Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa UKraine: Je, ndege hii ya kivita iliangukaje kwenye jengo la ghorofa nchini Urusi?
Uchunguzi unaendelea kuhusu ajali ya ndege ya kivita katika mji wa Yeysk nchini Urusi siku ya Jumatatu ambapo watu 15 waliuawa wakiwemo watoto watatu. Video na picha zimejitokeza kwenye mitandao ya kijamii, na kuturuhusu kujaribu kuunganisha kile kilichotokea.
Nini tunachojua?
Siku ya Jumatatu jioni, ndege ya kivita ya Urusi aina ya Su-34 iligonga jengo la makazi katika mji wa Yeysk nchini Urusi, zaidi ya maili 100 (160km) kutoka eneo la mji wa Ukraine unaoshikiliwa na Urusi Wizara ya ulinzi ya Urusi imedokeza kuwa hitilafu katika mojawapo ya injini ya ndege hiyo ndiyo chanzo cha ajali hiyo.
Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha moto mkubwa na moshi ukifuka kutoka kwenye eneo la juu la jengo hilo. Video nyingi vilevile zilithibitishwa na BBC kuhusu eneo la kaskazini mwa jengo hilo la ghorofa tisa lililopo kando ya barabara kuu ya Yeysk lililoshambuliwa.
Katika video hiyo, alama sawa na majengo yanaweza kuonekana. Tulipitia marejeleo haya na picha za mwonekano wa mtaani wa Google ili kuthibitisha ajali hiyo ilitokea nje kidogo ya barabara ya Ulitsa Kommunisticheskaya kusini mwa Yeysk.
Hali ya hewa pia ililingana katika kila video, kukiwa na anga angavu na jua kutua, kwa hivyo tunaweza kuwa na uhakika kwamba ajali hiyo ilitokea takriban 17:30 saa za nchini humo.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ndege hiyo aina ya Su-34 ilianguka baada ya kupaa kwa safari ya mafunzo kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi karibu na Yeysk.
Katika video ya moto baada ya shambulio, sauti za mlio na baadhi ya milipuko inaweza kusikika. Hizi zinaweza kusababishwa na risasi zilizokuwa zimebebwa na ndege wakati wa mazoezi ya kufyatua risasi.
Maafisa wa Urusi wanasema moto huo ulisababishwa na kumwagika kwa mafuta na kusisitiza kuwa hakukuwa na milipuko ya risasi.
Su-34 ni ndege ya kivita inayoendeshwa na marubani wawili ambayo mara nyingi hutumwa kulenga shabaha za ardhini.
"Su-34 ni mojawapo ya ndege za kisasa zaidi za Urusi lakini bado ina matatizo ambayo yamejitokeza, hasa katika mafunzo," anasema J Andrés Gannon, mtaalam wa usalama katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani (CFR).
Kumekuwa na visa vingine viwili vya ajali ya ndege aina ya Su-34 mwaka huu ambavyo havikuhusiana na mashambulizi ya adui, kulingana na Air Forces Monthly, Jarida la Uingereza linalofuatilia data ya ndege za kijeshi.
Je ilifanyikaje?
Picha za CCTV kutoka barabara kuu karibu na jumba hilo baadaye zilichapishwa katika mtandao wa telegram na Twitter.
Zinaonesha ndege ikishuka , halafu mwangaza mkubwa unoanekana kuwa mlipuko ndani ya ndege hiyo. Mlipuko huo unafuatiliwa kwa kasi na mwanagaza wa pili , ambao wataalam wanasema huenda ikawa ni marubani waliojaribu kutoka , kabla ya ndege hiyo kugonga jumbe hilo.
Ndege hiyo inaonekana kuruka kutoka magharibi, pengine kutoka uwanja wa ndege wa Yeysk nje kidogo ya mji ambao una uwanja wa ndege wa kijeshi.
