Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump anaitaka Marekani kusonga mbele baada ya sakata la Epstein..lakini huenda isiwe rahisi
Katika miezi miwili iliyopita, Wizara ya Sheria ya Marekani imetoa mamilioni ya nyaraka zinazohusiana na uchunguzi wake wa biashara ya ngono dhidi ya Jeffrey Epstein. Sasa, rais anataka taifa liendelee na mambo mengine, lakini je, litaweza?
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche, amesema kuwa mapitio ya serikali kuhusu faili za Epstein, yaliyohitajika na sheria iliyopitishwa na Congress mwezi Novemba , yamekamilika, na hakuna msingi wa kufungua mashtaka mapya.
"Kuna mawasiliano mengi. Kuna barua pepe nyingi. Kuna picha nyingi," Blanche alisema Jumapili. "Lakini hayo hayatoshi kuturuhusu kumshtaki mtu."
Ingawa mapitio ya wizara yanaweza kuwa yamekamilika, katika Bunge la Marekani, Baraza la Wawakilishi linaendelea na uchunguzi wake binafsi kuhusu Epstein.
Rais wa zamani Bill Clinton na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton wanatarajiwa kutoa ushahidi baadaye mwezi Februari, baada ya Warepublican kutishia kuwashikilia kwa kukaidi Congress.
Wakati huohuo, wanachama wa Congress na waathirika wa Epstein wanaendelea kuitaka serikali itoe taarifa zaidi, wakielekeza kwenye nyaraka wanazodai zipo lakini hazikujumuishwa katika faili zilizotolewa.
Hii ni ishara nyingine ya jinsi ilivyo vigumu kuachana na sakata hili kwa wale, kama Rais Donald Trump, ambao kwa wazi wangependa kuliacha.
Kwa sasa, hata hivyo, rais ameibuka kutoka kwenye dhoruba hiyo bila dalili za madhara ya kudumu.
Hilo haliko hivyo kwa baadhi ya watu wengine matajiri na wenye ushawishi mkubwa, ambao uhusiano wao na Epstein ulielezewa kwa uwazi zaidi katika nyaraka hizo, na ambao waliendelea kuwasiliana naye muda mrefu baada ya yeye kuhukumiwa kwa kosa la ngono mwaka 2008.
Kwa mfano, Andrew Mountbatten, Windsor, aliyekuwa mwana mfalme, Lord Peter Mandelson, aliyekuwa balozi wa Uingereza nchini Marekani, na aliyekuwa Waziri wa Hazina wa Marekani Larry Summers, wote wamekumbwa na athari za kitaaluma na binafsi kutokana na uhusiano wao na Epstein.
Mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates na bilionea wa teknolojia Elon Musk, miongoni mwa wengine, wamelazimika kutoa maelezo kuhusu barua pepe na kutajwa kwa majina yao katika nyaraka zilizotolewa.
Rais, alipokuwa Ikulu ya White House siku ya Jumanne, alisema anaamini kuwa "ni wakati wa kweli kwa taifa kuhamia kwenye mambo mengine."
"Hakuna chochote kilichotoka kunihusu mimi," alisema Trump, ambaye mara kwa mara amekanusha kufanya kosa lolote kuhusiana na Epstein.
Hata hivyo, hilo si sahihi kabisa.
Jina la rais lilitajwa zaidi ya mara 6,000 katika nyaraka hizo. Alitajwa mara kwa mara na Epstein na washirika wake. Wanaume hao wawili, wote wakazi wa New York City na West Palm Beach, walikuwa na uhusiano wa kirafiki kwa kiasi kikubwa katika miaka ya 1990 hadi, kulingana na Trump, walipokosana mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Moja ya marejeo hayo ya Trump, katika barua pepe iliyotolewa mwezi Desemba, yalivutia umakini.
"Nataka utambue kwamba mbwa ambaye hakubweka ni Trump," Epstein aliandika katika barua pepe ya mwaka 2011 kwa mshirika wake aliyekuwa tayari amehukumiwa, Ghislaine Maxwell. "[Mwathiriwa] alitumia saa nyingi nyumbani kwangu akiwa naye, lakini hajawahi kutajwa hata mara moja."
Katika rundo la hivi karibuni la faili, Wizara ya Sheria ya Marekani pia ilitoa orodha ya vidokezo vya FBI ambavyo havijathibitishwa, ikiwemo baadhi ya mwaka 2016 wakati Trump alikuwa katikati ya kampeni yake ya kwanza ya urais.
