Wafanyakazi wa Korea Kaskazini waiambia BBC kwamba wanafanya kazi 'kama watumwa' nchini Urusi

Picha ikionyesha mfanyikazi wa Korea Kaskazini akiwa amevalia magwanda ya kazi
Maelezo ya picha, BBC inafahamu zaidi ya Wakorea Kaskazini 50,000 hatimaye watatumwa kufanya kazi nchini Urusi
    • Author, Jean Mackenzie
    • Nafasi, Seoul correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Maelfu ya raia wa Korea Kaskazini wanaripotiwa kupelekwa Urusi kufanya kazi katika mazingira ya utumwa, ili kujaza pengo kubwa la ajira lililosababishwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Uchunguzi wa BBC umebaini kuwa hatua hii inachochewa na uhusiano unaozidi kuimarika kati ya Moscow na Pyongyang.

Urusi imekuwa ikitegemea misaada ya kijeshi kutoka Korea Kaskazini, ikijumuisha makombora, risasi na hata wanajeshi.

Sasa, kwa kuwa idadi kubwa ya wanaume wa Urusi wamefariki vitani, kujeruhiwa, au kukimbilia nje ya nchi, duru za ujasusi wa Korea Kusini zinasema Moscow inazidi kutegemea wafanyakazi wa Korea Kaskazini kama suluhisho la muda mrefu.

BBC imewahoji wafanyakazi sita wa Korea Kaskazini waliotoroka Urusi tangu vita vilipoanza, pamoja na maafisa wa serikali, watafiti, na watu wanaosaidia kuwaokoa wafanyakazi hao.

Walieleza kwa kina hali mbaya ya kazi wanayokumbana nayo, ikiwa ni pamoja na ulinzi mkali, ukosefu wa uhuru wa kimsingi, na mateso ya kimwili.

Jin, mmoja wa wafanyakazi hao, alisema kuwa mara alipowasili katika eneo la Mashariki mwa Urusi, alisindikizwa moja kwa moja kutoka uwanja wa ndege hadi eneo la ujenzi na afisa wa usalama wa Korea Kaskazini.

Alikatazwa kuzungumza au kutazama mazingira ya nje.

"Dunia ya nje ni adui yetu," alimwambia afisa huyo.

Aliwekwa kazini mara moja akijenga majengo ya ghorofa kwa zaidi ya saa 18 kwa siku, huku akiwa na mapumziko ya siku mbili pekee kwa mwaka.

Wafanyakazi wote sita tuliozungumza nao walielezea utumwa waliokumbana nao wakiamka saa kumi na mbili asubuhi na kulazimishwa kujenga vyumba vya juu hadi saa 2 asubuhi iliyofuata, na siku mbili tu za mapumziko kwa mwaka.

Tumebadilisha majina yao ili kuwalinda.

Kim Jong Un amemtumia Vladimir Putin silaha na wanajeshi kupigana vita vyake nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tae, mfanyakazi mwingine ambaye alifanikiwa kutoroka mwaka jana, alieleza jinsi mikono yake ilivyokuwa ikikakamaa kila asubuhi kutokana na uchovu wa kazi ya siku iliyotangulia. Chan, pia mfanyakazi wa ujenzi, alisema walipokuwa wakilazimika kufanya kazi hadi kupoteza fahamu kwa uchovu.

''Lakini wale waliokuwa wakilala wakiendelea na ujenzi kwa kusimama walichapwa na wasimamizi wao.''

Ilikuwa kana kwamba tunakufa polepole," alisema Chan.

Prof. Kang Dong-wan wa Chuo Kikuu cha Dong-A, Korea Kusini, amesema wafanyakazi hawa hukabiliana na mazingira hatarishi ya kazi, mara nyingi wakilazimika kufanya kazi usiku bila taa wala vifaa vya usalama vya kutosha.

Wanakaa kambini katika maeneo ya ujenzi usiku na mchana, wakilindwa kwa karibu na maafisa wa ujasusi wa Korea Kaskazini. Hukaa kwenye makontena yaliyojaa uchafu na wadudu au kwenye majengo yasiyokamilika, huku wakijisitiri na plastiki milangoni dhidi ya baridi kali.

Mmoja wao, Nam, alieleza jinsi alivyoanguka kutoka ghorofa ya nne na kuvunjika sura, lakini hata hivyo hakuruhusiwa kwenda hospitalini.

Pia unaweza kusoma:
Picha ikimuonyesha mwanamume wa Korea Kaskazini anayefanya kazi kwenye tovuti ya ujenzi yenye theluji nchini Urusi bila vifaa vyovyote vya usalama
Maelezo ya picha, Picha ikimuonyesha mwanamume wa Korea Kaskazini anayefanya kazi kwenye tovuti ya ujenzi yenye theluji nchini Urusi bila vifaa vyovyote vya usalama

Hadi mwaka 2019, maelfu ya wafanyakazi wa Korea Kaskazini walikuwa wakifanya kazi Urusi, na mapato yao yaliingiza mamilioni ya dola kwa utawala wa Kim Jong Un. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa ulipiga marufuku rasmi ajira hiyo, kwa lengo la kuzuia ufadhili kwa programu ya silaha za nyuklia ya Pyongyang.