Picha ya satelaiti iliyopigwa mapema mwezi huu inaonyesha ndege kumi kwenye uwanja wa ndege ambazo zinalingana na vipimo na rangi ya ndege ya Su-34.
Picha hii ya mtandao hapa chini ilionekana kwenye Telegram ikimuonesha rubani akiwa na parachuti upande wa kulia, ambaye anaonekana kujitoa kwenye ndege kabla ya kuanguka.
Parachuti hii ina michoro ya rangi za chungwa kuizunguka, zinazotambulika kama alama kwenye seti ya kijeshi ya Urusi, na inayolingana na mfano wa rubani wa Urusi aliyeonekana akitoka ndani ya ndege nchini Syria mnamo 2018.
Tunafanya uchunguzi zaidi ili kuthibitisha uhalisi wa picha hiyo.
Video iliyotumwa kwenye Telegram karibu na eneo la ajali inaonyesha rubani akiwa amelala chini na parachuti upande wa magharibi wa jengo lililoharibika.
Rubani yuko hai, amelala chali, na kujibu maswali.
Mtu anauliza kwa lugha ya Kirusi "Je, kila kitu kiko salama ?" ambayo anajibu "Ndiyo, ndiyo." Alipoulizwa iwapo ndege yake ilidunguliwa, rubani alisema "Hapana."
Hatujui ni nini kilifanyika kwa rubani wa pili, lakini Urusi inasema marubani wote wawili walitolewa kabla ya athari na wanahojiwa.
Wataalam wanasemaje?
Tulionyesha ushahidi wa video kutoka kwa mitandao ya kijamii kwa wataalam kadhaa wa usalama na ndege ili kupata tathmini yao ya kile ambacho kinaweza kutokea.
Andres Gannon, kutoka CFR alisema ushahidi unaoonekana unaonyesha hitilafu ya injini ndiyo sababu kuu ya ajali hiyo. Hii inaweza kuwa imesababisha usambazaji wa mafuta kuwaka, kulingana na miale miwili ya mwanga inayoonekana wazi kwenye video.
"La kwanza linawezekana wakati wa ueneaji wa mafuta ulipowashwa na hitilafu ya injini, na kisha mwangaza wa pili inaeleweka .
"Hatuoni kitu kinachoonekana kama shambulio la kombora. Hatuoni joto au mwanga wowote kutoka kwa chanzo chochote kinachokuja."
"Ni vigumu kuamini kuwa ni shambulizi la kombora," anasema Mark Cancian, mshauri wa masuala ya ulinzi katika Mpango wa Kimataifa wa Usalama.
Anasema Urusi ina kiwango cha "juu sana" cha ajali katika jeshi lake, kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa wa hitilafu ya ndege.
Mara ya kwanza alipoona picha za video, rubani na mwanahistoria wa usafiri wa anga Paul Beaver alisema miale iliyoonekana kabla ya ajali hiyo ililingana na kushambuliwa kwa ndege, badala ya kupata hitilafu.
Hata hivyo, akiichunguza kwa makini sasa anaona kuwa miangaza hiyo miwili ni matokeo ya marubani waliotoka nje ya ndege kabla tu ya kugonga jengo hilo.
"Sasa ninaamini kuwa ilikuwa ni kuvunjika kwa turbine [ya injini] na mwangaza uliotokea si mashambulizi ya kombora kutoka ardhini hadi angani, lakini sauti za myavuli iliotumiwa na marubani kutoka na kuruka."
Ripoti ya ziada ya Chris Partridge, Olga Smirnova, Soraya Auer, Tural Ahmedzade, Paul Myers, Daniele Palumbo, Erwan Rivault, Famil Ismailov na Vitaliy Shevchenko.
Ufafanuzi: Paul Beaver amebadilisha tathmini yake ya awali ya sababu ya ajali hiyo baada ya kutazama video zaidi. Kifungu hiki kimerekebishwa ipasavyo.