Fahamu kuhusu meli ya mafuta iliyokamatwa na Marekani karibu na pwani ya Venezuela

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wanajeshi wa Marekani waliokuwa na silaha walidhibiti meli ya mafuta katika Bahari ya Caribbean siku ya Jumatano, kufuatia shambulio la hivi karibuni la kampeni ya utawala wa Trump dhidi ya Venezuela.

Katika picha zilizotolewa na Washington, wanajeshi wa Marekani wanaonekana wakipanda meli kutoka kwenye helikopta ili kuikamata meli hiyo.

"Tumeikamata meli ya mafuta nje ya pwani ya Venezuela, kubwa zaidi... kubwa zaidi kuwahi kukamatwa," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.

Baadaye, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Pam Bondi aliarifu kwamba meli hiyo, ambayo ilidhaniwa kuwa imebeba mafuta ghafi ya Venezuela, ililengwa kwa "kuhusika kwake katika mtandao haramu wa usafirishaji wa mafuta unaounga mkono mashirika ya kigeni yanayojihusisha na ugaidi."

Bondi alihakikisha kwamba ukamataji huo ulifanyika karibu na pwani ya Venezuela na kwamba ulifanyika "salama".

Baada ya habari hizo kusambaa, serikali ya Venezuela ilielezea kilichotokea kama "wizi wa wazi na kitendo cha uharamia wa kimataifa" ambacho ni sehemu ya kampeni ya Marekani ambayo "inajibu mpango wa makusudi wa kupora rasilimali zetu za nishati."

"Serikali inathibitisha kwamba itaenda mbele ya vyombo vyote vya kimataifa vilivyopo kukemea uhalifu huu mkubwa wa kimataifa, na itatetea kwa dhati uhuru wake, rasilimali zake asilia na hadhi yake ya kitaifa," ilisema katika taarifa.

Kukamatwa kwa chombo hicho kunakuja huku kukiwa na kampeni ya mashambulizi ya silaha dhidi ya meli katika bahari ya Carribean na Pasifiki na wanajeshi wa Marekani, kwa kisingizio kwamba wanahusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya kwenda Marekani.

Zaidi ya watu 80 wamekufa katika mashambulizi hayo.

Pia unaweza kusoma

Washington pia inaishutumu serikali ya Venezuela kwa kuhusika katika biashara haramu ya dawa za kulevya, jambo ambalo Rais Nicolás Maduro amekataa, akisema kwamba kile Wamarekani wanachokitaka ni mabadiliko ya serikali huko Caracas.

Nini kinafahamika kuhusu meli ya mafuta iliyokamatwa?

Mamlaka nchini Marekani haikutoa taarifa kuhusu ni chombo gani au hatima yake itakuwaje baada ya kukamatwa Jumatano.

Kwa mujibu wa vyanzo vitatu vilivyonukuliwa na mtandao wa Marekani wa CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, ni meli ya mafuta iliyotambuliwa kama "Skipper".

Kampuni inayosimamia masuala ya hatari baharini nchini Uingereza ya Vanguard Tech pia iliripoti kwamba ilikuwa meli hiyo.

Ilibainisha kwamba, kwa mujibu wa ripoti, ni sehemu ya "meli za siri" na kwamba "iliidhinishwa na Marekani kusafirisha mafuta ya Venezuela."

"Skipper" ilikuwa ikisafiri chini ya bendera ya Guyana wakati nafasi yake ya mwisho ilipochapishwa siku mbili zilizopita, kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa meli ya MarineTraffic iliyopitiwa na timu ya BBC Verify.

Vanguard inaamini eneo lake la mwisho linalojulikana kabla ya operesheni ya anga lilikuwa kaskazini mashariki mwa Caracas.

Kampuni hiyo iliiambia BBC Verify kwamba, kwa mujibu wa taarifa ilizokusanya, inaamini kwamba kukamatwa huko kulifanyika mapema Jumatano asubuhi na kwamba meli hiyo inaweza kuwa "imedanganya nafasi yake kwa muda mrefu."

Hii ina maana kwamba inaweza kuwa ilikuwa ikisambaza eneo la uongo na, kwa hivyo, msimamo wake ulioripotiwa kwenye kurasa maalum kama vile MarineTraffic huenda usiwe sahihi.

Ni kawaida kwa meli kusajiliwa chini ya bendera ya nchi nyingine isipokuwa ile ya wamiliki wao, mara nyingi kwa sababu za kikodi.

Lakini usajili katika nchi za tatu pia hutumika kuepuka vikwazo vya kimataifa.

Majibu ya Caracas

Kufuatia kukamatwa huko, serikali ya Venezuela haikudai umiliki wa meli hiyo, lakini ilisema kwamba ilikuwa "wizi wa wazi na kitendo cha uharamia wa kimataifa," ambao "unatokana na mpango wa makusudi wa kupora rasilimali zetu za nishati."

Aliongeza kuwa hii ni pamoja na "wizi wa Citgo," kampuni tanzu ya mafuta ya serikali ya Venezuela PDVSA ambayo imewekewa vikwazo mara nyingi na Washington.

"Siku zote ilikuwa ni kuhusu utajiri wetu wa asili, mafuta yetu, nishati yetu, rasilimali ambazo ni za watu wa Venezuela pekee," serikali ya Maduro ilisema katika taarifa.

Venezuela ina akiba kubwa zaidi ya mafuta iliyothibitishwa duniani.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka Bondi, kukamatwa kwa meli hiyo ni sehemu ya uchunguzi kuhusu "usafirishaji wa mafuta yaliyokuwa yamewekewa vikwazo."

Bondi alionyesha kuwa operesheni hiyo ilihusisha Ofisi ya Upelelezi ya Shirikisho (FBI), Ofisi ya Upelelezi wa Usalama na Walinzi wa Pwani wa Marekani, kwa usaidizi kutoka Idara ya Ulinzi.

"Walitekeleza agizo la kukamatwa kwa meli ya mafuta iliyotumika kusafirisha mafuta yaliyowekewa vikwazo kutoka Venezuela na Iran."

Washington imeyaadhibu magenge mawili yenye asili ya Venezuela, Tren de Aragua na Cartel de los Soles, kama "mashirika ya kigaidi".

Kufuatia kukamatwa, bei ya mafuta ilipanda kidogo Jumatano, na kuzidisha wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chanzo hicho cha nishati kwa muda mfupi.