Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mtu mwenye haya asiyefaa kuwa mwanasiasa: Errol Musk baba wa Elon azungumza kuhusu mwanaye
Na Maria Jevstafjeva
BBC Russian
Elon Musk ndiye mtu tajiri zaidi duniani, mjasiriamali wa teknolojia aliyeweza kuwa na uhusiano na na kuingia kwa njia ya kipekee katika ofisi za juu zaidi za mamlaka ya kisiasa. BBC ilizungumza na baba yake Musk, Errol, ili kupata ufahamu kuhusu maisha ya utotoni ya Elon, na jinsi maisha hayo yalivyomuandaa kuwa mtu ambaye wengine wanamuita "rais asiye rasmi wa Marekani".
"Alinitumia pesa za kununua ndege ya injini mbili ambayo ninataka kuinunua," anasema Errol, akielezea mara ya mwisho alipokutana na mtoto wake mwenye ushawishi. "Mimi ni mfupi kidogo na kwahivyo alinitumia pesa ili niweze kununua. Kwa hivyo nilisema tu 'asante'."
Anasema mazungumzo hayo yalitokea siku moja kabla ya mahojiano yetu.
Errol Musk anajiunga nami kupitia Zoom kutoka jumba lake la kifahari la pwani karibu na Cape Town, akionekana ametulia na kujiamini. Nilikuwa nimewasiliana naye wiki kadhaa mapema kwa mahojiano kuhusu maisha ya utotoni ya Elon na nilishangaa alipojibu tu, "Sawa," siku iliyofuata.
Alizaliwa mnamo 1971 katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, Elon alilelewa na baba na mama yake mhandisi, Maye, mwanamitindo. Baada ya talaka ya wazazi wake, aliishi na Errol nchini Afrika Kusini kabla ya kuhamia Canada mnamo 1989.
Kulingana na Errol, Elon alikuwa "mvulana mzuri sana, asiye na shida" ambaye kila wakati alipata kile alichotaka. Anasema kila wakati alijua mtoto wake ataweka bidii hadi atakapokuwa "nambari moja".
Leo, Elon anaendesha Tesla, SpaceX, na X (zamani Twitter, na sasa anaanzisha AI). Jarida la The Wall Street Journal ilikadiria utajiri wake kuwa $419.4bn mwezi Februari.
Pia amekuwa mmoja wa washauri wanaoonekana zaidi wa rais wa Marekani na mkuu wa Idara mpya iliyoundwa ya Ufanisi wa Serikali (DOGE).
Machungu katika kukua kwake
Uhusiano wa Elon na baba yake umekuwa mgumu kwa muda mrefu, na alielezea utoto wake kuwa mbaya kwa mwandishi wa wasifu wake Ashlee Vance. "Unafukuzwa na magenge shuleni, kisha urudi nyumbani, na huko hali inakuwa mbaya pia," alisimulia.
Katika wasifu mwingine, kaka ya Elon Kimbal alimwambia Walter Isaacson kwamba baba yao aliwatukana wakiwa watoto. "Alikuwa akiwafokea kwa sauti kali, akikufundisha kwa masaa mengi – akikwambia huna thamani, mwenye maoni mabaya juu yako."
Katika mahojiano ya 2017, Elon alifikia hatua ya kumwita baba yake "mwanadamu mbaya". Errol anasema hajui kwa nini Elon angesema hivi. "Ninazungumza naye mara nyingi sasa. Nina hakika kwa baada ya muda ataweza kusema samahani."
"Kumbuka kwamba wavulana pia wanashindana kwa kiasi fulani na baba yao," anaongeza.
Errol hakubali kwamba utumishi wake wa kijeshi ulimshawishi, ingawa. "Uliambiwa uko chini kuliko na ilibidi ufanye kazi kwa bidii. Na hilo limewafanya kuwa wanaume wenye nguvu," anasisitiza.
Errol na Elon wanafanana sana: wote ni wafanyabiashara, wote wanachukuliwa kuwa watu wenye utata na wote wana watoto wengi. Errol ana saba, wakati Elon anaaminika kuwa na 14.
Errol amemkosoa mtoto wake kwa kuwapuuza baadhi yao kwasababu ya kazi, lakini anasisitiza kuwa alijaribu kutoa kipaumbele sawa kwa watoto wake wote.
Wakati wa mahojiano, hata hivyo, Errol anasahau kwa muda mfupi mmoja wa watoto wake mwenyewe, binti yake wa nne, ambaye mama yake ni binti yake wa kambo wa zamani, Jana Bezuidenhout. Jana aliingia katika familia ya Musk akiwa na umri wa miaka minne, wakati Errol alipomuoa mama ya Jana, Heide.
Ninashangaa wakati Errol mwanzoni anasema ana binti watatu, na kujirekebisha muda mfupi baadaye. Kisha anaongeza kuwa "anaendelea kumsahau (binti wa nne)", akicheka vibaya.
Mtoto wa kwanza wa Jana na Errol alizaliwa akiwa na umri wa miaka 30 hivi, na Errol alikuwa na zaidi ya miaka 70. Tangu wakati huo wamepata mtoto wa pili, lakini hawako pamoja tena.
Uchumba wao uliripotiwa kusababisha mpasuko kati ya Errol na Elon, ingawa Errol anasema wamerejea kwenye mazungumzo.
Siasa na matusi
Ninamkumbusha Errol wakati Elon alimtukana hadharani waziri wa mambo ya nje wa Poland, akimwita "mtu mdogo". Je, ana wasiwasi anapomuona mwanawe akiwaudhi watu hadharani?
"Nina wasiwasi sana juu ya kila neno ambalo Elon, au mtoto yeyote, anatamka, kwa kuhofia kwamba wanaweza kujiingiza kwenye matatizo," Errol anasema.
"Tangu alipokuwa mdogo sana, nilikuwa nikimuambia, huwezi kuwaambia watu wazima kuwa ni wajinga," Errol anakumbuka. "Na angesema, 'Kwa nini? Ni wajinga.' Na nilikuwa namwambia , ndio, ni wajinga, lakini huwezi kuwaambia hivyo."
Lakini Errol anaamini kwamba kuna uhuru zaidi katika ulimwengu wa siasa: "Watu wataitana majina siku moja, na kisha siku inayofuata wataungana tena."
Licha ya ushawishi dhahiri wa Elon katika mamlaka, Errol anaamini mtoto wake hafai kwa siasa. "Yeye ni mtu wa teknolojia. Watu wa teknolojia wanataka mambo yawe na maana," anasema, akiongeza kuwa Elon anajitahidi kufanya kazi na kila aina ya watu. "Lazima ufanye kazi na watu ambao wanaonekana kuwa maarufu, lakini wanaweza kuwa wajinga kabisa."
Lakini haya sio maoni ya Errol kwa wanasiasa wote: kuna wengine yeye na familia yake wanawapenda - hasa rais wa Urusi Vladimir Putin.
"Ukimtazama Putin kama mwanamume, sio katika muktadha wa siasa za kimataifa, ni vigumu kutomheshimu," Errol anasema. "Anazungumza kwa akili nzuri sana. Ni vigumu sana kutomuogopa kidogo Bw Putin."
Ninapoumuuliza ikiwa Elon anakubaliana na maoni haya, Errol anathibitisha kwamba anafanya hivyo. Ninapotaja uvamizi wa Putin nchini Ukraine, Errol anasisitiza kwamba "ni wakati tu ndio utakaoonyesha ni nani aliyeianzisha", licha ya ushahidi wa wazi wa uchokozi wa Urusi.
Wakati wa mahojiano, Errol anacheka vicheko kadhaa , haswa ninapopinga maoni yake ya kisiasa.
Errol anaamini kutoa Starlink kwa Ukraine mapema katika vita ulikuwa uamuzi sahihi, lakini mzozo ulipoendelea, maoni ya Elon yalibadilika. Anakataa madai kwamba mabadiliko ya Elon yalisukumwa na masilahi ya kifedha, akisema, "Familia yetu ina kila kitu - hatuhitaji pesa zaidi." Akizungumza nami kutoka kwenye chumba kikubwa , Errol ananionyesha ishara huku akirudia mara kadhaa, "Tuna kila kitu."
Mahojiano yanapokaribia mwisho, ninamuuliza Errol kile ambacho watu hawajui kuhusu Elon. Errol anasema mtoto wake hana ujasiri anapozungumza hadharani.
"Anahisi aibu. Bado analazimika kujifunza kuwa jukwaani mbele ya umati," Errol anasema.
"Chochote anachosema, anasema haraka iwezekanavyo."