Vita vya Ukraine: Kyiv yalaani madai ya Urusi ya bomu la mionzi

Ukraine imelaani madai ambayo hayajathibitishwa na Urusi kwamba Kyiv inaweza kutumia "bomu chafu" ama la mionzi - vilipuzi vya kawaida vilivyochanganywa na nyenzo za mionzi.

Rais Volodymyr Zelensky alisema hii ina maana kwamba Urusi yenyewe inaweza kuandaa mashambulizi ya aina hii.

Washirika wa Ukraine pia walipuuzilia mbali madai hayo, huku Marekani ikisema "inapinga kisingizio chochote cha Urusi kutaka kuendeleza vita".

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alitoa matamshi hayo machafu ya bomu alipozungumza na mwenzake wa Uingereza Ben Wallace.

Alisema "anajali kuhusu uwezekano wa uchochezi wa Kyiv unaohusisha matumizi ya bomu la mionzi

Siku ya Jumapili, Bw Shoigu pia alipigiwa simu na mawaziri wa ulinzi wa Marekani, Ufaransa na Uturuki, wakitoa tahadhari ya Moscow. Hakutoa ushahidi wa kuunga mkono mashtaka yake.

Akijibu hili, Rais Zelensky aliishutumu Urusi kuwa "chanzo cha kila kitu kichafu ambacho kinaweza kufikiriwa katika vita hivi".

Alisema Urusi inatishia ulimwengu "kwa maafa ya mionzi" katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho ilikiteka na pia alizungumzia vitisho vya Moscow vya kulipua bwawa kubwa kusini mwa Ukraine. Kremlin inakanusha madai hayo.

Kiongozi wa Ukraine pia alisisitiza kwamba "ulimwengu unapaswa kujibu kwa hatua kali zaidi".

Wakati huo huo, Bw Wallace alisema alikanusha madai ya Bw Shoigu kwamba "Ukraine inapanga hatua zinazowezeshwa na nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Uingereza, ili kuzidisha mzozo nchini Ukraine".

Pia alionya kwamba madai kama hayo "hayapaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuongezeka zaidi".

Maoni kama hayo yalitolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, ambaye alizungumza na Bw Shoigu siku ya Jumapili, katika simu ambayo ilikuwa ya pili ndani ya siku kadhaa.

Na katika taarifa yao ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Uingereza na Marekani walisema serikali zao "zote zinapinga madai ya uwongo ya Urusi kwamba Ukraine inajiandaa kutumia bomu chafu kwenye eneo lake", na kusisitiza kwamba wataendelea kuiunga mkono Ukraine katika "vita vya kikatili vya Rais [Vladimir] Putin vya uchokozi".

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanaona kuwa shutuma hizo za Urusi zinakuja baada ya msururu wa kushindwa kwa jeshi la Urusi na huku wanajeshi wa Ukraine wakiendelea na operesheni zao za kukabiliana na mashambulizi mashariki na kusini mwa nchi hiyo.

Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita (ISW) ilisema katika mfululizo wa ujumbe wa Twitter kwamba Bw Shoigu "huenda alitaka kupunguza au kusimamisha msaada wa kijeshi wa Magharibi kwa Ukraine na pengine kudhoofisha muungano wa Nato katika wito wa kutisha".

Hata hivyo, ISW iliongeza: "Kremlin haiwezekani kuandaa shambulio la bomu la mionzo ili kupata kisingizio cha kuishambulia Ukraine kwa kile ambacho huitwa 'False Flag'

Madai ya Shoigu yanaendeleza kampeni ya muda mrefu ya habari ya Urusi."

Katika matukio mengine Jumapili:

  • Kampuni ya nishati ya serikali ya Ukraine imesema imerejesha sehemu ya vifaa vya umeme kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora ya Urusi na ndege zisizo na rubani.
  • Shirika la utangazaji la RT la Urusi lilisema linamsimamisha kazi mfanyakazi wake mkuu Anton Krasovsky, baada ya kusikika akisema katika kipindi cha TV kwamba watoto wa Ukraine wanapaswa kuzama au kuchomwa moto hadi kufa.
  • Idara ya usalama ya Ukraine SBU ilithibitisha kwamba Vyacheslav Bohuslayev, mkuu wa zamani wa kampuni ya Motor Sich, alikamatwa baada ya kushtakiwa kwa kuuza injini za anga nchini Urusi kinyume cha sheria.