Mzozo wa DRC: 'Waume zetu wanawindwa, tutaishi vipi wakipotelea vitani?'

    • Author, Alfred Lasteck & Ashley Lime
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Author, Ashley Lime
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Wanamgambo wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wanakaribia mji wa Uvira, mji katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyanzo vimeieleza BBC.

Kwa kuidhibiti miji ya Bukavu, Kamanyola na Luvungi, inasemekana wanamgambo wa M23 wanahama kuelekea mji wa pili mkubwa katika Mkoa wa Kivu Kusini, wenye wakazi zaidi ya 700,000.

Wakazi waliouzungumza na BBC walisema wasiwasi unazidi kuongezeka kutokana na ripoti za mapigano kati ya jeshi la Congo na vikundi vya wanamgambo vinavyounga mkono serikali.

Rehema (si jina halisi), mama wa watoto watatu na mkazi wa Uvira, aliiambia BBC kwamba hali ni ngumu katika mji huo kufuatia ripoti za vifo huko Goma na Bukavu.

"Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa mgogoro huu. Hatuwezi kupigana, lakini pia hatujui tufanye nini wakati huu M23 inasemekana inakuja Uvira," alisema.

Alisema maisha yatakuwa magumu ikiwa waume zao, ambao wanawindwa na waasi, watakufa katika mapigano.

Unaweza kusoma

Rehema alisema familia yake haijalala kwa siku mbili na kwamba jeshi la Congo haliwezi kuwakinga kwa sababu ya vurugu na uporaji mkubwa.

Chanzo kilichotaka kutotajwa jina kilielezea BBC kuwa alishuhudia uporaji, unyang'anyi na hata mauaji ya raia yanayotekelezwa na wanajeshi walipozunguka mji wenye ziwa ambalo ni mpaka na Burundi.

"Hivyo, sote tuko ndani tukisubiri M23 waje. Hii ni kama ilivyotokea Bukavu. Nimeamua kubaki kwa sasa kwa sababu nilijua kwamba maisha ni magumu sana kwa wale waliovuka kwenda kwenda kwenye kambi za wakimbizi huko Bujumbura. Hakuna chakula," alisema.

BBC inabaini kwamba raia wa Congo wanaokimbia kwenda Bujumbura, mji mkuu mkubwa wa Burundi, wanatakiwa kuishi kwa familia za waathirika.

Wakazi walisema kuwa mji huo umeshuhudia mapigano katika siku mbili zilizopita kati ya jeshi la Congo (FARDC) na wanamgambo wake walioungana na Wazalendo, huku wakisema kwamba wanamgambo wanajaribu kuzuia wanajeshi kuondoka mjini humo.

Vita ndefu zaidi?

Wapiganaji Wazalendo wanaripotiwa kutaka kuchukua silaha kutoka kwa jeshi la DR Congo, wakilaumu wanajeshi wa serikali kwa kukimbia mstari wa mbele na kujiondoa kusini zaidi hadi Kalemie.

"Wazalendo walijitokeza kupinga unyanyasaji wa jeshi la kawaida na walikuwa wanahitaji wanajeshi wa kawaida kuwaachia silaha zao," kilisema chanzo kimoja, na kuongeza kuwa takribani watu 15,000 wa Congo wamevuka mpaka na kuingia Burundi. "Bado kuna maofisa wengi wa jeshi la kawaida wanakuja hapa.

Jana, wengi wao waliondoka mjini kwa meli. Waliondoka hapa kuelekea Kalemie, wakipanda meli ya Amani," kilisema chanzo kingine. Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha taarifa hizi kwa uhuru.

Jumatano, mapigano ya silaha na uporaji kwenye mji ulizuia kabisa usafiri, ikiwa ni pamoja na huduma za kibinadamu.

Doctors Without Borders, shirika la misaada ya matibabu, limeomba kulindwa kwa raia, misheni ya matibabu, na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

"Kote mjini, timu za kutoa huduma za matibabu na misaada ya kibinadamu ziko hatarini. Hospitali katika eneo hili zinaendelea kupokea watu walioumia kila siku, ikiwa ni pamoja na raia. Tunahofia kuhusu upatikanaji wa huduma za afya," inasema tamko lililochapishwa kwenye ukurasa wa X wa shirika hilo.

Mwanazuoni na Mkurugenzi wa Kundi la Utafiti la Congo, Jason Stearns, ambaye pia ni profesa mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Simon Fraser, anasema kuna dalili zote za kuwa huu ni mwanzo wa vita ndefu zaidi.

"M23 wameanza kuweka muundo wa utawala, miundo ya ushuru, na wanaajiri wapiganaji wapya. Wanatembea zaidi ndani ya Congo.

Uvira inaonekana kuwa ni kituo kimoja katika vita ndefu. Wakati huo huo, jeshi la Congo limekuwa katika hali ya kuchanganyikiwa tangu wakati wa mapigano na kutekwa kwa Goma," anasema Stearns.

Anabainisha kuwa ingawa jeshi la Burundi limejiondoa, jeshi la Afrika Kusini liko katika kambi za ndani ya Goma na makandarasi binafsi wameondoka, hivyo "kijeshi, hakuna kitu cha kuzuia M23".

Jumapili iliyopita, M23 ilichukua udhibiti wa mji wa Bukavu, bila upinzani mkubwa kutoka kwa jeshi la Congo na washirika wake. Maisha huko yameanza kurudi kama kawaida, kwa mujibu wa vyanzo, mji ukiwa chini ya udhibiti wa M23.

Mkazi mmoja aliiambia BBC kuwa biashara ndogo, ATM za benki na maduka vimefunguliwa tena. "Tunaweza kutoka nje ya nyumba zetu, watu wanajitahidi kutoka baada ya hasara zilizotokea mwishoni mwa juma. Maisha ni bora sasa… M23 ipo kila mahali," alisema mkazi huyo, akiongeza kuwa AFC/M23 wameatangaza kwamba shule zitafunguliwa Jumatatu.

Mzozo wa miongo mingi una mizizi yake, kwa sehemu, katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994, ambapo takribani watu 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi, waliuawa na wafuasi wa Hutu.

Baada ya hapo, Watu wengi wa Hutu walikimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakiwemo baadhi waliohusika katika mauaji hayo.

Rwanda inasema kuwa bado wamekuwa tishio. Wakosoaji wanasema Kigali ina macho yake kwenye utajiri mkubwa wa madini wa DR Congo, ambao ni muhimu kwa teknolojia nyingi duniani, ikiwemo kompyuta mpakato na simu za mkononi.

Hata hivyo, Kigali inakanusha tuhuma zinazosema inaunga mkono waasi.

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga