Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo kuhusu eneo lisilojulikana sana lenye utajiri wa mafuta unaosababisha wasiwasi wa kimataifa
- Author, Norberto Paredes
- Nafasi, BBC World Service
Katikati ya Amerika, mivutano ya mpaka juu ya eneo linaloshindaniwa inasababisha wasiwasi wa kimataifa.
Mzozo ni juu ya uhuru wa Essequibo, eneo linalounda theluthi mbili ya Guyana (ina ukubwa sawa na Tunisia, na kubwa kuliko Uingereza, Cuba au Ugiriki).
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro alitangaza wiki hii kwamba eneo la Venezuela katika eneo hilo litaundwa, baada ya nchi hiyo kufanya kura ya maoni yenye utata kuhusu suala hilo. Pia aliamuru makampuni yanayomilikiwa na serikali kuanza kuchunguza na kutumia hifadhi ya mafuta katika eneo hilo na kuunda eneo jipya la ulinzi wa ardhi inayozozaniwa.
Hilo lilichukuliwa kuwa “tishio lililo karibu” na Guyana, ambayo imedhibiti Essequibo kwa zaidi ya karne moja.
Rais wa Guyana Irfaan Ali alisema nchi hiyo inachukua hatua zinazohitajika kujilinda na Venezuela na imefikia washirika wa kikanda, ikiwa ni pamoja na Kamandi ya Kusini ya jeshi la Marekani.
Mvutano unaoongezeka umelaaniwa na nchi kadhaa za Magharibi, huku Marekani ikitoa wito wa "azimio la amani" na Uingereza ikizingatia hatua za hivi majuzi za serikali ya Venezuela kuwa "hazina haki".
Lakini, ni eneo gani linalozozaniwa la Essequibo na kwa nini mzozo huu unaleta wasiwasi?
1. Eneo la Essequibo lina umuhimu gani?
Essequibo ni ardhi yenye pori lenye utajiri wa mafuta linalosimamiwa na jirani wa Venezuela, Guyana.
Pia inajulikana kama Guayana Esequiba, eneo la 159,500-kilomita mraba (61,600-maili mraba) linaunda theluthi mbili ya jumla ya ardhi inayodhibitiwa na Guyana kwa sasa. Ni nyumbani kwa raia 125,000 kati ya 800,000 wa Guyana.
Mkoa huo una utajiri wa dhahabu, shaba, almasi, chuma, bauxite na alumini.
Uchumi wa Guyana umekuwa ukipitia mabadiliko tangu kugunduliwa kwa mafuta ghafi kwenye maji kutoka eneo linalozozaniwa mnamo 2015.
Kampuni ya Marekani ya Exxon Mobil ilipewa leseni za uchunguzi wa mafuta na Guyana, na hivyo kuongeza uzalishaji, akiba na mapato ya Guyana.
2. Ni nini historia ya mzozo huo?
Essequibo ilikuwa sehemu ya Utawala wa Uhispania wa Venezuela wakati wa karne ya kumi na tano.
Wakati Venezuela ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uhispania mnamo 1811, ilichukua ilitwa majukumu ya utawala juu Essequibo.
Miaka mitatu baadaye Uingereza ilitia saini mkataba na Uholanzi kupata karibu kilomita za mraba 51,700 mashariki mwa Venezuela, bila kufafanua mpaka wa magharibi wa kile ambacho kingekuwa British Guiana.
London ilimteua mgunduzi Robert Schomburgk mnamo 1840, ambaye alichora mstari uliodai kilomita za mraba 80,000 za ziada na ambao ulipanuliwa miongo minne baadaye.
Mwaka 1895 Marekani ilipendekeza kwamba mzozo huo utatuliwe katika usuluhishi wa kimataifa na miaka minne baadaye Mkataba ya Usuluhishi wa Paris ulitolewa, ambao uliacha eneo hilo chini ya utawala wa Uingereza.
Baada ya hati zilizohoji kutopendelea kwa uamuzi huo kufichuliwa miongo minne baadaye, Venezuela iliona kuwa ni batili na kurudisha madai yake.
Mnamo 1966, Uingereza ilitoa uhuru kwa Guyana na pande zote zilijitolea kutafuta suluhu, lakini hakukuwa na uamuzi wa Umoja wa Mataifa na kesi hiyo ilisimama wakati wa serikali ya Hugo Chavez kutokana na uhusiano mzuri kati ya marehemu rais wa Venezuela na Georgetown.
Lakini mvutano kati ya Venezuela na Guyana uliibuka baada ya ugunduzi wa mafuta wa 2015.
Wachambuzi wanasema sasa kwamba serikali ya Maduro ina malengo ya kiuchumi na kisiasa katika madai yake juu ya Essequibo.
Maduro alitoa wito wa maandamano kadhaa ya "umoja wa kitaifa" "kulinda" Essequibo na kuwataka watu mashuhuri wa Venezuela kujihusisha na mzozo huo.
Kama sehemu ya "umoja huu wa kitaifa", serikali ya Venezuela ilifanya kura ya maoni yenye utata kufuatia kampeni kali ya kushinikiza raia kuunga mkono uhuru wa Venezuela dhidi ya Essequibo.
Wakosoaji wanasema Maduro anajaribu kuonekana kama mlinzi wa maslahi ya Venezuela, katikati ya shinikizo la kimataifa na wito wa uchaguzi huru na wa haki mwaka 2024.