Licha ya marufuku hiyo, takriban wafanyakazi 10,000 walipelekwa Urusi mwaka jana, na inakadiriwa zaidi ya 50,000 huenda wakaingia mwaka huu.

Wengi wao huingia kwa visa za wanafunzi, njia ambayo wachambuzi wanaiona kama mbinu ya Urusi kukwepa vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Katika tukio la nadra mwezi Juni, Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, alikiri kuwa wafanyakazi 5,000 kutoka Korea Kaskazini wangetumwa kujenga upya mkoa wa Kursk, ambao awali ulikuwa umetekwa na Ukraine.

Korea Kusini pia inaamini kwamba wafanyakazi hao huenda wakapelekwa kwenye maeneo ya Ukraine yaliyotwaliwa na Urusi kwa ajili ya ujenzi mpya.

"Urusi ina uhaba mkubwa wa nguvu kazi kwa sasa, na wafanyakazi kutoka Korea Kaskazini wanatoa suluhisho bora ni wa gharama nafuu, wachapakazi, na hawaleti shida," anasema Prof. Andrei Lankov, mtaalamu wa mahusiano ya Korea Kaskazini na Urusi.

Maua haya yalitumwa kwa Kim Jong Un na makampuni mbalimbali ya ujenzi ya Urusi mwezi Aprili, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini

Chanzo cha picha, KCNA

Maelezo ya picha, Maua haya yalitumwa kwa Kim Jong Un na makampuni mbalimbali ya ujenzi ya Urusi mwezi Aprili, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini

Kwa wengi nchini Korea Kaskazini, ajira ya nje huonekana kama fursa ya kipekee ya kupata fedha.

Wengi huondoka kwa matumaini ya kuondoa familia katika umasikini, au kuanzisha biashara watakaporejea.

Lakini ukweli ni mchungu.

Kikosi kinachochaguliwa baada ya uhakii hutakiwa kuacha familia zao nyumbani.

Mshahara wao mkubwa hupelekwa moja kwa moja kwa serikali kama ada ya uaminifu, na kinachobakia ni kiasi kidogo tu mara nyingi kati ya dola 100 hadi 200 kwa mwezi ambacho huchukuliwa kuwa madaftari ya ahadi, wakiahidiwa kulipwa wanaporudi nyumbani.

Hii ni mbinu ya kuwadhibiti ili wasitoroke.

"Nilijiona kama mfungwa gereza lisilo na milango," alisema Tae, baada ya kugundua wafanyakazi kutoka Asia ya Kati walikuwa wakilipwa mara tano zaidi kwa kazi ndogo zaidi.

Jin anakumbuka walivyokuwa wakidhihakiwa na wafanyakazi wengine:

"Hamtambuliki kama watu. Ninyi ni mashine zinazozungumza."

Wakati fulani, meneja wa Jin alimwambia kuwa huenda hatapokea pesa zozote atakaporejea Korea Kaskazini kwa sababu serikali ilizihitaji badala yake.

Hapo ndipo alipoamua kuhatarisha maisha yake ili kutoroka.

Tae alichukua uamuzi wa kuasi baada ya kutazama video za YouTube zinazoonyesha ni kiasi gani wafanyakazi nchini Korea Kusini walilipwa.

Usiku mmoja, alipakia vitu vyake kwenye mjengo wa mapipa, akajaza blanketi chini ya shuka zake ili ionekane kana kwamba bado alikuwa amelala, na akatoka nje ya eneo lake la ujenzi.

Alisimamisha teksi na kusafiri maelfu ya kilomita kote nchini ili kukutana na wakili aliyesaidia kupanga safari yake kuelekea Seoul.

Katika miaka ya hivi majuzi, idadi ndogo ya wafanyikazi wameweza kupanga kutoroka kwao kwa kutumia simu mahiri zilizopigwa marufuku, zilizonunuliwa kwa kuokoa posho ndogo ya kila siku waliyopokea kwa sigara na pombe.


Picha ya mwanamume wa Korea Kaskazini akiwa mbele ya ghorofa ya Seoul
Maelezo ya picha, Vibarua wachache wamefanikiwa kutoroka Urusi wakati wa vita hivyo na kufika Seoul

Katika juhudi za kuzuia Raia wa Korea Kaskazini kutoroka zaidi, mamlaka za Korea Kaskazini zimeongeza ukandamizaji.

Prof. Kang anasema wafanyakazi sasa hulazimika kupitia mafunzo ya kiitikadi na vikao vya kujitathmini, wakitakiwa kuapa utii kwa Kim Jong Un na kueleza mapungufu yao binafsi.

Hapo awali walikuwa wakiruhusiwa kutoka mara moja kwa mwezi kwa makundi, lakini sasa wanatoka kwa nadra sana, na kwa usimamizi mkali.

Kwa mujibu wa Kim Seung-chul, mwanaharakati anayewasaidia wakimbizi kutoka Korea Kaskazini, idadi ya waliotoroka kutoka Urusi imepungua kwa nusu tangu mwaka 2022 kutoka wastani wa watu 20 kwa mwaka hadi 10 pekee.

"Wafanyakazi hawa wanaweza kuwa urithi wa kudumu wa urafiki wa vita kati ya Kim na Putin," alisema Prof. Lankov.

"Hata baada ya vita kuisha, uhamishaji huu wa wafanyakazi huenda ukaendelea kwa miaka mingi

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid