Je, ni mkwamo kwa Afrika kusini, baada kufungiwa msaada kutoka kwa Trump?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Afrika Kusini inaonekana kuwa kwenye njia panda katika uhusiano wake na Marekani, ambapo uhusiano huo umeanza kuonekana kutetereka kufuatia uamuzi tata wa Rais Donald Trump wa wiki iliyopita wa kukata msaada wa kifedha kwa nchi hiyo.

Trump alisema Afrika Kusini inatekeleza kile alichokiita "vitendo visivyokuwa haki na visivyo na maadili" dhidi ya jamii ya wachache wa kizungu wa Afrikaans na kwa kupeleka kesi ya kigaidi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwezi Desemba 2023.

Hatua hii imeleta mshangao mkubwa nchini Afrika Kusini, huku wataalamu wakihofia kuwa huenda akatumia fursa hii kumaliza upatikanaji wa bidhaa za Afrika Kusini katika soko la Marekani kupitia mpango maalum wa biashara wa Marekani na Afrika uitwao Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (Agoa).

Nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa kirafiki tangu kumalizika kwa utawala wa wachache wa kizungu mwaka 1994, wakati shujaa wa kupinga ubaguzi wa rangi na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Nelson Mandela, alipochaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.

Ingawa ilichukua Marekani miaka 14 zaidi kumtoa Mandela kwenye orodha yake ya "wahalifu wa kigaidi" kwa namna alivyohusika katika kupinga mfumo wa ubaguzi wa rangi, ambao ulianzishwa na watawala wa kizungu wa Afrika Kusini mwaka 1948.

Mivutano ya hivi karibuni ilizuka siku chache baada ya kuapishwa kwa Rais Trump mwezi uliopita, wakati Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliposaini sheria ya Muswada wa Utaifishaji, inayoruhusu serikali kuchukua ardhi bila fidia katika hali fulani.

Hatua ya Trump ilikuja wiki iliyopita alipolisisitiza kuwa atakata msaada wa kifedha katika siku zijazo kwa kile alichokiita "mambo mabaya, mambo ya kutisha" ambayo uongozi wa nchi hiyo unafanya.

Rais wa Marekani aliongeza kwamba Afrika Kusini, bila msingi wowote wa ukweli, ilikuwa "inachukua ardhi" na "ikafanya mambo ambayo huenda yakawa mabaya zaidi kuliko hayo".

Alisisitiza msimamo wake mbele ya majibu makali kutoka kwa serikali ya Afrika Kusini na kusaini agizo la utekelezaji Ijumaa iliyopita kuzuia msaada.

Hii inafikia jumla ya takriban dola milioni 440 ($440m) - kiasi cha msaada kilichotengwa mwaka 2023 - ingawa ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini ulisema baadaye kwamba fedha kutoka Pepfar, mpango wa Marekani unaopambana na kuenea kwa HIV duniani, hautaathirika, huku wakiongeza kuwa "si shughuli zote za Pepfar zitakazoendelea".

Afrika Kusini ni mojawapo ya wapokeaji wakubwa wa Pepfar, inayochangia takriban 17% kwenye mpango wake wa HIV/Aids ambapo takriban watu milioni 5.5 wanapokea dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI.

Katika agizo lake la utekelezaji, Trump alidai pia kuwa Afrika Kusini ina "shangaza inapopuuza haki za wananchi wake" na kuchukua "msimamo mkali" dhidi ya Marekani na mshirika wake Israel katika kesi yake ya ICJ.

Mbali na kufunga msaada, Trump alitoa pendekezo la kuwasaidia wakimbizi kutoka kwa jamii ya Afrikaans, ambao ni wazungu wengi kutoka vizazi vya wahamiaji wa Kiholanzi na Kifaransa, kuhamia Marekani.

