Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vitisho kwa wanaharakati na wakosoaji Tanzania: 'Tumehukumiwa kifo kwasababu ya kuikosoa serikali'
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu Tito Magoti anasema alichokipitia miaka mitano iliyopita kilikuwa ni kifo hivyo ana ujasiri dhidi ya vitisho vipya anavyovipata hivi sasa
Siku chache zilizopita Magoti aliandika katika mtandao wake wa ‘X’ kwamba amepokea taarifa na onyo kwamba maisha yake yapo hatarini
Pamoja na kuishi kwa tahadhari , Magoti anasema anatambua gharama ya kutetea haki za binadamu kwasababu wapo wengi wasiopenda kile wanaharakati kama yeye wanachokifanya
Decemba 2019, Magoti alitekwa jijini Dar es Salaam na baadae kushtakiwa kwa uhujumu uchumi.
“Mimi ni Mkristo, ninaamini kwamba kilichonitokea kipindi kile kilikuwa ni kifo, kwa hiyo nimeshakufa, na kwamba sitakufa tena. Nina ujasiri wa kutosha kuendelea kuamini kwamba ninachokifanya ni sahihi na kwamba kuna gharama ya hichi tunachokifanya”” amesema Magoti
Hofu ya kutekwa na kupotezwa imeendelea miongoni mwa baadhi ya Watanzania wakati wanaharakati, wanahabari na wanasiasa wakiripoti kupokea jumbe za vitisho na tahadhari.
Tamko la Chama Cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) la tarehe 11 Septemba limelaani taarifa za vitisho dhidi ya Tito Magoti na mawakili wengine Peter Madeleka na Onesmo Olengurumwa
'Rudi nyumbani, wakuulie nyumbani'
Mtangazaji wa kituo cha radio na runinga cha TVE na Efm Roland Barnabas Malaba akifahamika zaidi kama ‘Mandege’ ameripoti pia kupata onyo la jaribio la kutaka kumdhuru.
Malaba anasema taarifa hizo zimeishitua familia yake hata mama na mjomba wake kumtaka apumzike kufanya kazi na kuondoka Dar es Salaam.
“Inaumiza kwasababu unapokea simu kutoka kwa mama anasema ‘chukua likizo, njoo nyumbani, njoo wakuulie nyumbani” amesema Malaba
Ingawa Malaba na Magoti wanaamini taarifa hizo ni za uhakika wamesema hawajazifikisha polisi kwasababu hawana imani na chombo hicho
“Kutoa taarifa kwa polisi ni kuutusi utashi wangu kwasababu hakuna msaada wowote ambao polisi wanaweza kunipatia ikiwa watu wanaokotwa kama kuku hapa Dar es Salaam, jiji linalotambulika kama kitovu cha biashara, polisi watanipa msaada gani?” amesema Magoti
“Sijafanya hivyo kwasababu tunaambiwa hao polisi wenyewe ndio wanaotutafuta. Yaani inakuwaje unaenda kutoa taarifa kwa mtu ambaye mnaambiwa hawa ndio wanaowatafuta, hawa ndio wanaofanya haya matukio?” amehoji Malaba
'Ubaya wetu, ni ukweli wetu'
Wote 'Malaba na Magoti' wanashangazwa na njama za kutaka kuwadhuru wakidai kwamba hakuna kibaya chochote wanachokifanya zaidi ya kutaka uwajibikaji serikalini
“Sisi tunatoa mawazo yetu kwa uzuri kabisa, lakini tunaonekana ni watu wabaya. Yaani ubaya wetu ni ukweli wetu. Kwasababu sisi si watu wabaya, si kwamba tunaitukana serikali. Mimi sijawahi kuitukana serikali hata siku moja, sijawahi kumtukana rais, sijawahi kutukana viongozi. Natoa mawazo yangu kama Mtanzania. Sasa hadi mwenyewe kuna muda nakaa chini najiuliza, kwanini nionekane mbaya kwa kutoa mawazo yangu?” amehoji Malaba
Malaba anasema hakujulishwa jambo moja maalumu ambalo limefanya kuonywa juu ya uwezekano wa kutekwa na kupotezwa, hata hivyo hii si mara yake ya kwanza kupewa onyo.
“Huko nyuma niliwahi kupewa onyo kwamba nilimkosoa rais kwenye safari yake ya Korea (Kusini), nakumbuka hiyo. Nikajiuliza nimewahi kukosoa wapi, nikiangalia tweets zangu sikuona nilipokosoa ila nikakumbuka kwamba niliwahi ku-retweet moja kati ya tweet ilikuwa ni ya chombo cha Habari cha Korea iliyokuwa ikielezea kwamba tunasaini mkataba lakini kuna kitu kuhusu rasilimali zetu, ndio hivyo tu” amesema Malaba
'Bora kufa ukiwa umetekeleza wito'
Magoti amesema hawezi kuacha kuiwajibisha serikali na kupigania haki za binadamu kwasababu anaamini anachokifanya ni wito wake. Ameongeza kwamba anatiwa moyo kuendelea na harakati zake kutokana na matokeo yatokanayo na ukosoaji anaoufanya yeye na wengine pia
“Tunafanya hivi kwa ajili yetu, tunafanya hivi kwa ajili ya taifa letu lakini pia kuna matokeo yanatokea. Tunaopata matokeo mengi tu kupitia hii kazi. Mtazungumza hadi serikali itajitokeza, itakiri udhaifu, na kama haitakiri basi itatafuta namna nyingine ya kufukia kilichofanyika hata kama ni kwa njia za propaganda na kujisafisha lakini tunapata matokeo” amesema Magoti
Mwanasheria huyu amedai kwamba wapo watu wengi ambao hawazungumzi au kujihusisha na harakati kama zake lakini bado wanapotezwa.
“Kuliko kufa umekalia wito wako, ni vyema ukafa ukiwa umeshatekeleza wito wako ambao unadhani kwamba umeitiwa. Kwahiyo mimi nimeshakubali kwamba upande huu wa Maisha ni upande sahihi na pengine kuna siku tutasikilizana. Kwahivyo licha ya ubinadamu, mimi nina ujasiri wa kutosha tu kuendelea kufanya shughuli zangu kwa jinsi ambavyo ninaweza kufanya”
Kuhusu kujihami dhidi ya hatari inayowakabili, Malaba anasema hana namna au nyenzo nyingi sana za kujihakikishia usalama wao zaidi ya kuishi Maisha ya tahadhari.
“Hatuna jeshi, hatuna chochote. Kwahiyo ni kuwa makini tu na maisha yetu, hatujui. Sasa hivi kila mtu tunayemuona mbele yetu tunaona ni adui tu. Kila sura geni tunayoiona, tunaona ni adui kwetu, kila sura geni. Kwahivyo hatuna cha kufanya, tupo tumemkabidhi maisha yetu Mwenyezi Mungu” amesema Malaba