Hivi majuzi Marekani ilipunguza vikwazo ilivyokuwa imeweka kwa sekta ya mafuta ya Venezuela kwa kubadilishana na serikali kuondoa marufuku dhidi ya mgombea mkuu wa upinzani, Maria Corina Machado.
Hata hivyo, marufuku ya Bi Machado kugombea wadhifa huo bado ingalipo.
3. Nini kilifanyika baada ya kura ya maoni?
Zaidi ya 95% ya Wavenezuela waliojitokeza kupiga kura waliunga mkono madai ya Venezuela kuhusu Essequibo, kulingana na maafisa.
Katika kura hiyo ya maoni, serikali ya Venezuela iliwataka wapiga kura kuunga mkono msimamo wake kuhusu mzozo huo.
Swali lililokuwa na utata zaidi lilikuwa la tano, ambalo liliwauliza Wavenezuela ikiwa walikubaliana na "kuundwa kwa jimbo la Guayana Esequiba" na "kuingizwa kwake katika ramani ya eneo la Venezuela".
Elvis Amoroso, mkuu wa Baraza la Taifa la Uchaguzi na mshirika wa karibu wa Rais Maduro, alisema kuwa kura 10.5m zilipigwa.
Vyombo vya habari vya upinzani pia viliripoti kuwa vituo vya kupigia kura vimekuwa kimya sana siku nzima, hivyo kutilia shaka madai ya serikali kwamba watu wengi walijitokeza kupiga kura.
Kabla ya kura hiyo ya maoni, Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliionya Venezuela kutochukua hatua yoyote ambayo inaweza kubadilisha hali iliyopo Essequibo.
Kura hiyo ya maoni ilisababisha wasiwasi katika nchi jirani ya Guyana na serikali yake ilisema ilikuwa "macho".
Hata hivyo, mvutano uliibuka Jumanne baada ya Maduro kutangaza mipango ya kuunda eneo la Venezuela huko Essequibo na kuamuru kampuni zinazomilikiwa na serikali kutoa mafuta, gesi na madini mengine katika eneo hilo.
Rais wa Guyana Irfaan Ali alisema kwamba "wanajitayarisha kwa hali mbaya zaidi", ingawa pia alisisitiza kwamba anataka "hili kutatuliwa kwa njia ya amani".
Ali alionya kuwa nchi yake inaungwa mkono kijeshi na Marekani na inaungwa mkono na Uingereza na Jumuiya ya Madola na shirika la Jumuiya ya Caribbean.
Kamandi ya Kusini mwa Marekani ilitangaza mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Vikosi vya Ulinzi vya Guyana siku ya Alhamisi.
Mazoezi hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano kati ya majeshi yote mawili na katika ngazi ya kikanda, kulingana na taarifa .
Ingawa Kamandi ya Kusini ilihakikishia haya ni mazoezi ya kawaida, wataalam walitafsiri kama jibu kwa hatua za hivi karibuni za serikali ya Venezuela.
Mamlaka ya Venezuela imekosoa hatua hiyo . Waziri wa ulinzi Vladimir Padrino alisema ni "uchochezi".
4. Je! ni nini maoni ya jumuiya ya kimataifa?
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano wa dharura siku ya Ijumaa kuhusu mzozo unaokua kwa kasi ambao Guyana ilisema "unatishia amani na usalama wa kimataifa".
Kamandi ya Kusini mwa Marekani ilisema katika taarifa kwamba "itaendeleza ahadi yake kama mshirika wa usalama anayeaminika wa Guyana na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alizungumza na rais wa Guyana "kuthibitisha tena uungaji mkono usioyumba wa Marekani kwa uhuru wa Guyana".
Blinken alitoa wito wa "azimio la amani" na kwa pande zote "kuheshimu tuzo ya usuluhishi ya 1899 inayoamua mpaka wa ardhi kati ya Venezuela na Guyana, isipokuwa, au hadi, wahusika wafikie makubaliano mapya, au chombo cha kisheria chenye uwezo kitaamua vinginevyo".
Blinken na Ali walibainisha amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliyotolewa tarehe 1 Disemba, ambayo ilitaka wahusika kujiepusha na hatua yoyote ambayo inaweza kuzidisha au kuongeza mzozo.
Uingereza ilisema "inasikitishwa na hatua za hivi majuzi zilizochukuliwa na Venezuela, kuhusiana na eneo la Essequibo la Guyana".
"Tunaamini kuwa hii haina msingi na inapaswa kukoma," Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema kwenye mitandao ya kijamii.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva pia alionyesha "wasiwasi unaokua" wakati wa mkutano wa kilele wa uchumi wa Amerika Kusini huko Rio de Janeiro siku ya Alhamisi.
"Ikiwa kuna jambo moja ambalo hatutaki hapa Amerika Kusini ni vita," Lula alisema.
Wanachama wa muungano wa kibiashara wa Mercosur "wanaonyesha wasiwasi wao mkubwa juu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Jamhuri ya Bolivari ya Venezuela na Jamhuri ya Ushirika ya Guyana," ilisema taarifa ya pamoja kutoka Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay, nchi wanachama wa umoja huo.
Wanachama wasio wa Mercosur Chile, Colombia, Ecuador na Peru pia walitia saini taarifa hiyo.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi