Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Lazima tujipange upya' - je Liverpool kuwa na 'msimu mbaya zaidi usiosahaulika'?
Msimu uliopita Liverpool walikaribia kabisa kutwaa makombe manne makubwa. Miezi minne baada ya kushindwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa, Jurgen Klopp sasa anauliza kama timu yake inahitaji "kujipanga upya".
Kipigo cha usiku wa kuamkia leo cha mabao 4-1 kutoka kwa Napoli kilimaanisha kuwa Liverpool sasa wameshinda mechi mbili pekee katika mechi saba za kwanza za mashindano yote msimu huu.
Beki wa zamani wa England Jonathan Woodgate aliambia BBC Radio 5 Live jinsi Napoli 'walivyoiangamiza' Liverpool na Reds kuishiwa nguvu na maarifa.
Beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand kupitia BT Sport alielezea kuchapwa huko kwa Liverpool kuwa ni "aibu" wakati mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Michael Owen alisema inaweza "kuwa na msimu mbaya".
Klopp amesimamia mafanikio ndani ya Liverpool tangu alipowasili mwaka 2015, lakini je, baada ya kuanza msimu huu kwa wasiwasi, je, ni wakati wa kufanya mabadiliko?
'Nahitaji muda kutafakari hilo'
Liverpool walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 mpaka wakati wa mapumziko huku wakilala kwa moja ya vipigo vibaya zaidi ilivyowahi kupata katika Ligi ya Mabingwa.
"Tunacheza na Wolves Jumamosi na huenda wasicheke na sisi. Wanaweza kusema na hata nami ningesema hivyo hivyo kwamba - ni wakati muafaka wa kucheza nao [Liverpool]. Hatuchezi vizuri vya kutosha, hilo liko wazi na ndiyo maana tunapoteza michezo. Kuna kazi ya kufanya, jukumu langu na ninahitaji muda wa kulitafakari."
Beki wa kushoto wa Liverpool Andy Robertson alisema wachezaji walihitaji "kurejea kwenye misingi" kufuatia uzembe katika safu ya ulinzi. "Tulistahili matokeo haya. Lazima uwe tayari kupigana. Tunapaswa kuzinduka haraka ."
Liverpool 'imekosa ari ya kupigana'
Makosa ya mtu binafsi yaliigharimu pakubwa timu hiyo huko Naples hasa Joe Gomez na Trent Alexander-Arnold walipata shida dhidi ya timu hiyo ya Italia.
Piotr Zielinski aliifungia Napoli bao la kuongoza dakika ya tano kabla ya Andre-Frank Anguissa na Giovanni Simeone kufanya matokeo kuwa 3-0 hadi mapumziko.
Zielinski alifunga tena dakika mbili za kipindi cha pili na hadi Luis Diaz anafunga bao la kufutia machozi mambo yalikuwa yameshaharibika tayari.
Ferdinand alisema "unaweza kuona hasira na Klopp" na kuhoji ari ya wachezaji wa Liverpool, wakati mlinzi wa zamani wa Reds Jamie Carragher alielezea kama "safu ya ulinzi iliyotoboka".
"Maoni ya 'lazima tujipange upya' - ni kauli kubwa," aliongeza Ferdinand. "Si mara nyingi ambapo unaweza kusema Liverpool ilikosa ari na nguvu ya kupigana lakini [hapa] walikosa vitu hivyo vyote. Nyota wao wengi sana hawako karibu na viwango vyao tulivyovizoea."
'Wamiliki wanatarajia nibadilishe hali ya mambo'
Lakini je, Klopp "atashindwa kupata suluhisho? Kocha huyo wa Ujerumani, ambaye ameshinda kila taji la nyumbani akiwa na Liverpool, na vile vile Ligi ya Mabingwa wakati akiwa katika klabu hiyo, alisema anahitaji "wakati wa kulifikiria".
"Hatukuwa na uwezo wa kujilinda na kushambulia," aliongeza Klopp. "Kila kitu kiko wazi lakini kwa nini kilitokea, siwezi kujibu sasa.
Siku ambayo Chelsea ilimtimua meneja Thomas Tuchel, Klopp hata alipoulizwa katika mkutano wa wanahabari kama anahofu ya nafasi yake mwenyewe. "Si kweli, wamiliki wetu ni watulivu na wanatarajia nirekebishe mambo na sidhani kama kuna mtu mwingine atafanya," alijibu.
Baada ya juhudi za msimu uliopita, ambazo ziliifanya Liverpool kuwa nyuma ya alama moja tu dhidi ya Manchester City katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England, kuingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutwaa vikombe viwili vya nyumbani, msimu huu mambo yamekuwa tofauti sana.
Na bahati mbaya hawana muda mrefu wa kujipanga upya kwani mechi yao inayofuata ni dhidi ya Wolves kwenye Ligi kuu England itapigwa Jumamosi huko Anfield.