Kocha mpya Brazil: Je, Ancelotti atarudisha utukufu wa Brazil Kombe la Dunia?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sam Harris
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Carlo Ancelotti amekubali kuchukua nafasi ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil. Uamuzi wa Brazil wa kumleta kocha wa kigeni, ni kielelezo cha matamanio ya kusaka ushindi katika kombe la dunia la 2026.
"Ancelotti ni chaguo la Brazil kwa sababu ya mafanikio yake, ameshinda katika nchi tano," anasema mchambuzi wa soka wa Amerika Kusini, Tim Vickery.
Uwezo wa Brazil kutawala soka la kimataifa umeporomoka katika miongo miwili iliyopita. Licha ya kushinda mataji mawili ya Copa America ndani ya kipindi hicho - 2007 na 2019. Lakini rekodi yao kwenye Kombe la Dunia imekuwa ya kukatisha tamaa.
Hawajashinda kombe la dunia tangu walipotwaa kwa mara ya tano mwaka 2002. Ajabu ilikuja mwaka 2014, pale Brazil, walipokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia, lakini walidhalilishwa kwa kufungwa magoli 7-1 na Ujerumani katika nusu fainali.
"Kila kombe la dunia tangu 2002 wameondolewa na timu ya Ulaya katika hatua ya mtoano," anasema Vickery.
"Wanataka ushindi na ndio sababu wamechukua kocha kutoka Ulaya wakati huu. Wanasema 'kama tunataka kuzifunga timu za Ulaya, tunahitaji mtu anayezijua'."
Brazil ya sasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mechi za sasa za Brazil za kufuzu Kombe la Dunia zina walakini. Wanaelekea kufuzu lakini kwa tabu, tayari wamefungwa mabao 4-1 na Argentina, na hilo limewafanya kusaka majibu.
Makocha wamekuja na kuondoka katika miaka ya hivi karibuni huku kukiwa na kelele za kutaka timu inayoshinda.
Kocha Tite, anayeheshimika kwa kuleta hali ya utulivu, alijiuzulu baada ya kombe la dunia la Qatar 2022. Kocha wa hivi karibuni wa timu hiyo, ni Dorival Junior, alitimuliwa kufuatia kufungwa na Argentina.
Hilo limesababisha Shirikisho la Soka la Brazil kuuda mpango uitwao Project Ancelotti. Utaanza rasmi tarehe 26 Mei, wakati Muitaliano huyo mwenye umri wa miaka 65 akimaliza kibarua chake huko Madrid, na Xabi Alonso anatarajiwa kuwa mrithi wake.
Kocha wa kigeni

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika kipindi cha zaidi ya karne, shirikisho la soka la Brazil limeepuka kwa kiasi kikubwa kuwaamini makocha wa kigeni. Ni makocha watatu tu ambao sio Wabrazil wamewahi kuiongoza timu hiyo, na walifundisha mechi saba pekee kwa jumla.
Raia wa Uruguay Ramon Platero alikuwa wa kwanza mwaka 1925 na kusimamia michezo minne, Joreca kutoka Ureno alisimamia michezo miwili mwaka 1944, na Muargentina Filpo Nunez alisimamia mchezo mmoja mwaka 1965.
Na ligi ya ndani ya Brazil ya Serie A hali iko kama hivyo. Fikra za muda mrefu ni kwamba; Mbrazil ndiye anayeweza kuelewa maana ya kucheza soka la Brazil.
Lakini utamaduni huu ulibadilika mara baada ya kocha wa Ureno, Jorge Jesus, kuchukua nafasi ya ukocha 2019 katika klabu ya Flamengo. Kuwasili kwake kulitoa matumaini kwamba mfumo mzuri wa Ulaya unaweza kuleta mafanikio.
Jesus aliongoza Flamengo kutwaa taji la ligi na vilevile Copa Libertadores, huku klabu hiyo ya Rio de Janeiro ikiwa na moja ya misimu yenye mafanikio zaidi kuwahi kutokea. Timu yake ilishinda michezo 43 kati ya 57 kabla ya Jesus kuondoka Julai 2020.
Tangu wakati huo kumekuwa na mabadiliko ya ndani na kukubalika makocha wa kigeni nchini Brazil.
Ancelotti atakwenda Brazil akiwa na mataji matano ya Ligi ya Mabingwa na mataji ya ndani nchini Italia, Uingereza, Ufaransa, Uhispania na Ujerumani.
Ancelotti atapeleka nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa msimu wa 2024-25 akiwa Real Madrid umekuwa mgumu, huku timu yake ikipoteza mbele ya Barcelona kwenye fainali ya Copa del Rey na kutolewa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Arsenal, mafanikio yake ya zamani yanahesabiwa.
Timu aliyochezesha ya AC Milan mwanzoni mwa miaka ya 2000 ilijumuisha nyota wa Brazil kama Paolo Maldini, Andrea Pirlo na Kaka. Na akiwa Madrid ameruhusu vipaji vya Wabrazil kama Vinicius Jr na Rodrygo kukuwa.
"Vinicius Jr anapenda kufanya kazi na Ancelotti. Atafurahishwa na uteuzi huu," anasema Vickery.
"Sio yeye tu. Pia kiungo wa kati wa Manchester United, Casemiro anaweza kurejea kuimarisha safu yao ya kiungo - ambayo imekuwa moja ya nafasi yenye wasiwasi."
Washambuliaji Vinicius na Rodrygo wamekuwa muhimu kwa mafanikio ya hivi karibuni ya Madrid na Ancelotti.
Vinicius, licha ya kung'ara katika uchezaji wake nchini Uhispania, uchezaji wake kwa Brazil mara nyingi umekuwa mbaya, ana rekodi ya mabao sita tu katika mechi 39.
Wachambuzi wanasema, anapata tabu kwa sababu ya mipangilio tofauti ya mbinu, lakini Ancelotti anajua jinsi ya kupata kilicho bora kutoka kwa Vinicius – kumpa jukumu lake, kumuongezea kujiamini na kumpa uhuru ndani ya mfumo wake wa uchezeshaji.
Kumteua Ancelotti ni hatua kubwa kwa Brazil, kwani sasa wako tayari kubadilika ili kuirejesha nafasi yao kwenye kilele cha soka.
Iwapo Ancelotti ataweza kuleta utulivu katika timu, huku akiwatumia wachezaji kama Vinicius, na pengine akimtumia Neymar vizuri, anaweza kuwa mtu bora wa kuiongoza Brazil kurejea kwenye utukufu wake.
Ikiwa ataweza kufanya hivyo, hatokuwa tu ameipatia ufumbuzi Brazil, pia atakuwa ametoa ufafanuzi mpya juu ya maana ya soka la Brazil katika zama za sasa.















