'Sitaki kufa nikiwa na miaka 24' - Mwanamke wa Gaza aliyekwama kwenye kivuko cha Rafah

Tala
Maelezo ya picha, Tala anasema nduhgu yake mdogo Yazid anaogopa sana, na mishtuko yake inazidi kuwa "mbaya zaidi"
    • Author, Fergal Keane
    • Nafasi, BBC News, Jerusalem

Hili lilikuwa jaribio lao la tatu kuvuka. Lakini kulikuwa na sababu za kutumaini. Taarifa zote za habari zilisema mpaka bila shaka utafunguliwa.

Familia ilikuwa imeitwa na ubalozi wa Jordan na kuambiwa waende kwenye kivuko cha Rafah.

Mama yake Tala Abu Nahleh ni raia wa Jordan. Watu wenye pasipoti za kigeni walikuwa wanatarajia kuruhusiwa kuvuka mpaka sawa na wale waliojeruhiwa na wagonjwa mahututi.

Kakake Tala Yazid mwenye umri wa miaka 15 ni mlemavu na anaugua kifafa. Anaweza kuondoka kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa msaada wa kiti cha magurudumu. Hospitali za Gaza hazina dawa anazohitaji, huku shambulio la bomu likizidisha hali yake.

"Mara tu hali ilipoanzakuwa mbaya," Tala anasema, "aliingiwa na hofu sana, ugonjwa wake wa kifafa uliendelea kuwa mbaya zaidi. Kila wakati ninapofikiria umefikia pabaya zaidi, ndivyo hali yake inazidi kuzorotaza."

Tala anatokea katika familia ya watu sita na yeye tu ndiye anawakimu kimaisha. Alishinda ufadhili wa masomo na kusoma Marekani, Beirut na Lebanon. Jinsi anavyojiamini kwa uwezo wake wa kujieleza ni rahisi kufikiria unaweza kuiongoza familia yake kupitia changamoto za maisha nje ya mipaka ya Gaza.

"Tunajitahidi kuishi. Hatuna uhakika kwamba tutafanikiwa, lakini tunajaribu kufanya kila tuwezalo ili kuishi, kwa sababu sitaki kufa nikiwa na umri wa miaka 24."

Katika kivuko cha Rafah umati wa watu umekuwa ukiangalia orodha ya wale ambao wameidhinishwa kuondoka.
Maelezo ya picha, Katika kivuko cha Rafah umati wa watu umekuwa ukiangalia orodha ya wale ambao wameidhinishwa kuondoka.

Mpaka ni mahali ambapo neno "bahati" lina maana tofauti. Linamaanisha kutoroka mabomu, njaa na ukosefu wa maji.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Linamaanisha pia kuwaacha nyuma wapendwa wako ambao hawana pasi za kigeni za kusafiria, au ambao hawajajeruhiwa vibaya kiasi cha kustahili kuhamishwa, au ambao wamenaswa katikati ya mapigano na hawawezi kufika mpakani.

Idadi ya wale ambao wameondoka, au wataweza kuondoka, ni asilimia ndogo tu ya wakazi wa Gaza wa watu milioni 2.2.

Mona - hakutaka kutaja jina la ukoo - ni raia wa Australia kupitia ndoa. Alikuja mpakani akiwa peke yake huku akiwa amezongwa na mawazo kuhusu familia yake iliyokwama huko Gaza.

“Sina raha hata kidogo kwa sababu naelekea kwengini wakati ndugu zangu, familia yangu yote imesalia nyuma, naomba Mungu akijalia wote wawe mahali salama, hali ni mbaya huko. , ni mbaya sana," anasema.

Makundi ya wanaume yalikusanyika mbele ya karatasi zilizobandikwa kwenye madirisha,zilizoandikwa orodha ya majina wale wanaostahili kutumia kivuko hicho upande wa Gaza.

Kwa jumla, raia 400 wa kigeni na watu waliojeruhiwa waliweza kuondoka Gaza katika siku ya kwanza ya uokoaji siku ya Jumatano.

Sio wote waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuvuka kuingia Misri walifanikiwa siku ya Jumatano
Maelezo ya picha, Sio wote waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuvuka kuingia Misri walifanikiwa siku ya Jumatano

Kufikia mwisho wa siku hiyo, ilikuwa wazi kwa Tala Abu Nahleh kwamba familia yake isingekuwa na bahati hiyo. Walirejea kwa nyumba yao, yenye giza kama ya majirani zao kwa sababu hakuna umeme.

Tala alitutumia ujumbe wa video akisema hajui lakufanya. Alisikika na alionekana kuchoka.

"Tulirudi nyumbani hatuna umeme, hatuna chakula cha leo, hakuna maji safi ya kunywa au hata maji ya kuoga. Na siku nyingine ipepita, kaka yangu hana dawa, na bado tuko hapa. Na ni usiku." Sijui kama tutafanikiwa kesho, lakini natumai hivyo."

Ripoti ya ziada ya kutoka kwa Mahmoud Bassam huko Gaza, na Hanin Abdeen, Alice Doyard, Morgan Gisholt Minard, na John Landy huko Jerusalem.