Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kutekwa nyara na kusafirishwa mara mbili - maisha ya mfanyabiashara wa ngono nchini Sierra Leone
Isata, mama asiye na mwenzi mwenye umri wa miaka ishirini, ni kielelezo cha kutisha cha maisha ya wafanyabiashara wa ngono nchini Sierra Leone.
Amepigwa, ameibiwa, ametekwa nyara, amesafirishwa hadi nchi nyingine, ameokolewa, ameuzwa na kuokolewa tena.
Mbali na hayo yote, alikuwa na uraibu wa dawa hatari ya kulevya ya mitaani, kush, ambayo imesababisha madhara makubwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
BBC Africa Eye ilitumia miaka minne kufuatia maisha ya kundi la wafanyabiashara wa ngono huko Makeni, takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Freetown.
Mji huo upo katika eneo lenye utajiri wa almasi, uliochochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone - mzozo ambao umekuwa na athari mbaya ambazo zinaendelea kushuhudiwa hadi leo.
Isata ni mmoja wa mamia ya wafanyabiashara wa ngono huko Makeni. Sawa na wanawake wote tuliozungumza nao, amechagua kutumia jina lake la kwanza pekee.
"Yote ninayoyafanya najitolea kwa ajili ya binti yangu. Nimepitia maumivu mengi sana mitaani,” alisema.
"Nilikutana na mwanamume katika klabu. Alirarua nguo zangu. Alichukua pesa kutoka kwenye sidiria yangu. Nilikuwa nikijaribu kumtoroka. Alinipiga kisogoni na bunduki yake. Alitaka kuniua.”
Ni maisha hatari - baadhi ya wanawake tunaokutana nao pia wameambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU). Wengine wameuawa.
Lakini wengi wanahisi hawana la kufanya.
Katika eneo lenye giza lenye matope la jiji, wafanyabiashara wawili wa ngono walionyesha eneo lenye magunia tupu ya nafaka yaliyotapakaa ardhini.
Mmoja wa wanawake hao vijana, Mabinty, alituambia hapa ndipo walipofanya kazi bega kwa bega – wakikutana na wanaume 10 kwa usiku mmoja.
Wanaume huwalipa dola moja kwa tendo moja la ngono.
Anajaribu kupata pesa za kutosha kuwasaidia watoto wake. Alikuwa na sita, lakini watatu walikufa.
Wengine watatu wako shuleni.
“Mtoto mmoja amemaliza mitihani yake. Sina pesa za kumlipia aende shule, isipokuwa kujiuza kingono. Haya ni mateso yangu,” alisema.
Maelfu ya wanawake wanakadiriwa kufanya biashara ya ngono kote Sierra Leone.
Wengi wao ni wanawake vijana walioachwa mayatima kutokana na vita hivyo, ambavyo viligharimu maisha ya zaidi ya watu 50,000 na kuwakosesha makazi karibu nusu ya wakazi wa nchi hiyo hadi vilipomalizika mwaka 2002.
Mashirika ya kutoa misaada yanasema idadi ya wasichana wadogo wanaofanya biashara ya ngono imeongezeka zaidi huku nchi hiyo ikikabiliana na kuporomoka kwa uchumi wake kulikosababishwa na mlipuko wa Ebola na janga la corona.
Kama majanga mengi, haya yamewaathiri wanawake kwa njia isiyo sawa.
Ukahaba sio haramu nchini, lakini wanawake wanaonekana kama watu waliotengwa na wanapokea msaada mdogo kutoka kwa serikali au jamii.
Muda mfupi baada ya kukutana na Isata mnamo 2020, alitekwa nyara na genge la wahalifu na kulazimishwa kuwa mtumwa wa ngono huko Gambia, Senegal na hatimaye Mali.
Alifanikiwa kushika simu na kuelezea maisha yake huko.
"Jinsi wanavyotukaribia, ni kama wanataka kutuua hatuna namna isipokuwa kukubali," alisema.
"Ninateseka sana."
BBC Africa Eye wakati huo iliweza kumtafuta na shirika la Umoja wa Mataifa, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), lilimsaidia Isata kurejea Sierra Leone.
Aliachana na kazi ya ngono lakini, tulipomuona mwaka 2021, alikuwa akihangaika kupata pesa za kutosha kumtunza binti yake, kwa kupika chakula katika eneo hilo.