Msimamo wake umeungwa mkono na makundi yenye misimamo ya kihafidhina ya Afrikaans, ikiwa ni pamoja na AfriForum na Solidarity, ambayo yanataka serikali iache sheria inazozita "za ubaguzi wa rangi" kama vile hatua za kutengeneza usawa wa rangi na nguvu ya uchumi kwa watu weusi.

Hii inaendana na maoni ya mshauri wa karibu wa Trump, Elon Musk, bilionea wa teknolojia ambaye alizaliwa Afrika Kusini. Alihoji kwenye mtandao wa X kwa nini Ramaphosa alikubali "sheria za kumiliki ardhi zenye ubaguzi wa wazi".

Hii si mara ya kwanza kwa sera ya mageuzi ya ardhi ya Afrika Kusini kumkasirisha Trump.

Mnamo 2018, wakati wa urais awamu ya kwanza ya urais wake, alidai mamlaka za Afrika Kusini kuwa zinahusiana na "uuaji wa wakulima kwa wingi" na kumtaka waziri wake wa zamani wa masuala ya kigeni kuchunguza suala la serikali "kuchukua ardhi kutoka kwa wakulima wazungu".

Wakati matamshi ya Trump yakizua upinzani wakati huo, Dkt. Oscar van Heerden, mchambuzi wa kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Johannesburg, aliiambia BBC kuwa "hakukuwa na hatua kali kama hii iliyochukuliwa hadi kufikia hatua ya kusaini agizo la utekelezaji."

Kwa sasa, uhusiano wao uko katika hali tete - kila nchi inajiandaa kwa hatua yake ijayo.

Katika sekta ya biashara, Donald MacKay, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri ya biashara ya XA Global Trade Advisors yenye makao yake Johannesburg, alisema kuwa ingawa Marekani ni mojawapo ya washirika wakubwa wa biashara wa Afrika Kusini, siyo "mshirika wake wa karibu zaidi katika biashara."

Afrika Kusini inauza madini mbalimbali kwa Marekani, ikiwa ni pamoja na platini, chuma, na manganizi.

Pia ni moja ya wauzaji wakubwa chini ya Agoa, ikizalisha takriban dola bilioni 2.7 ($2.7bn) mwaka 2023, hasa kutoka kwenye mauzo ya magari, vito vya mapambo, na madini.

Unaweza pia kusoma

"Kwa miaka mingi, uhusiano huo umekuwa na mabadiliko ya kupanda na kushuka. Haujawahi kuwa na nguvu sana [tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu wachache Afrika Kusini]. Lakini wakati huo, pia sidhani kama ulidhoofika kama ilivyokuwa katika miaka ya hivi karibuni na sidhani kama ni kosa la Afrika Kusini," Bwana MacKay aliiambia BBC.

Hata hivyo, alikiri kuwa Afrika Kusini imefanya "mengi" katika miaka ya hivi karibuni kumkera Marekani.

"Usumbufu huu unajikusanya na chini ya Rais Trump... hii inaonekana kama fursa ya kuiweka Afrika Kusini mahali pake."

Dkt. Van Heerden aliielezea kama mabadiliko ya muktadha huo kwa sehemu kuwa "mabadiliko ya kimataifa" na "ushindani mpya unaoikabili Marekani" kutoka kwa nchi kama China, India, na Brazil.

Wakati wataalamu walizungumzia manufaa ya Agoa, ambayo itakaguliwa mwishoni mwa mwaka huu, walikubaliana kwamba athari yake huenda isiwe kubwa kama baadhi wanavyohofia.

Agoa ilianzishwa mwaka 2000 na inatoa kwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara upatikanaji wa bila ushuru wa bidhaa zaidi ya 1,800 za Marekani.

Bwana MacKay alisema atashangaa kama Afrika Kusini itaendelea kunufaika na makubaliano haya baada ya uhakiki.

"Hisia zangu ni kwamba, kwa sababu yoyote ile ambayo Trump amekasirikia Afrika Kusini, kwa sasa Agoa itakuwa ni njia rahisi ya kuitia adabu Afrika Kusini."

