Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Corneille Nangaa: Kutoka kuwa mkuu wa uchaguzi DRC hadi kuongoza waasi wa M23
Kama umekuwa ukifuatilia habari za hivi karibuni kuhusu mzozo wa kivita kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23, hasa baada ya waasi hao wanaungwa mkono na Rwanda kuuteka mji wa Goma bila shaka jina la Corneille Nangaa halitakuwa geni masikioni.
Kauli zake kali zimekuwa zikigonga vichwa vya habari hususan pale aliposema, "Lengo letu [la mapigano] si Goma wala Bukavu bali Kinshasa, chanzo cha matatizo yote."
Akiwa mkuu wa muungano wa Congo River Alliance (CRA) ambao ni washirika wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, Corneille Nangaa Yubeluo ameteka miji muhimu ya mashariki mwa Congo, ikiwa ni pamoja na mji muhimu wa Goma.
Nangaa, si Mtutsi na wachambuzi wanasema analeta sura tofauti zaidi ya Wakongo kwenye kundi hilo.
Sio mgeni katika siasa za DRC. Mwaka 2015 aliteuliwa kuwa mkuu wa Tume ya uchaguzi ya DRC chini ya utawala wa Rais Joseph Kabila na mwaka 2018 aliongoza uchaguzi uliogobikwa na utata wa wizi wa kura uliomuweka madarakani rais wa sasa Felix Chilombo Tschisekedi.
Kwanini Nangaa aliuasi utawala wa Kinshasa?
Baada ya kuondolewa madarakani kama mkuu wa tume ya uchaguzi mnamo 2021, Nangaa alionekana kutofurahia uamuzi huo. Alisema atagombea urais katika mwaka 2023 lakini, baada ya mabishano ya hadharani na Rais Tshisekedi kuhusu madai ya makubaliano ya awali yanayohusishwa na uchaguzi wa 2018, na akatangaza kuunda muungano wa kumuondoa madarakani Rais wa DRC.
Aidha kutoelewana na mamlaka ya Congo, ikiwa ni pamoja na mzozo kuhusu kibali cha uchimbaji madini, kulimfanya Nangaa kukimbilia uhamishoni nchini Kenya. Mnamo 2023, alijiunga na Congo River Alliance, muungano wa kisiasa na kijeshi ukijumuisha vyama 17 na vikundi vya waasi vinavyopinga serikali ya Tshisekedi na kuwa mwanasiasa mkuu wa muungano huo.
Kando na uchimbaji madini, malalamishi yake pia yanaaminika kuwa yanatokana na kukataa kwa Rais Tshisekedi kukataa kumtetea ili Marekani imuondolee Nangaa kwenye orodha yake ya vikwazo, kulingana na Christian Moleka, mtaalamu wa siasa katika taasisi ya wataalam ya Dypol Congo. "Mtazamo wake kwamba alitendewa vibaya na mamlaka ndio ulimsukuma kuelekea kwenye siasa kali," Moleka aliliambia shirika la habari la AP.
Nangaa ambaye alizaliwa tarehe 9 Julai 1970 katika eneo ambalo kwa sasa linaitwa Mkoa wa Haut-Uele nchini DRC, alianza kazi yake mbali na uwanja wa vita. Alisomea uchumi katika Chuo Kikuu cha Kinshasa kabla ya kufanya kazi na mashirika ya kimataifa, likiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
'Nafasi ya Nangaa katika M23'
Ushirika wa Nangaa na M23 umeonekana kuwa wa faida kwa waasi hao kwa kuleta sura ya kisiasa ndani ya kundi hilo la wapiganaji, kutokana na uzoefu wake wa siasa wa kuurai umma wa Wakongo kuwaunga mkono waasi hao.
Kauli zake kali na za moja kwa moja kwa serikali ya Kinshasa zimemfanya kuwa maarufu kwa baadhi ya Wakongo, vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa.
Katika mkutano na waandishi wa habari kutoka Goma, alisisitiza kwamba Tshisekedi hajawahi kushinda urais kihalali na akasema: "Ikiwa nimemuunda mnyama huyu, nadhani ni juu yangu kumshinda." Yeye na washirika wake wameweka wazi kuwa lengo lao kuu ni kunyakua mamlaka huko Kinshasa.
''Baadhi ya Wakongo wanamuamini kwasababu ametoka upande wa serikali, wanamsikiliza sana …wanasema anajua siri za serikali kwasababu amekuwa upande wa serikali,'' mmoja wa wakimbizi wa kutoka eneo la Bunia DRC anayeishi Nairobi kwa sasa ameiambia BBC.
Mkakati wake unaonekana si wa kijeshi tu bali pia ni wa kisiasa na anatafuta kuungwa mkono zaidi na jamii ya Watutsi ambayo kihistoria inahusishwa na M23.
Kupanda mamlaka?
Mafanikio ya Mchumi huyu yalianza mwaka 2015 alipoteuliwa kuwa rais wa Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi (CENI) chini ya rais wa wakati huo Joseph Kabila.
Aliwajibika kuandaa uchaguzi uliocheleweshwa wa 2018 na akamtangaza Félix Tshisekedi mshindi kwa njia ya kutatanisha. Muda wake katika CENI uliisha mwaka wa 2021 huku kukiwa na madai ya udanganyifu katika uchaguzi na vikwazo vya Marekani kwa "kuhujumu uchaguzi wa DRC ".
Kwa nini aliigeuka dhidi ya serikali ya Congo?
Awali akihusishwa na wasomi wa nchi hiyo ndani ya utawala, lakini baadaye Nangaa alijitenga na Rais Tshisekedi. Kabla ya uchaguzi wa 2023, Nangaa alisema kuwa matokeo ya 2018 yalibadilishwa katika makubaliano ya siri kati ya Tshisekedi na Kabila, jambo ambalo Tshisekedi anakanusha.
Mnamo Agosti 2023, Nangaa aliibuka tena kama mhusika mkuu katika mizozo ya kivita ya DRC, akizindua CRA - muungano wa vyama 17 vya kisiasa, vikundi viwili vya kisiasa na wanamgambo wenye silaha. Miongoni mwao lilikuwa ni March 23 Movement (M23), kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda. Nangaa amejiweka katika nafasi ya kiongozi katika uasi dhidi ya serikali ya Tshisekedi.
Mzozo huo umesababisha vurugu kubwa, huku zaidi ya watu 100 wakiuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa. Hospitali za Goma zimezidiwa, na jiji linakabiliwa na uhaba wa maji na umeme.
Juhudi za kidiplomasia za kukomesha mapigano zimepiga hatua kidogo, na vyombo vya kikanda kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) vinajadili iwapo vitaondoa vikosi vyao vya kulinda amani.
Kuhukumiwa kifo
Mnamo Agosti 2024, mahakama ya kijeshi huko Kinshasa ilimhukumu Nangaa, pamoja na viongozi kadhaa wa M23, kifo bila kuwepo mahakamani baada ya kuwatia hatiani kwa mashtaka ya uhaini, uhalifu wa kivita na uasi.
Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) ziliweka vikwazo dhidi yake na muungano wake kwa "kuchochea ukosefu wa utulivu" na kujaribu kuipindua serikali ya Kongo.
Licha ya hukumu hiyo, Nangaa anaendelea kufanya kazi kwenye uwanja wa vita. Muungano wake unapanua ushawishi wake zaidi ya Kivu Kaskazini, huku ripoti zikisema analenga kupanua shughuli zake hadi eneo la kusini-mashariki lenye utajiri wa madini, hususn Katanga, ambako upinzani wa kisisasa dhidi ya Tshisekedi ni mkubwa.
Muungano anaouongoza Nangaa sasa unasonga mbele kuelekea katika mji wa Bukavu, huku Umoja wa Mataifa ukiendelea kuripoti kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika maeneo ya Mashariki mwa DRC, hususan katika mji wa Goma baada ya kudhibitiwa na waasi. Umoja wa Mataifa unasema watu takriban 7,000 wameyakimbia makazi yao katika mji huo.
Imehaririwa na Athuman Mtulya