Wanafunzi wanaojihusisha katika biashara ya ngono kugharamia maisha yao katika vyuo vikuu

Wakati alipoishiwa na fedha na kuishia kuiba maziwa katika vyumba vya wanafunzi wenzake, aliamua kuna njia moja pekee ya kujipatia pesa.

Jamaa ambaye hakutaka kutajwa jina anasema alikutana na wanaume wakati akiwa mwanafunzi katika chuo kikuu na alilipwa kati ya £20 na £120.

"Ni kazi ambayo daima niliiona kama njia rahisi ya kujipatia pesa wakati nikikabiliwa na wakati mgumu. Nilifanya hivyo wakati nikiwa na uhitaji mkubwa," amesema.

Hatimaye wazazi wake, waligundua na kulisitisha. Hakuzungumza na mtu mwingine yeyote akiwemo aliyekuwa mpenzi wake kuhusu kilichotokea.

Sasa ana kazi, lakini anasema hayuko katika nafasi ya kuwausia au kuwashauri wanafunzi wengine ambao pia wanapata tabu kujikimu.

"Nalijutia nikitazama nyuma. Lakini ningewekwa tena katika hali hiyo, huenda ningeli liregea tena," anasema.

Pesa za dharura

Utafiti uliofanywa umeashiria kuwa wanafunzi 25 wamewahi kushiriki katika biashara hiyo, ikiwemo kutoka na wanaume wazee au sugar daddy kama wanavyofahamika kwa umaarufu na wengine hata kushiriki ngono ili kujipatia pesa.

Utafiti huo wa National Student Money, uliofanywa na mtandao wa Save the Student, unakusanya maoni ya zaidi ya wanafunzi 3000.

Idadi ya walioulizwa - ambao walishiriki biashara hiyo ya ngono - ni mara mbili ya idadi iliokuwepo mwaka uliotangulia.

6% ya wanafunzi wanasema wanaweza kushiriki biashara hiyo iwapo wangehitaji fedha za dharura.

Karibu wanafunzi wanne kati ya watano wana wasiwasi kuhusu kujikimu, kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa Agosti.

Kwanini biashara hiyo na sio nyingine?

Hili ni tatizo linalodhihirika miongoni mwa wanafunzi pia katika baadhi ya vyuo Afrika.

Sababu kubwa inayotajwa ni kutaka kuishi maisha kupita kiwango au uwezo wa mtu.

Nicy Aluoch, mwanafunzi aliyehitimu hivi karibuni na sasa ni msanii nchini Kenya anaeleza kuwa baadhi ya wanafunzi hutafuta njia za kupata pesa ili kuweza kumudu vitu kama 'mavazi ya kisasa, pesa za kwenda kujivinjari na pia kupata umaarufu na kujionesha miongoni mwa vijana wenzao'.

Shinikizo ambalo analitaja kuwepo miongoni mwa vijana katika kutaka kuwa na 'maisha ya kwenye mitandao ya kijamii'.

"Tunataka kuwa na ushawishi katika makundi yanayotuzunguka. Sisi ni rafiki wa rafiki zetu na kwahivyo tunataka tuwe bora au juu kuliko wote".

Nicy anaeleza kwamba kuna mitindo mipya kila siku duniani. Na vijana wengi wanataka wawe mbele ya vijana wenzao ili kujithibitisha kwamba wanaweza kuwa bora.

Hata hivyo anashauri kwamba njia ni nyingi kama kwa mfano vijana kujihusisha katika ujasiriamali ili kuweza kujikimu na pia kuridhisha wazazi kwamba "our child is not a liability".

"Unapokuwa shuleni unaambiwa maisha ni magumu nje. Binafsi nilitaka kuingia utu uzimani bila ya tashwishi. Kwahivyo nilijiwekea kuwa nitafanya kazi kwa bidii, nilishiriki katika mashindano nikiwa chuoni, na mengineyo ili niweze kuwa mtu ninayetaka kuwa".

Faith Muthoni mwanafunzi mwingine aliyehitimu hivi karibuni anasema tatizo la biashara ya ngono linadhihirika na kumeshuhudiwa visa vya wasichana katika vyuo vikuu wanaojihusisha katika biashara ya ngono na wazee ili kujipatia pesa.

Anasema binafsi kilichompatia msukumo ni matamanio ya kuwa na maisha bora.

Katika muda wake akiwa katika chuo kikuu, Faith anasema amefanikiwa kukabiliwa na changamoto hiyo ya kujikimu kifedha kwa kujihusisha na biashara ndogo ndogo.

Anaeleza kwamba aliwahi kuuza soksi, manukato na hata kujitafutia kibarua kinachoendana na alichokuwa akisomea, kupiga chapa au kuandika makala katika mitandao.

Utafiti huo wa kitaifa uliofanywa nchini Uingereza umegundua kwamba 57% ya walioulizwa wamesema wameugua matatizo ya afya ya akili kwasababu ya kuwa na wasiwasi wa pesa - kiwango kilichoongezeka kwa asilimia kumi na moja kutoka mwaka uliotangulia.

Mtaalamu wa masuala ya afya ya akili Hannah Morish anasema kazi zinazohusu masuala ya ngono zinaweza kuchangia mtu kuwa na wasiwasi na pia msongo wa mawazo.

"Kazi hizi zinaweza kumfanya mtu mpweke kwasababu ya unyanyapaa unaondamana nao, kumaanisha iwapo mwanafunzi anapitia kipindi kibaya itakuwa vigumu kwao kulizungumzia, na kuchangia kuzidi upweke," amesema.

"Vyuo vikuu na muungano wa wanafunzi wanahitaji kukagua iwapo wana ushauri na nafasi salama katika vyuo hivyo au katika mitandao yao kuwasaidia wanafunzi wanaofikiria au ambao tayari wanajihusisha na kazi za aina hii."