Wakati mwingine tulipopata taarifa mpya kumhusu Isata, mwaka wa 2023, alikuwa amerejea kwenye ukahaba baada ya kujihusisha na kush - mchanganyiko wa dawa za kulevya zinazouzwa kwa bei nafuu, ambazo zinaweza kuwa na mifupa ya binadamu .
Dawa hiyo imekuwa tatizo nchini Sierra Leone, rais ameitangaza kuwa ni dharura ya kitaifa.
Katika mtego wa uraibu, Isata alimuacha mtoto wake mdogo - mtoto wa miezi minne tu. Alikuwa akitunzwa na mama Isata, Poseh.
“Mfadhaiko wa maisha ya mtaani ulimfanya avute kush. Ni msongo wa mawazo,” Poseh alisema.
Nata pia ni mama asiye na mume mwenye umri wa miaka ishirini.
Ana binti watatu.
Tulikutana naye nyumbani, ambapo alikuwa akijiandaa kutoka kwenda kufanya kazi.
“Nataka watoto wangu wafanye vyema maishani. Natumai maombi yangu yatajibiwa na Mungu,” alisema.
Binti yake alimtazama mama yake akipaka vipodozi. Alituambia alitaka kuwa wakili akiwa mkubwa.
"Ili kumsaidia mama yangu," alisema.
Katika jiji , tulikutana na msichana mwingine mchanga, Rugiatu, mwenye umri wa karibu miaka 10.
Mama yake Gina pia alikuwa mfanyabiashara wa ngono. Aliuawa mnamo 2020 akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Sasa Rugiatu anaishi na bibi yake.
"Mama na baba yangu wamekufa sasa. Nimebaki na bibi yangu tu. Bibi yangu akifa, ninachoweza kufanya ni kwenda kuomba mitaani,” Rugiatu alisema.
"Sitaki waniue pia mitaani."
Tulipomwona Nata tena, hakutambulika. Yeye, pia, anatumia dawa ya kulevya ya kush.
"Sifurahii kuwa hivi, lakini sitaki kufikiria sana," anatuambia.
“Wakati fulani mimi hulia ninapokumbuka. Ndiyo maana ninavuta sigara, kusahau.”
Binti zake watatu wamelazimika kwenda kuishi na jamaa.
Mapema 2024, kulikuwa na habari mbaya zaidi kutoka kwa Isata.
Alikuwa amesafirishwa tena, kama sehemu ya kundi la wanawake ambao waliahidiwa kazi ya yaya nchini Ghana lakini badala yake walipelekwa Mali na kulazimishwa kushiriki biashara ya ngono katika eneo la machimbo ya dhahabu.
“Nataka nipelekwe nyumbani. Ninaomba, najutia kila kitu,” Isata anatuambia kupitia simu.
Alisema aliingiwa na wasiwasi wakati mwanamume aliyeamuahidi kazi ya uuguzi alipokwepa vizuizi vya polisi na vituo vya mpaka katika kila hatua ya safari.
"Alitukabidhi kwa mwanamke Mnigeria anayeitwa Joy," alisema.
"Tuliuliza: 'Ulituambia tunaenda Ghana kwa kazi ya yaya, hii ni Ghana?'"
"Joy alituuliza: 'Je, hamkuambiwa mnakuja kufanya kazi ya ngono?' Kisha nikasema: ‘Hapana’.”
“Akasema: ‘Nenda ukachukue pesa’ na umpe.”
Sawa na wanawake wengi waliosafirishwa, Isata aliambiwa lazima afanye kazi kwa bidii apate kiasi kikubwa cha fedha ili aweze kuwalipa wafanyabiashara haramu ya usafirishaji wa binadamu waliomleta ili aweze kununua wake.
Walimwambia alipe $1,700 (£1,300).
Angelazimika kufanya mapenzi na mamia ya wanaume ili kupata pesa nyingi hivyo.
Waliomuuza walimwambia ana miezi mitatu ya kuwalipa.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia watu wanaosafirishwa kwa njia haramuIOM - linasema maelfu ya raia wa Sierra Leone, wakiwemo watoto, wanasafirishwa kila mwaka.
Wanatekwa nyara au kulaghaiwa kusafiri nje ya nchi kwa ahadi ya kazi bora.
Badala yake, huuzwa kwa wageni katika nchi zinazozunguka bara na kuishia katika kazi ya kulazimishwa au utumwa wa kingono. Huenda wengi wasiwahi kurejea kwao tena.
Kwa bahati nzuri kwa Isata, hatimaye amefanikiwa kurudi Makeni, na anaishi na mama yake na watoto wawili.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla