myahudi wa Kiisraeli, Rami pia anarejelea 'kukaliwa' kwa Palestina alipoulizwa kuhusu jukumu la The Parents Circle katika kupunguza migogoro.
"Hali isiyo ya kawaida ni utawala wa kundi moja la watu juu ya wengine. Hali isiyo ya kawaida ni uvamizi wa Israel. Tulipoteza watoto wetu kwa sababu ya hali hii, na tunahitaji kuibadilisha."

Chanzo cha picha, Getty Images
Wawili hao wanazungumza na vijana, wakiwemo wanafunzi wa shule za upili kutoka pande zote mbili.
Kama Rami anavyoeleza, ni kama "kuingia kwenye mdomo wazi wa volkano hai... Kuna bahari ya damu ndani ya watu hao wawili, hisia nyingi."
"Na jibu ni la kushangaza. Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu sana, unajua, shutuma, wakati mwingine [kutukana], wakati mwingine uchokozi.
"Lakini mwisho wa darasa, [hata kama] kutakuwa na mtoto mmoja tu anayetikisa kichwa kukubali ujumbe huu, ni muujiza. Tuliokoa tone moja la damu. Unajua, katika Uyahudi tone moja la damu ni tone moja la damu ya dunia nzima
Msamaha
Kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Hamas na ya kulipiza kisasi kutoka kwa Israel, Rami alisema kuwa kujadili amani ni changamoto hasa.
"Hali ni nzito sana."
Aliambia BBC kwamba anapokea barua nyingi za chuki.
"Hamas haiwezi kuondolewa kama nzi, kama mbu. Hamas ni wazo. Inabidi ukaushe kinamasi badala ya kuua mbu." Rami alisema.

Chanzo cha picha, Rami Elhanan
Amani ya kudumu
Baba wote wawili wanatumaini kuona amani ya kudumu katika maisha yao.
"Nilikutana na muuaji wa binti yangu mahakamani. Ninamwita mwathiriwa. Nikamwambia... 'Haukuua adui au magaidi; umeua tu msichana asiye na hatia wa miaka 10," Bassam alisema. .
"Yeye ni mwathirika wa elimu yake, simulizi yake, historia yake."
Ujumbe wake sio tu kwa Waisraeli na Wapalestina bali kwa wote wanaohusika katika migogoro na vita duniani kote.
"Unapojiachilia kutoka kwa chuki hii, kutoka kwa kisasi hiki, unakuwa mtu huru. Hakuna anayeweza kukukalia , na huna adui wa kumshinda. Vinginevyo, mimi sio mwoga. Nitalipiza kisasi bila huruma yoyote. , lakini utabadilisha nini? Hakuna."
Imehaririwa na Andrew Webb na kutafsiriwa na Yusuf Jumah












