Siasa za Afrika upinzani au uadui?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika kipindi cha baada ya ukoloni, mataifa mengi ya Afrika yalitazama demokrasia kama mwanga wa matumaini mfumo unageuza nchi kuwa sehemu ya majadiliano ya kitaifa, kushirikisha raia wote na kuipa serikali wajibu wa kuwajibika kwa walio madarakani. Upinzani ulikuwa sehemu muhimu ya mfumo huo, ukitarajiwa kuwa sauti mbadala inayosimamia masuala ya uwazi, haki na utawala bora. Kwa dhana hii, uwepo wa upinzani haukutazamwa kama uadui, bali kama sehemu ya kiini cha demokrasia yenye afya.

Lakini safari ya siasa za Afrika imekuwa tofauti na matumaini hayo. Katika nchi nyingi, upinzani umegeuzwa kuwa tishio linalopaswa kuzimwa badala ya kuwa mshirika wa maendeleo.

Kwa mwanasiasa wa upinzani katika maeneo mengi ya bara, kuingia katika siasa ni sawa na kuweka maisha rehani. Wengi hawana uhakika na kesho yao. Wengine wameshambuliwa, wengine wamefunguliwa mashtaka, na wengine wametoweka katika mazingira yenye utata. Na wakati huu ambapo vyama vya upinzani vinashinda uchaguzi katika mataifa kadhaa, mvutano kati ya utawala na wapinzani umeongezeka maradufu.

Katika makala hii tunachunguza hali ya upinzani barani Afrika inayoibua swali la siasa za Afrika upinzani au uadui?

Maswahibu ya wapinzani Afrika

Athari za kisiasa kwa wapinzani katika nchi nyingi za Afrika zimekuwa nzito, zenye historia ya kukamatwa, kushambuliwa, na kufunguliwa mashtaka yenye utata. Moja ya mifano ya wazi iko Rwanda, ambako kiongozi wa chama cha upinzani ambacho hakijasajiliwa, Victoire Ingabire Umuhoza, alikamatwa tena mwezi Juni 2025 akiwa nyumbani kwake Kigali. Mamlaka zilidai kuwa anakabiliwa na tuhuma za "kuunda kikundi cha uhalifu" na "kupanga shughuli zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani." Ingabire, ambaye tayari aliwahi kufungwa kwa miaka minane kati ya 2010 na 2018 kwa tuhuma ambazo mashirika ya haki za binadamu yalizitaja kama za kisiasa, alikuwa anahudhuria kesi inayowahusu wanachama wa chama chake. Hata hvyo serikali ya Rwanda inashikilia msimamo wake kwamba amefanya makosa, haonewi.

Hali kama hiyo imewahi kushuhudiwa Uganda kwa muda mrefu. Mwanasiasa mkongwe wa upinzani, Dr. Kizza Besigye, amekamatwa zaidi ya mara 100 katika kipindi cha miaka 20, mara nyingi akituhumiwa kwa "kuchochea maandamano" au "kujaribu kuvuruga utulivu."

Uganda pia inashuhduia anayopitia kiongozi kijana wa upinzani, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine), ambaye alikamatwa mara kadhaa, na mara nyingine polisi walivamia ofisi za chama chake wakidai "kuwatafuta wahalifu", hatua ambayo wachambuzi wa kisiasa waliitaja kama jitihada za kudhibiti upinzani.

Tanzania pia imekuwa katika orodha ya nchi zinazoangaliwa kwa karibu. Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema na mwanasiasa wa upinzani mwenye historia ndefu ya kukosoa serikali, yuko ndani kwa makosa ya uhaini na uchochezi. Hili liliibua hisia nzito nchini humo, hasa baada ya kumbukumbu ya mwaka 2017 ambapo Lissu alipigwa risasi zaidi ya 16 katika tukio ambalo halijawahi kupata ufumbuzi kamili.

Kiongozi wa zamani wa chama hicho, akiwemo Freeman Mbowe, aliwahi kukaa jela kwa tuhuma za ugaidi kabla ya kesi yake kufutwa. Katika matukio tofauti, viongozi wengine wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara akiwemo makamu mwenyekiti wa chama hicho John Heche.