Dkt. Van Heerden aliongeza kwamba hata kama makubaliano hayo hayata huishwa, au Afrika Kusini ikatengwa, biashara zinazofaidika kwa sasa nazo zitapata hasara za muda mfupi lakini zitajikwamua katika miaka michache.

Alisema kwa sasa serikali ya Rais Ramaphosa inachagua njia ya kidiplomasia - ingawa ukosefu wa maslahi wa utawala wa Trump katika diplomasia unapunguza sana nafasi ya mafanikio.

Hii labda haijasaidiwa na jibu la moja kwa moja la Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola Jumatano kwa hatua ya Trump, akisema kuwa "hakuna namna" kwamba Afrika Kusini itaondoa kesi yake dhidi ya Israel katika mahakama ya ICJ.

"Kusimamia misingi yetu wakati mwingine kuna madhara, lakini tunabaki imara kwamba hili ni muhimu kwa dunia, na sheria ya kimataifa," Lamola aliiambia Financial Times.

Afrika Kusini imelaumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza, shutuma ambazo Israel inakanusha.

Kwa upande mwingine, Ramaphosa, katika nafasi yake kama rais wa G20, ametangaza kwamba atatuma ujumbe ulimwenguni kote kufafanua sera za ndani na za nje za Afrika Kusini - na Washington ikiwa ni kituo muhimu.

Afrika Kusini ilichukua urais wa G20, kundi la nchi zinazokutana kujadili masuala ya kiuchumi na kisiasa ya kimataifa, mwezi Disemba mwaka jana, ikiwaona kama fursa ya kuongeza hadhi yake kimataifa.

Lakini, katika kile kinachotazamwa kama dhihaka kwa Afrika Kusini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ametangaza kwamba hatashiriki mkutano wa G20 wa mawaziri wa mambo ya nje utakaofanyika wiki ijayo Johannesburg.

"Kazi yangu ni kuendeleza maslahi ya kitaifa ya Marekani, siyo kupoteza pesa za walipa kodi au kulea chuki dhidi ya Marekani," alisema.

Afrika Kusini ni sehemu ya Brics, muungano wa nchi kubwa zinazoendelea ikiwemo Brazil, Urusi, India, na China, zinazojaribu kupinga nguvu za kisiasa na kiuchumi za mataifa tajiri ya Amerika ya Kaskazini na Ulaya Magharibi.

Bwana MacKay anaamini itakuwa vigumu kwa Afrika Kusini na mataifa mengine kusimamia uhusiano na Marekani chini ya "siasa isiyotabirika zaidi duniani", akionyesha kuwa itabidi waanze kuiangalia Brics kama mshirika mbadala.

Lakini jambo muhimu kwa Afrika Kusini, Umoja wa Ulaya (EU), mojawapo ya washirika wake wakubwa wa kibiashara, umeimarisha msaada wake kwa nchi hiyo.

António Costa, rais wa Baraza la Ulaya - ambalo linaweka mwelekeo mkuu wa kisiasa na vipaumbele vya EU - aliandika kwenye mtandao wa X Jumatatu kwamba alizungumza na Ramaphosa kwa njia ya simu ili kuonyesha "kujizatiti kwa EU katika kuimarisha uhusiano na Afrika Kusini".

Ikiwa jitihada za Afrika Kusini za kuvutia zisifanye kazi, Dkt. Van Heerden anapendekeza serikali inaweza kuchagua "kujadiliana kwa nguvu" na kutumia madini inayoyatoa kwa Marekani kama "kadi ya kubadilishana".

Lakini anatoa onyo: "Afrika Kusini itabidi itafakari kwa makini jinsi wanavyocheza mchezo huu [ambapo] hatua ya kwanza tayari imechezwa na Rais Trump na Elon Musk."

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Sarana na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi