Teksi zinazopaa zinajiandaa kuruka

Teksi inayoruka ya kampuni ya Hyundai itakuwa sokoni baada ya miaka mitatu. Kampuni hiyo inasema teksi hiyo litaleta mapinduzi makubwa katika usafiri wa mijini.

Hyundai iliiweka wazi teksi inayoruka katika Maonyesho ya Kielektroniki ya Las Vegas. Kampuni hiyo ya kutengeneza magari ya Korea inasema gari hilo liitwalo S-A2, litakuwa tayari kwa matumizi ya umma 2028.

Pia Unaweza Kusoma

Kampuni ya Hyundai

S-A2 imeundwa na kampuni tanzu ya Hyundai inayoitwa Supernal. Msimamizi wa mradi huo ni Jaeon Shin ana uzoefu wa kufanya kazi na NASA.

S-A2 ina propela nane zinazotumia betri na inaweza kuruka hadi mita 457 kutoka ardhini. Kasi yake ya juu ni kilomita 190 kwa saa, inaweza kuruka kati ya kilomita 40 na 64.

Hyundai imeunda teksi hii ya kuruka kwa matumizi katika miji na kuruka kwenye njiaa za mkato. Inasema propela zake hazina kelele.

Supernal imetangaza kuwa majaribio ya safari za S-A2 yataanza 2025, na safari za kibiashara zitaanza 2028 baada ya kupata cheti cha usalama.

Hyundai sio kampuni pekee ya kutengeneza magari yanayoruka. Toyota, Mercedes-Benz, Volkswagen na baadhi ya watengenezaji magari wa China pia wanapanga kuingia katika soko hili.

Watengenezaji magari wanatabiri mahitaji ya magari ya kibinafsi yatapungua katika miaka ijayo, na wanatahitaji njia zingine za kuongeza mapato.

Teksi hizi ni suluhisho la msongamano wa magari katika miji mikubwa na mahitaji yao yanatarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo.

Taasisi ya utafiti ya Marekani, Mordor imetabiri thamani ya soko la teksi za angani za mijini mwaka 2036 itakuwa zaidi ya dola bilioni 45.

Kampuni ya Xpeng

Katika Maonyesho ya Kielektroniki ya Las Vegas, kampuni ya magari ya China, Xpeng ilitangaza kuunda SUV ya magurudumu sita ambayo pia inaruka. Xpeng inasema wanunuzi nchini China wataweza kuagiza gari hilo baadaye mwaka huu kwa bei ya dola za kimarekani 170,000.

Gari hili limetengenezwa na kampuni tanzu ya Xpeng iitwayo AeroHT, iliyoanzishwa 2013 ili kutengeneza magari yanayoruka.

Mkurugenzi wa kampuni hii anasema muundo wa SUV bado haujakamilika, lakini safari za majaribio zimefanywa na kampuni inajiandaa kwa uzalishaji wake wa mwisho.

Wazo lililowasilishwa na Xpeng ni gari ya abiria watano na inaweza kutembea katika barabara mbovu. Ni gari ya umeme na inaweza kusafiri hadi kilomita 1000 kwa kila chaji.

Gari hili linaweza kuendeshwa na watu wawili huku Xpeng ikisema linafaa kwa wapenda mazingira na timu za uokoaji. Xpeng inatarajia kuuza gari 10,000 kwa mwaka nchini China na inasema litauzwa katika masoko mengine ikiwa itapata leseni.

Kampuni ya Kia

Kia alizindua gari jipya kwenye Maonyesho ya Kielektroniki ya Las Vegas. Gari hiyo inayoitwa PV5, ni ya kwanza katika mfululizo wa bidhaa mpya za magari na programu ambazo Kia inasema zitaleta mapinduzi katika mtandao wa uchukuzi.

PV5 van ni ya umeme na imeundwa kwa njia ambayo wanunuzi wanaweza kuirekebisha kulingana na mahitaji yao.

Sehemu ya nyuma ya gari hili inaweza kubadilishwa kutoka gari la abiria hadi gari la kubeba mizigo. Katika gari la abiria, viti vinaweza kuwekwa pamoja au kusogezwa nyuma

Sehemu ya migizo ya gari hilo pia linaweza kuwekwa kwa namna tofauti, kwa mfano, kuigeuza kuwa duka la simu.

Usukani wa gari unaweza kuhamishwa wakati wa maegesho ili kuongeza nafasi kwa dereva. Kuna kabati ambapo dereva anaweza kuweka vitu vyake.

Kia inasema inatengeneza programu ambazo zinaweza kutoa huduma kama vile kusafirisha vifurushi vya posta. Pia inafanya kazi na Uber kuandaa magari haya kama teksi.

Magari mapya ya Kia yatazalishwa katika kiwanda nchini Korea Kusini na yatazinduliwa mwaka 2025. Kia inasema itazalisha magari 150,000 kila mwaka. Bei ya gari inatarajiwa kuwa karibu dola 40,000.

Imeundwa kuweza kubadilisha mwelekeo kwa digrii 90. Hivyo, dereva anaweza kuegesha gari kwa urahisi au kuzunguka katika nafasi ndogo.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah