Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini watu wanachoma moto mali za bilionea Elon Musk?
- Author, Na Sammy Awami
- Akiripoti kutoka, BBC News Swahili, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Polisi katika jimbo la Massachusetts nchini Marekani wanachunguza tukio la kuchomwa moto kwa vituo saba vya kuchaji magari aina ya Tesla.
Tesla ni kampuni ya magari yanayotumia umeme. Inamilikiwa na bilionea mfanyabiashara Elon Musk, ambaye pia ni afisa mwandamizi katika serikali ya Rais Donald Trump.
Taarifa za awali za uchunguzi wa kipolisi zinasema chanzo cha moto katika vituo hivyo kinaonekana kuwa ni vitendo vya makusudi na si ajali ya kiufundi.
Matukio kama haya yameripotiwa kutokea nchini Marekani, Ufaransa na hata Ujerumani. Siku za hivi karibuni hata magari aina ya Tesla yamekuwa yakichomwa moto pia, huku mwanamke mmoja katika jimbo la Colorado alikamatwa na polisi muda mfupi kabla hajachoma moto duka linalouza magari ya Tesla.
Matukio haya yameunganishwa moja kwa moja na ukaribu wa Musk kwa Trump na uungwaji wake mkono wa siasa na sera zenye misimamo mikali.
Musk ni mmoja wa mabilionea wa Marekani waliokuwa mstari wa mbele kabisa kumuunga mkono Trump wakati wa kampeni za uchaguzi huku akitumia mtandao wake wa 'X' kumnadi Trump na sera zake, kumpinga sera za mpinzani wake na kuhamasisha watu kujiandikisha na kumpigia kura Trump.
Mtandao wa 'X' una watumiaji zaidi ya milioni 600 kila mwezi na Musk ndiye mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao huo.
Bilionea huyu hata aliendesha bahati nasibu na kutoa dola milioni moja kila siku kwa mshindi mmoja aliyesaini tamko linalopigania haki ya kujieleza Marekani. Mchezo huu lakini ulikuwa ndani ya majimbo yenye ushindani mkali pekee kati ya Trump na mpinzani wake Kamala Harris.
Jitihada hizi za Musk na nyingine nyingi zilimkosha sana Trump na kumuweka karibu Musk zaidi, akizunguka nae katika maeneo mengi aliyokwenda na kumtaja katika mikutano yake mingi
Aliposhinda Urais, Trump alimpatia Musk taasisi mpya ijulikanayo kama 'Department of Government Efficiency' au DOGE – yenye lengo la kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ufanisi wa watumishi wa umma.
Moja ya wahanga wakubwa wa taasisi hii ya DOGE ni shirika la msaada wa kimataifa la Marekani USAID, ambalo Musk amedai limefuja pesa nyingi za umma kupitia misaada linayotoa ulimwenguni kote huku akililaumu kuchochea sera za urengwa wa kushoto.
Musk ametaka shirika hili lifutwe kabisa. Kufikia hivi sasa, USAID limevunjwavunjwa huku asilimia tisini ya misaada yake imesimamishwa – ambayo ni mabilioni ya dola yaliyokuwa yakitumwa hasa kwa nchi masiki kusaidia miradi kama ya Ukimwi na lishe.
Mfanyabiashara huyu pia anaaminika kuwa kinara wa kuishawishi serikali ya Trump kusitisha misaada yake kwa Afrika ya Kusini huku akidai kwamba serikali ya Afrika Kusini imepitisha seria na sera zinazonyanyasa wazungu wa nchi hiyo.
Wiki mbili zilizopita, DOGE ilituma barua pepe kwa watumishi wa umma wa Marekani ikiwataka waandike barua pepe kuelezea kile walichokuwa wamekifanya ndani ya wiki. Taasisi hiyo ilionya kwamba ikiwa mtu hataandika barua pepe hiyo basi atahesabika kama amejifukuzisha kazi.
Tayari mamia ya maelfu ya watumishi wa umma wamefukuzwa kazi kwa kile kinachodaiwa kuwa aidha nafasi zao hazina tija katika utumishi wa umma au taasisi zao hazina maslahi yoyote kwa umma.
Musk amekuwa mstari wa mbele pia kuunga mkono vyama vya siasa vyenye misimamo mikali nje ya Marekani katika nchi kama Ufaransa na Ujerumani. Ameilaumu Uingereza kwa kuminya haki ya kujieleza na kumuita Waziri mkuu Keir Starmer dikteta.
Misimamo hii ya Musk inaungwa mkono na watu wengi – hasa nchini Marekani kupitia vuguvugu la kisiasa la 'Make America Great Again (MAGA)' lililoibuliwa na Trump.
Hata hivyo, wahafidhina wa kati na wale wanaounga mkono sera za mrengwa wa kushoto wanapinga vikali sera na misimamo ya Musk na kuhoji kiwango cha ushawishi alichonacho Musk katika serikali ya Trump.
Wengi wamekwenda mbali hata kumuita Naibu Rais wakiamini kwamba sera nyingi za serikali ya sasa ya Trump za mambo ya ndani na nje zina chembechembe za ushawishi wa Musk.
Mbali na kuchomwa moto kwa vituo vya umeme, mauzo ya magari aina ya Tesla barani Ulaya kwa mwezi Januari yanaripotiwa kushuka kwa 45%, huku katika nchi kama Ujerumani na Ufaransa mauzo yakishuka kwa 60%.
Wakati baadhi ya wachambuzi wanadhani inawezekana kushuka huku kwa mauzo ni kutokana na watumiaji wa Tesla kujizuia kununua sasa wakisubiri kutoka kwa toleo jipya la Tesla Model Y, wapo wanaoamini kushuka huku kwa mauzo ya Tesla na uchomwaji moto wa vituo vyake vya kuongeza umeme ni matokeo ya ushiriki wa Musk katika siasa na hata uungwaji wake mkono wa siasa zenye misimamo mikali.
Imehaririwa na Dinah Gahamanyi