Hali kama hii imekuwa ikijirudia katika nchi kama Zimbabwe, DRC, Cameroon na nyingine. Katika mifano yote hii, mtazamo mmoja unajitokeza: katika nchi nyingi za Afrika, tofauti za kisiasa zimegeuzwa kosa, na upinzani umepewa nafasi ya adui wa serikali badala ya mshindani kisiasa.

Ingawa upande wa serikali kwa nchi zote, wakati wote wameeleza hawamuonei mtu, wapinzani wanafanya makosa ambayo yanawatia matatani.

Upinzani uadui? utawala malaika?

Uhusiano kati ya utawala na upinzani katika Afrika mara nyingi umejengwa juu ya woga na kutokuaminiana. Katika baadhi ya nchi, chama tawala hujiona kama chama pekee halali, na ukosoaji wa serikali huchukuliwa kama hujuma dhidi ya taifa. Matokeo yake ni mazingira ambayo upinzani hauonekani kama sehemu ya mustakabali wa taifa bali kama tishio linalopaswa kudhibitiwa.

Yanaayotokea katika nchi za afrika Tanzania imekuwa mfano wa mgawanyiko huu, na yanahitimisha kuhusu namna watawala wanavyojichukulia ama kuwachukulia wapinzani. Na namna pia wapinzani wanavyowachukulia watawala.

Upande mmoja unajiona malaika, na ndiyo maana hawakamatwi, kushambuliwa wala kuzuiwa kwa shughuli zao za kisiasa na upande wa pili unajiona adui, unaoonewa kila kukicha.

Kwa ujumla, hali hii inazidisha taswira kwamba utawala ni "malaika wasioguswa," na upinzani ni "waovu" ambao hawapaswi kuwepo. Huu ni msingi dhaifu wa siasa kwa sababu unapovunja nafasi ya upinzani, unavunja pia misingi ya uwajibikaji na uwazi.

"Siasa si uadui, lazima pande zote zitizame namna bora ya kufanya siasa, upinzani uheshimu sheria na utawala uheshimu sheria, bila kuonea mtu", kuheshimu sheria hapa ndiyo muarobaini", anasema mmoja wa wachambuzi wa siasa za Afrika.

Nini cha kujifunza kutoka dunia nyingine

Dunia nyingi zenye demokrasia imara zimejenga utamaduni wa kuheshimu upinzani kama sehemu muhimu ya utawala. nchini Uingereza, kwa mfano, kila wiki Waziri Mkuu hukabiliwa na maswali ya moja kwa moja kutoka kwa kiongozi wa upinzani, linalofanyika pia Tanzania, kwa kuwepo kwa maswali kwa waziri mkuu.

Lakini kwa Uingereza, husikii mpinzani anapitia maswahibu ya aina ya wanayopitia wapinzani Afrika. Muhimu serikali na upinzani kuhojiana kila wasaa ili kuwa na muelekeo mmoja kama taifa na kuondoa hofu ya upinzani ni uadui.

Nchini Marekani, licha ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa, matamshi ya ukosoaji hayatafsiriwi kama misingi ya kufungua mashtaka ya jinai. Bunge na mahakama zinatoa nafasi kwa hoja tofauti, na upinzani ni sehemu ya mchakato wa kutengeneza nchini.

India, taifa kubwa la kidemokrasia, limejenga utamaduni wa wanasiasa kukosoana hadharani lakini kushirikiana katika masuala ya kitaifa yote ikiwemo ya maendeleo na usalama wa taifa. Upinzani unapewa nafasi bungeni ama wawe na hoja kali kwa serikali ama laini, haijarishi, na hata mchakato wa kutengeneza sera unajumuisha maoni ya pande zote.

Afrika inaweza kujifunza kutokana na mifano hii kwamba kuheshimu upinzani si udhaifu wa serikali bali ni nguvu ya utawala wa kisasa. Lakini pia upinzani kuheshimu mamlaka inaonyesha ukomavu wa kisiasa. Demokrasia ya kweli inaishi kwa kuwepo kwa hoja mbadala, sio ukimya.