Orodha hiyo inajumuisha tuhuma nyingi za unyanyasaji wa kingono zilizotolewa dhidi ya Trump, Epstein na watu wengine maarufu.
Vidokezo hivyo vya FBI, vingi vikiwa havina ushahidi wa kuviunga mkono, vilitoweka kwa muda kutoka kwenye tovuti ya nyaraka ya Wizara ya Sheria siku ya Jumamosi.
Hilo lilichochea hisia kwa baadhi ya watu kwamba wizara hiyo ilikuwa ikifanya kazi kumlinda rais.
"Baadhi ya nyaraka zina madai yasiyo ya kweli na ya kuchochea hisia dhidi ya Rais Trump yaliyowasilishwa kwa FBI kabla tu ya uchaguzi wa 2020," Idara ya Haki ilisema kuhusu faili hizo.
"Madai hayo hayana msingi na ni ya uongo, na kama yangekuwa na chembe yoyote ya uaminifu, bila shaka yangekuwa tayari yametumiwa dhidi ya Rais Trump."
Kumekuwa na picha chache mpya za Trump, lakini hakuna hata moja iliyotoa taarifa mpya zaidi kuliko picha na video ambazo kwa muda mrefu zimekuwa wazi kwa umma.
Na Trump, ambaye anajulikana kuepuka kutumia barua pepe, hana rekodi yoyote iliyoandikwa ya mawasiliano ya moja kwa moja na Epstein. Hakuna taarifa mpya inayodhoofisha kwa kiasi kikubwa dai la rais kwamba urafiki wake na Epstein ulimalizika karibu mwaka 2004.
Kile kilichoonekana kuwa karibu zaidi na "bomu la kisiasa" ,ujumbe mchafu na wa kupendekeza ambao inadaiwa Trump alimwandikia Epstein kwa ajili ya kitabu cha kumbukumbu cha siku yake ya kuzaliwa mwaka 2002, ulitolewa na mali ya Epstein, siyo serikali.
Trump amekanusha vikali uhalisia wa ujumbe huo.
Wademocrat wamekanusha kuwa ukosefu wa ushahidi mkali dhidi ya Trump unaweza kumaanisha kwamba wizara ilihifadhi nyaraka zinazomshutumu.
"Unasema nyaraka zote zimetolewa," Kiongozi wa Upinzani Seneti, Chuck Schumer, aliandika katika taarifa. "Je, hiyo inajumuisha yote ya memos za washirika wa usaliti, memos za ulinzi wa kampuni, ripoti za awali za Polisi wa Palm Beach, n.k.?"
"Je, kila nyaraka inayotaja neno Trump imeachiliwa?"
Mmoja wa waathirika wa Epstein, Lisa Phillips, aliiambia BBC kwamba yeye na wenzake hawakuridhika na hatua za wizara hiyo kuhusu Epstein.
"Imenyanyasa mahitaji yetu yote matatu," alisema.
"Namba moja, nyaraka nyingi bado hazijafunuliwa. Namba mbili, tarehe iliyowekwa kwa ajili ya kuachiliwa imepita kwa muda mrefu. Na namba tatu, DOJ ilitoa majina ya wengi wa waokokaji, na hilo si sawa. Tunahisi wanacheza michezo nasi, lakini hatutaacha kupigania haki."
Hasira na kukata tamaa miongoni mwa wafuasi wa Trump juu ya kusitasita kwa serikali kuachilia nyaraka zote za Epstein, labda tishio kubwa zaidi kwa hadhi ya kisiasa ya rais, inaonekana kupungua kwa wimbi hili la nyaraka mpya zilizotolewa.
Ingawa baadhi ya wakosoaji, kama mwanacongress wa zamani Marjorie Taylor Greene, wanaendelea kumlaumu rais, sehemu kubwa ya wafuasi wake wa Make America Great Again inaonekana kuhamia mbali na habari za Epstein.
Wademocrat, wakirejelea masharti ya kisheria, wanadai kupata nakala zisizofichuliwa za nyaraka nyingi zilizotolewa. Na ushahidi wa Clinton unaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa kisiasa.
Rais anaweza kudai kuwa ni wakati wa taifa kuhamia mambo mengine, lakini miaka baada ya kifo cha Epstein, sakata hili limeonesha kuwa bado linaishi.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi